Thursday 18 January 2007

SMZ yafanya kweli

Kwa muda mrefu mifuko ya plastic nyepesi imekuwa ikitumika kwa wingi katika visiwa vya Zanzibar, kuja kwa mifuko hiyo kulitokana na kisiwa hicho kuwa kivutio cha pekee cha biashara katika afrika ya mashariki katika ile miaka ya tisini mwanzoni... Matumizi ya mifuko hiyo ilikuwa ni kwa bidhaa mbalimbali, aidha mteja hakupaswa kulipia chochote kwa ajili ya bidhaa yake kutiwa ndani ya mifuko hiyo.
Umaarufu wa mifuko hiyo ikashika kasi kiasi kwamba ikiwa sio lazima tena kwenda sokoni au dukani ukiwa na kikapu au mkoba. Umaarufu huo ukaongezeka hadi kufikia kwenye vyakula, sasa ikawa ukienda kununua mbatata za urojo huna haja ya kwenda na chombo chako kwani mifuko ya plastiki ipo. Ukishindwa kumaliza biriani yako hotelini, huna shaka kwani mifuko ya plastiki ipo, iwapo chakula kwenye sherehe au shughuli za misiba kikabaki na ukataka kwenda nacho nyumbani, mifuko ya plastiki ilikuwa ni karibu kuliko chombo chochote kile.
Wenye kuishi kwenye nyumba za ghorofa nao wakaja na udhuru wao, kuwa maji ni ya shida na kamwe hajafiki kwenye ghorofa zao! hivyo kuwafanya wapate shida kubwa linapokuja suala la kujisaidia iwe haja kubwa au ndogo. Njia mbadala ya karibu ikawa ni kutumia mifuko hiyo ya plastiki kukamilisha haja zao, na baade kuitupa chini.
Watumiao vyombo vya moto nao hawakuwa nyuma katika kutumia mifuko hiyo. Chombo kiliendeshwa hadi kwisha mafuta, baada ya hapo mtu hukimbilia kituo cha kuuzia mafuta na mfuko wake wa plastiki. Baada ya kuuziwa mafuta ya kuyatia chomboni mfuko hulembewa mbali pasipo kujali lolote.
Miaka ikaenda na ustawi wa mifuko ya plastiki ukashamiri, sasa ikawa kila baada ya hatua mbili utembeapo kwa miguu unakanyaga mifuko iliotupwa ya plastiki. Bustani, baraza na viunga vyote vikajaa uchafu wa mifuko ya plastiki. Kelele za mji kuwa mchafu zikapamba moto na Halmashauri ya Mji ikaonekana haifanyi kazi yake ipasavyo.
Serikali ikaliona hilo, semina, kongamano na warsha zikafanyika ili kujua athari za mifuko hiyo, Halmashauri kwa upande wake ikatunga sheria ndogo ya kudhibiti matumizi ya mifuko, ambayo haikuwahi kufanya kazi hata siku moja.
Baada ya miaka kumi na ushee sasa, serikali imeona na kuamua kulivalia njuga tatizo la mifuko ya plastiki nyepesi, na ni baada ya kuja na sheria kali dhidi ya matumizi ya mifuko hiyo. Ikiwa ni pamoja na kutumikia kifungu cha miezi sita jela au faini ya dola za kimarekani 2000.00.
Matumizi ya mifuko hiyo kwa zaidi ya miaka kumi kumesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ya kisiwa hicho pamoja na bahari ya Hindi. Ikumbukwe kuwa Taka maji ambazo huchanganyika na mifuko hiyo humwagwa kwenye bahari pasipo kuwepo na mchujo wowote ule, hivyo kuwepo na uharibifu wa maisha katika bahari.
Wafanyabiashara kwa upande mmoja wamekuwa mstari wa mbele kupinga kupigwa marufuku kwa utumiaji wa mifuko mepesi ya plastiki kwa kigezo cha serikali kupoteza mapato ilhali mazingira yakitetekemea. Uwamuzi wa serikali ni wa kuungwa mkono kwa dhati kuanzia kwa wananchi hadi kwa wafanyabiashara, kwani unalengo muhimu wa kuhifadhi na kutunza mazingira ya kisiwa chetu!

8 comments:

Simon Kitururu said...

Matumizi ya mifuko kwa watu wamagorofani halafu wanayatupa chini nilikuwa sijawahi kusikia.Duh !Hiyo kali!Lakini tutunze mazingira yetu!

Simon Kitururu said...

Nilikuwa na maanisha yale matumizi ya mifuko kama choo

Egidio Ndabagoye said...

Kweli mifuko ya plastiki imekuwa kero sana hata pale Dar.Mimi nafikiri badala ya kukusanya vyuma chavu(vilivyo na mabomu) ni bora pia na hii mifuko inakusanywa na kuifanyia Recycle.

Mtumizi ya mifuko kwa watu wa magorofani wakati wa shida ya maji haiko Zenj tu ipo sehemu nyingi Dar ndio usiseme! Kipindi cha shida ya maji ukipita katika magorofa ya wahindi kula Kariakoo unakuta mifuko kibao chini thubutu kuikanyaga.

Kaziyabure said...

Ni hatua nzuri sana kwa SMZ ila kinachonishangaza mimi kwa nini fine zinafanya kwa USD. Hii ni kuonyesha bado tunatawaliwa kifikra.

Egidio Ndabagoye said...

He! George umenena labda Kibunango anajua atuambie.

Kibunango said...

Well, Lengo la kwanza la sheria hii ni kuwabana wafanyabiashara, ambao ndio wanahusika katika kuingiza mifuko hiyo. Faini imewekwa katika US dollar ili kuwezesha kufanya kazi kwa wafanyabiasha wa ndani na nje ya nchi. Aidha imekuwa ni kawadia kwa US dollar kutumika katika shighuli zote za kibiashara...

Natumai Baada ya kudhibiti uingizwaji wa mifuko, Us dollar haitotuimka tena...

Anonymous said...

Chege,
sisi wa bara tunaaiita "Rambo". Mifuko inachafua sana mazingira, labda na Bara watafuata mfano wa Zenji na kuzipiga marufuku rambo, hasa hizo za wa magorofani za kugeuza rambo kuwa choo! Noma!
PS: where is Fano?

Kibunango said...

G Mwasokwa:
Mambo na habari za siku nyingi? Kuhusu Fanon ameshatangulia kunako haki, baada ya kupata ajali ya Vespa Mwishoni mwa mwaka 2003.