Tuesday 9 January 2007

Alijenga Baba na kamalizia Mtoto

Leo Wazenj na Watz wanasherekea siku ya Mapinduzi ya Zanzibar ukiwa ni mwaka wa 43. Mapinduzi hayo ambayo lengo lake kubwa ilikuwa kuwapa weusi wengi madaraka ya kujitalawa.

Tokea Mapinduzi kumeshapita awamu zaidi ya sita za uongozi wa ngazi ya juu kabisa visiwani humo, nikiwa na maana marais wa serikali ya mapinduzi, maarufu kama SMZ. Kila awamu iliingia na mambo yake waliyoona ni muhimu kwa wakati wao, zaidi kila awamu inakumbukwa kwa mazuri na mabaya waliyofanya.

Awamu ya kwanza ilikuwa na lengo la kuwawezesha wananchi walio wengi kuwa na maisha bora. Na hii ilithibitishwa na ujenzi wa nyumba bora katika kila pande ya kisiwa hicho. Juhudi za ujenzi huo zilifanyika kwa pamoja kati ya serikali na wananchi. Yaani wote walishiriki kikamilifu katika ujenzi wa nyumba tena wakitumia kila kitu katika kufanikisha azma ya serikali kuwapatia maakazi bora. Utaratibu uliotumika ni kuvunja nyumba ndogo ndogo zilizojengwa kiholela na kujenga nyumba kubwa za ghorofa. Mfano ni majengo ya Forodhani. Kwa upande mwingine nchi za ulaya nazo hazikuwa nyuma kuona wakaazi wa kisiwa hicho wananufaika, Ujerumani nao wakajenga nyumba za maendeleo katika mtaa wa Kikwajuni ambazo zilikuwa na kila kitu ambacho kinahitajika kwa maisha bora.

Awamu iliyofuata ikaona ni vema kuwa na nyumba nzuri vijijini vilevile, hivyo nayo ikajikita katika kujenga nyumba za vijiji huku wao wakitoa mafundi na vifaa vya ujenzi na wananchi wakifyatua matofali. Vijiji vikajengwa na wananchi wakahamia.

Awamu mbili zikapita pasipo kujishughulisha kabisa na masuala ya ujenzi wa nyumba, licha ya kuwepo na matatizo na kasoro nyingi katika ujenzi wa nyumba katika awamu zilizopita. Mojawapo ya matatizo ni kutomalizika kwa ujenzi wa Nyumba za Michenzani na baadhi ya nyumba za vijiji kukosa wakaazi. Aidha matatizo mabaya ya matumizi ya nyumba hizo na uchakavu wa nyumba. Mbaya zaidi ni kwa wale ambao walivunjiwa vibanda vyao kupisha majengo hayo waliendelea kusota pasipo kujua ni lini watanufaika na nyumba bora.

Awamu ya tano iliingia na aina mpya ya ujenzi wa nyumba, ambao uliitwa nyumba za mkopo nafuu, lengo likiwa ni ujenzi wa nyumba za kisasa kwa kuwauzia wananchi hasa wafanyakazi wa SMZ ambao wengi wao walikuwa hawana nyumba. Serikali ya Uchina ikajitutumua na kujenga nyumba za mkopo nafuu. Kasheshe ikaanza wakati wa ugawaji wa nyumba hizo, malengo yakapindishwa na waliopata wakapata na waliokosa wakakosa, malalamiko yakazidi na serikali kama kawaida yake ikaendelea kutoa ahadi kuwa zitajengwa zingine. Zaidi awamu hii ikachungulia na kule kwenye mabaki ya ujenzi wa nyumba za Michenzani. Wakajipanga na kumalizia block moja, wanainchi wakapata nyumba, kama vile haitoshi kukawepo na malalamiko kuwa nyumba nyingi wamepewa watu toka kisiwa cha pili.

Kuingia kwa awamu ya sita kukabadili kidogo sura ya ujenzi wa nyumba, wao wakaona ni bora kumalizia majengo ya Michenzani na kuwapa wale waliovunjiwa nyumba zao karibu miaka therathini na ushee! Wakawata watu hao kuwa wavumilivu kwani serikali haina fedha za kutosha ila nyumba zitamaliziwa.
Hapa sio kama zamani ambapo wananchi walishiriki ujenzi wa nyumba hizo. Sasa ikawa ni kazi ya serikali pekee kumalizia nyumba hizo. Pengine wananchi walishachoka kuisaidia serikali yao. Sijui.

Umaliziaji wa nyumba za Michenzani utakuwa ni furaha ya pekee kwa Rais Aman Abeid Karume. Kwani nyumba hizo zilijengwa na baba yake ambae alikuwa ndio rais wa kwanza wa SMZ. Pengine Karume ameshawishika kumalizia nyumba hizo ili kukamilisha ndoto za baba yake ambae alitaka kuona kuwa wananchi wake wanaishi katika nyumba zilizo bora kabisa. Aidha ni kuondoa kero za wale ambao walivunjiwa nyumba zao kwa mategemo ya kuishi kwenye nyumba bora, na kujikuta wakisubiri kwa zaidi ya miaka arobaini.

Mwisho napenda kuipongeza SMZ kwa kufikisha miaka 43.

No comments: