Sunday 19 November 2006

SMZ iamke sasa...

Kisiwa cha Zanzibar ni kidogo sana,hata hivyo kimejaliwa kuwa na mambo mengi sana kiasi cha kuwa kivutio cha aina yake!Anyway sina haya ya kueleza mengi kuhusu kisiwa hicho...

Kitu ambacho nataka kuzungumzia ni juu ya utunzaji wa mazingira na hasa sehemu ambazo wanaishi wazenj wenyewe. Makaazi ya wanavisiwa hao na hasa wale waishio maeneo ya Ng'ambo sio ya kuridhisha kabisa. Na hapana shaka yoyote kuwa Halmashauri ya mji wa Zanzibar inashindwa kuuweka eneo hilo katika hali ya usafi inayostahili.

Cha kusikitisha zaidi, wananchi wa maeneo hayo wanapotaka kujiondolea kero zao kwa upande mmoja wanakutana na pingamizi na Halmashauri hiyo, na kufanya juhudi zao kutozaa matunda yoyote.

Hapa nina mfano wa mradi ambao ulifunguliwa ili kusafisha na kutunza mazingira ya wadi ya Mkele. Mradi huo kwa sasa umekufa na tatizo la uchafu wa mazingira ukiendelea. Kinachosikitisha zaidi ni sababu za msingi ambazo zimepelekea kufa kwa mradi huo ambao ulitazamiwa kuwa ni mradi dila katika kuondoa kero za mazingira machafu ambao unasimamiwa na wananchi wenyewe.

Moja ya sababu kubwa ya kufa kwa mradi huo ni kwa manispaa ya zanzibar kutoachia maeneo ambayo yangeweza kuingiza kipato ili mradi huo uweze kujiendesha. Labda hapa nieleze kwa ufupi aina ya mradi huo. Huu ulikuwa ni mradi wa ukusanyaji na utupaji wa taka, ambapo wananchi waliokuwa akipata huduma hii ilipaswa kuchangia gharama za ukusanyaji na utupaji wa taka hizo. Maeneo yote ya wadi yaliorodheshwa katika mradi huu.. nikiwa na maana ya sehemu za kuishi na zile za biashara.

Hata hivyo Manispaa ilikata kutua maeneo ya biashara yaliyopo kwenye eneo la mradi huu ingawa mradi ulikuwa ukisafisha maeneo hayo vile vile. Kukosekana kwa mapato toka katika maeneo ya wanafanya biashara, ambao kwa kiasi kikubwa ndio wazalishaji wakubwa wa taka, kulizoretesha kabisa mapato ya mradi huo. Ikumbukwe kuwa wafanyabiashara hao nao walitiwa hesabuni kama ndio sehemu kubwa ya kupatikana kwa mapato ya mradi huo kabla ya kuanza. Hata hivyo Manispaa ilikataa kabisa kuachia maeneo ya wafanyabiashara kuhudumiwa na mradi huo.

Sababu nyingine ni migongano ya viongozi juu ya kuendesha mradi huo. Viongozi wa kisiasa katika eneo hilo walitumia mradi kujionyesha kwa viongozi wenzao na wananchi kwa ujumla, hii ilijenga vita vya ndani kwa ambavyo lengo lilikuwa ni kuzolotesha mradi mzima...na lengo hilo limefanikiwa.

Wakati wote huu wa mvutano juu ya uendeshaji wa mradi huu serikali kuu SMZ ilika kimya tu, pamoja na kuwa wao pia walichangia kiasi fulani kuanzishwa kwa mradi huo. Ukaaji kimya wa SMZ pengine ulitokana na kutotambua kero za wananchi juu ya taka, au tu ilitaka kuridhisha upande mmoja(manispaa) na kuacha mradi ukifa kwa matatizo ambayo yalikuwa yanawezekana kutatuliwa pasipo bughuza zozote.

Ili hali ya mazingira iwe nzuri kisiwani huko ni vema SMZ sasa wakaamka na kuheshimu maamuzi ya wananchi. Sio vema SMZ kuchangia kuanzishwa kwa miradi na kushindwa kuona miradi hiyo ikisimama yenyewe na kuendelea. Ubinafsi miongoni mwa watendaji wa SMZ, vita kati ya viongozi wa kisiasa ni mambo ambayo yanatakiwa kupigwa msasa na hasa kwenye suala zima Utunzaji wa Mazingira.

Ni jambo la aibu sana kwa kisiwa hicho kuwa kichafu kiasi cha kusababisha ugonjwa wa kipindupindu, ambao haukuwepo miaka ya huko nyuma!

No comments: