Monday 25 December 2006

Shirika la Meli Zanzibar: Kulikoni?

Imelipotiwa hivi karibuni kuwa Meli ya Mv Maendeleo ilishindwa kuendelea na safari yake kuelekea Pemba ikiwa inatokea Zanzibar. Tatizo lilikuwa ni kuzimika kwa injini yake. Kabla ya kuanza kwa safari hiyo, injini ya meli hiyo ilishindwa kuwaka, hata baada ya kuwaka safari ya kwenda Pemba haikukamilika kwani meli hiyo ilisimama na kubidi kulaza abiria wote ndani ya meli hiyo umbali mfupi tokea katika Bandari ya Malindi Zanzibar.
Kushindwa kuendelea kwa safari hiyo kulizua kero kubwa kwa abiria ambao licha ya kutofika safari yao, iliwalazimu kulala ndani ya meli hiyo katika mazingira magumu, huku hali ya bahari ikiongeza ugumu wa kukesha katika chombo hicho.
Shirika la Meli la Zanzibar ni mojawapo wa mashirika yanayotoa huduma ya usafiri baharini katika visiwa vya Zanzibar, aidha zaidi ya kusafirisha abiria wanahudumia pia usafirishaji wa mizigo na mafuta ya magari. Shirika hilo ndio kongwe katika usafiri wa baharini na lenye vyombo vikubwa.
Tokea kuanzishwa kwake limekuwa tegemeo kubwa kwa usafiri, kabla ya kuingia kwa mashirika binafsi katika sekta hiyo. Hata hivyo mafanikio yake yamekuwa ni kidogo au pengine kutokuwepo kabisa. Shirika hilo limeshauza baadhi ya meli zake, lakini haijawahi kuongeza meli nyingine yoyote licha ya kuendeshwa kibiashara. Meli zake zote ni mbovu na pamoja na kutumia gharama kubwa kuzifanyia matengenezo bado zimekuwa zikiendelea kuwa mbovu na mbovu zaidi.
Meli zake za abiria zote mbili yaani Mv Mapinduzi na Mv Maendeleo zimeshawahi kuzuiwa kuingia katika Bandari ya Dar es Salaam kutokana na kushindwa kukamilisha taratibu za kiusalama zinazohusu vyombo vya baharini. Hata hivyo zimekuwa zikiruhusiwa tena kuingia katika bandari hiyo kwa sababu ambazo hata mimi sijaweza kuzifahamu. Zaidi ya kutokuwa na mfumo unaotakiwa wa usalama meli hizo zimechakaa na kuchoka hasa upande wa injini zake. Hazina uwezo wa kufanya safari kwa miezi mitatu mfululizo pasipo kuharibika injini zake.
Uchakavu wa meli hizo unatokana na kutumika kwa muda mrefu na kwa upande mwingine ni kutokana na hujuma zinazofanywa na wafanyakazi wa meli hizo. Kuna hujuma nyingi zinazofanywa na wafakazi hao kuanzia kuuza kwa vipuli hadi mafuta ya meli hizo. Vitendo hivi ufanyika bila kificho na kwa ushirikiano miongoni wa wafanyakazi hao.
Zaidi Shirika hilo baada ya kufanya kazi kwa miaka zaidi ya arobaini na mbili, inawapasa sasa watuonyeshe mafanikio yao kwa kuweza kuwa na vyombo vya uhakika. Miaka chini ya kumi iliyopita Mv Maendeleo iliwahi kukodishwa, na ilikuwa ikifanya kazi vizuri tu, mara baada ya muda wa kukodishwa kwisha meli hiyo imeshindwa kuwa nzima tena. Na kabla ya kukodishwa ilikuwa mbovu. Sasa ni swala la kujiuliza kwanini meli hiyo iliweza kufanyakazi vizuri ilipokodishwa na kwanini inashindwa kufanya kazi chini ya shirika lenyyewe...
Kulikoni?

No comments: