Monday, 25 December 2006

Zenj na visa vya ardhi mwaka huu....

Mwezi wa tatu 2006
Kuna kauli moja iliwahi kutolewa na rais wa awamu ya nne katika SMZ kuwa Zanzibar ni "Njema na kila atakae kuja basi anakaribishwa" Kutokana na kauli hiyo Zanzibar ilishuhudia mabadiliko ya nguvu katika sekta zote kuanzia ya kibiashara,kijamii na kadhalika. Mamia ya watu walianza kufanya biashara wageni wakiongezeka na kuufanya mji wa zanzibar kuwa mdogo kutokana na msongamano wa watu.
Kuingia kwa awamu ya tano kulishuhudiwa na mabadiliko makubwa zaidi,mabadiliko haya zaidi yalikuwa katika kuendeleza ardhi ya zanzibar. Hapa inabidi tukumbuke kuwa ardhi yote ya Visiwa vya Zanzibar ni mali ya serikali. Hivyo ili uweze kuendeleza ardhi hiyo ni shurti uwe na hati ya kumiliki ardhi hiyo toka serikalini. Katika awamu ya tano kulikuwa na wimbi kubwa la ujenzi wa nyumba za kuishi na mahoteli, kutokana na kuwa serikali ndio mmiliki wa ardhi kwa kiasi kikubwa ilishindwa kukidhi maombi mengi ya viwanja. Hili likawa ni tatizo kubwa na tena kubwa sana. Hadi mwaka huo tayali mji wa zanzibar ulikuwa unafuata mapendekezo ya mastertplan ya wachina ya mwaka 1982 iliyotiliwa nguvu na sheria ya upimaji miji na ardhi ya mwaka 1985.
Master plan hiyo iliongeza ukubwa wa mji wa zanzibar na ilikuwa imeshatenga maeneo ambayo serikali ilitakiwa kuyaendeleza aidha kwa kujenga nyumba au kugawa ardhi hiyo kwa wananchi wanaotaka kujenga nyumba. Hilo halikufanyika na kama lilifanyika basi ni kwa kiwango kidogo sana. Maeneo hayo yaliyopimwa na kuonyeshwa kwenye master plan ni pamoja na eka tatu ambazo zilitolewa na serikali ya awamu ya kwanza na ya pili kwa lengo la kuwapatia wananchi wa visiwa hivyo sehemu za kulima. Katika awamu hizo wananchi wengi walikuwa wanaishi katika maeno ya umbali wa maili tano kuzunguka mji.
Eka tatu karibu zote zilikuwa nje ya mji na ziliguswa na master plan. Kutokana na mabadiliko ya kiuchumi na mahitaji makubwa ya ardhi kwa ajili ya ujenzi, eka tatu taratibu zilianza kujengwa. Ilikuwa ni kazi ya ziada kujenga katika eka hizo ukizingatia kuwa ardhi ni mali ya serikali. Hata kupitia Mambo msige ambao wao pia wanatoa hati ya kumiliki mali, wananchi waliona huko ndiko kwepesi kwa kupata hati ya kumiliki ardhi.Hivyo wananchi walianza kujenga misingi ya nyumba katika heka hizo na baadae kuziuza na serikali kupitia idara yake ya mambo msige kuidhinisha na kuthibitisha uuzaji na uendelezaji wa ardhi hiyo ambayo awali ilikusudiwa kuwa ni ya kilimo.
Vita kati ya idara za serikali ukaanza taratibu kati ya idara ya Ardhi na Idara ya Mambo msige, huku serikali kuu ikikaa kimya. Leo katika kusoma gazeti nimekutana na kauli ya Waziri wa Waziri wa Maji, Ujenzi na Ardhi Bw. Mansour Yussuf Himid akisema kuwa smz itabomoa nyumba zote zilizojengwa kwenye eka tatu. Kauli hii kwa kweli imenitisha mno. Na ni kauli nzito sana kwa waelfu ya wakaazi wa Visiwa hivyo. Kwani kwa namna moja ama nyingine watakaoadhirika na bomoabomoa hiyo ni wengi, na ni kuanzia kwenye mahoteli yote ya kitalii yaliyojengwa baada ya mwaka 1985, viwanda na maelfu ya nyumba za kuishi.
Tutabomoa nyumba zilizojengwa kwenye ardhi za ekari tatu
zilizotolewa kwa
wananchi baada ya Mapinduzi,’’ alisisitiza Waziri
.

http://www.ippmedia.com/ipp/nipashe/2006/03/16/62186.html

Mapema mwezi wa nne 2006

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeagiza nyumba zote zilizojengwa katika vyanzo vya maji zibomolewe na watendaji wa serikali waliotoa vibali vya ujenzi walipe fidia hizo. Zaidi hapa..http://www.ippmedia.com/ipp/radio1/2006/04/14/64264.html

Mwezi wa nne 2006

Hatimae Waziri Kiongozi wa SMZ amebadili kauli yake juu ya ulipwaji wa fidia kwa nyumba zitakazobomolewa kwenye vyanzo vya maji.Sasa wale waliojenga nyumba hizo hawatalipwa fidia tena.... Zaidi ametupa lawama kwa watendaji wa SMZ kwa kuwa wavivu na mwenye upungufu mkubwa wa kiuwezo katika utendaji wa kazi zao...

Chanzo:http://www.ippmedia.com/ipp/nipashe/2006/04/17/64424.html

2 comments:

KITURURU said...

Hii kasheshe!

ndesanjo said...

Matatizo ya viwanja bado hatujayaona, sio visiwani tu bali hata bara. Vibali vinatolewa bila kufuatilia taratibu za mipango miji na vijiji. Kauli za wanasiasa nazo zinatolewa kihisiahisia. Kila kitu ni sukuma twende, tutajua huko mbele.