Sunday 21 January 2007

Mstakabala wa Soko la Usiku....

Wengine wamediriki kusema ni mojawapo wa kivutio cha watalii wawepo Zanzibar, huku wengine wakisema ni sehemu nzuri ya kwenda jioni iwapo huitaji kupika, na vijana wakipasha kuwa ni sehemu nzuri ya kukutana na marafiki wapya! Hiyo sio sehemu nyingine yoyote bali ni bustani ya Forodhani. Soko la chakula na vinywaji baridi wakati wa usiku.
Kwa miaka mingi eneo la bustani ya Forodhani limekuwa likitumika kwa shughuli mbalimbali, ikiwemo ya soko la lachakula kuanzia jioni hadi usiku. Jioni eneo hilo hilo hutumika kwa ajili ya michezo hasa mpira wa miguu na kuogelea. Muda wa maghahalibi ukifika eneo hilo hugeuka na kuwa soko. Miaka ya karibuni matumizi katika eneo hilo yamezidi kuongezeka, siku hizi asubuhi hadi usiku eneo hilo hutumika na wauza vinyago na batiki. sehemu nyingine hutumika kwa madereva kupumzika wakati wakisubiri wateja wao... hasa watalii.
Upanukaji wa matumizi ya eneo hilo kumeleta uharibifu mkubwa wa mazingira ya bustani hiyo. Aidha wingi wa watu watumiao bustani hiyo umezidi sana kiasi cha bustani hiyo ya Forodhani kuchakaa kwa kasi kubwa. Pamoja na kuzidiwa huko na wingi wa watumiaji bustani hiyo imeendelea kutumika kwa shughuli kupishana kutokana na muda wa siku, yaani asubuhi eneo linatumika hivi, mchana vile na usiku namna hii. Na inapotekea shughuli maalumu basi hutavutiwa muda muufaka ili isije kera shughuli zingine, na hasa soko la chakula....!
Uharibifu wa kwanza kuonekana katika bustani hiyo, ulitokana na wauzaji wa vyakula katika eneo hilo kuanza kupika ndani ya bustani. Hali ya bustani ikawa ni mbaya sana, hadi kufikia kufungwa. Baada ya kuafikiana na Manispaa ya Zanzibar, wafanyabiashara wa usiku walikubali kurejea mtindo wao wa awali wa kutopika katika bustani. Zaidi ni kuja na vyakula ambavyo vimekwisha pikwa tokea majumbani mwao. Tatizo lao likawa limepatiwa dawa.
Kwenye mikusanyiko ya watu hapakosi kadhia zake, wenye vipando hasa pikipiki, vespa na magari madogo, wakaona ni vema kuingia na vyombo vyao ndani ya bustani hiyo. Sijui ni nini hasa kilichopelekea watu hao kufanya hivyo. Vijia ndani ya bustani ambavyo vilikuwa ni maalumu kwa watembeao kwa miguu vikavamiwa na vyombo, haikuchukua muda navyo vikachoka. Mamlaka kama kawaida ikachukua hatua. Mara hii ikawa ni kuvipiga marufuku vyombo vyote ndani ya bustani.
Uchovu wa bustani hiyo sasa ukawa upo wazi kwa kila mtu kuuona, pasipo kujali kama ni mtaalamu au la.. Wanjanja vilevile wakaona hilo huku wakijua mapungufu ya mamlaka husika katika kutengeneza bustani hiyo. Wajanja hao wakatoa masharti yao ili kuweza kurejesha madhali nzuri ya bustani hiyo, ambayo sasa ilikuwa ni mojawapo ya vivutio vya utalii katika kisiwa cha Zanzibar. Sharti lao kubwa walitaka wapewe eneo la kufanyia biashara ndani ya bustani hiyo, aina ya biashara yao ni mgahawa. Bila ajizi Mamlaka husika wakatoa nafasi, Mgahawa ukajengwa na bustani ikafanyiwa matengenezo kidogo sana. Mgahawa ukashamiri na bustani ikaendelea kuharibika.
Bustani hiyo ina bahati ya kusimamiwa na zaidi ya Idara tatu kubwa za serikali, Kuna Manispaa ya Zanzibar, ipo Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe na Idara ya Mipango Miji. Mamlaka hizi zote zimekuwa zikishindana katika kusimamia bustani hiyo, na hasa linapokuja suala la uendelezaji wa bustani hiyo. Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Miji Mkongwe, chini ya sheria ya mwaka 1994, imekuwa ikidai ndie muhusika mkuu, huku Manispaa chini ya sheria ya mwaka 1995 nayo ikidai inapaswa kusimamia eneo hilo. Idara ya Mipango miji ikiendelea kutumia sheria yake ya mwaka 1985, imekuwa ikitaka kuhusishwa kwa kila kitu ndani ya bustani hiyo.
Idara hizo kila mmoja kwa wakati wake ilijaribu kupanga ni kwa namna gani eneo hilo litaweza kurudishwa katika hali yake hasa kimazingira. Manispaa kupitia Mpango wa Mji Endelevu waliona ni vema kufanyia matengenezo bustani hiyo. Lengo kubwa la Mji endelevu ni kuwashirika wadau wote wa bustani hiyo katika matengenezo ya bustani. Hii ni kwa sababu waliamini kwa kuwashirikisha wadau patakuwepo na uendelevu wa bustani. Mamlaka ya hifadhi na uendelezaji wao walikubaliana na Agha Khan kuifanyia matengenezo bustani hiyo na zaidi kuipanua. Wakati taasisi hizi mbili zikijadili nani afanye matengenezo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ikaibuka na ufadhili toka kwa asasi ya Mke wa Rais wa Zanzibar(Karume) kuwa wapo tayali kuanza kuifanyia matengenezo bustani hiyo, chini ya maelekezo ya Manispaa.
Mamlaka ya hifadhi na uendelezaji mji mkongwe, wakaona iwapo watabariki matengenezo hayo watakuwa wanakwenda kinyume na Agha Khan, ambao wanampango wa muda mrefu wa kutengeneza bustani hiyo na kisha kuigawa upya. Hivyo wakashindwa kutoa idhini ya matengenezo. Manispaa ambao hukusanya mapato katika eneo hilo, wakaanza kufanya matengenezo kwa kasi ya konokono kupitia mfuko wa Mji endelevu, huku wakisikilizia ni nani ambae atapewa baraka zote kati ya Agha khan na asasi ya mke wa rais.
Hayo yakiendelea kwa upande wangu napenda kuwashauri kuwa uwamuzi wowote ambao utatolewa basi uwashirikishe moja kwa moja wadau wa eneo hilo. Matengenezo hayo yawe ni kwa faida ya wadau wa eneo, ambao wapo hapo kila siku. Na iwapo watashirikishwa katika matengenezo na kuhakikishiwa kuendelea kufanya biashara katika bustani hiyo, watakuwa na uchungu iwapo wataona bustani hiyo itaharibika, kwani kwa kushiriki kwao katika matengenezo ni njia mojawapo ya kuwafanya waithamini eneo hilo na kulienzi.

No comments: