Wednesday 11 April 2007

Tindikali kwa wauza kilaji Zanzibar

Sijui kisiwa kitaendelea vipi katika sekta ya Utalii kama wauzaji vinywaji vikali wataendelea kuteswa namna hii haya mambo yakuchanganya maswala ya kidini na uchumi hayana maendeleo yoyote Somalia mfano.




Wakala mwingine wa pombe amwagiwa tindikali

2007-04-10 10:28:44
Na Mwinyi Sadallah,Zanzibar

Wakala mwingine wa kusambaza pombe Zanzibar, Bw. Chadalal Javed, amemwagiwa tindikali usoni, muda mfupi baada ya kufungua duka lake lililoko mtaa wa Empire mjini hapa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mjini Magharibi Bw. Bakar Khatib Shaaban alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Tukio hilo lilitokea jana saa 3:00 asubuhi.

Alisema kwamba mfanyabishara huyo mwenye asili ya Asia, alivamiwa na mtu asiyejulikana, muda mfupi baada ya kufungua duka lake.

``Ghafla mfanyabiashara huyo alimwagiwa kemikali na kumjeruhi sehemu za usoni na tayari amepelekwa jijini Dar es Salaam kwa matibabu zaidi,`` alisema Kamanda Bakari.

Alisema kuwa wakati tukio likitokea, mfanyabiashara huyo alikuwa dukani na mkwewe wakijiandaa kutoa huduma kwa wateja wao.

Alisema hata hivyo, polisi hawakufanikiwa kuchukua sampuli za kemikali iliyotumika, kwa vile baada ya tukio kutokea, wahusika waliharibu mabaki ya kemikali hiyo.

Kamanda Bakari alisema kwamba iwapo wangefanikiwa kupata mabaki ya kemikali hiyo, wangeweza kupeleka kwa Mkemia Mkuu kujua aina ya kemikali iliyotumika.

``Hatufahamu, aina ya kemikali iliyotumika,lakini tunaendelea na uchunguzi kwa kuwa mtu aliyefanya uhalifu huo alifanikiwa kukimbia baada ya tukio,`` alisema Kamanda Bakari.

Mfanyabiashara huyo anamiliki duka la Scorch Store, ambalo linatumika kusambaza pombe Zanzibar katika mahoteli ya kitali, baa na watumiaji wa rejareja Zanzibar.

Kamanda Khatib alisema hilo ni tukio la pili kutokea kwa wamiliki wa maduka ya pombe. Alisema mwezi uliopita mfanyabiashara mwenye asili ya Kiasia, Bw. Kirikti Mandala, alimwagiwa tindikali akiwa dukani kwake eneo la Michenzani.

Alisema kwamba katika tukio hilo watu wawili walihojiwa na polisi, lakini hadi sasa hakuna mtu aliyefikishwa Mahakamani kuhusiana na tukio hilo.

Hivi karibuni baadhi ya wanaharakati wa dini, wamekuwa wakilalamika kuongezeka kwa idadi ya baa katika manispaa ya Zanzibar, kitendo ambacho wanasema ni kinyume na mila na utamaduni wa Mzanzibari.

Mwezi uliopita wanaharakati hao, waliandamana kupinga ongezeko hilo la idadi ya baa katika mji wa Zanzibar, lakini hawakutoa takwimu za ongezeko hilo.

* SOURCE: Nipashe

2 comments:

Simon Kitururu said...

Hi sio safi kabisaa!Nashindwa kuelewa watu watumiao dini kama kisingizio cha kufanya uhalifu wa kuumiza wenzao.Hivi mtu ukienda kinyume cha dini si utapata kwenda jehanamu?Sasa jamaa kwanini wasihubiri hivyo na kuachia watu wachague wenyewe kwenda Jehanamu au Peponi?

MTANZANIA. said...

Ninachokiona mm huenda ikawa ni ileile tofauti ya kiitikadi ndiyo inapelekea haya yote. Inahitajika elimu ya kutosha kwa hawa wenzetu.