Thursday 19 April 2007

Uchafuzi wa Mandhari ya Bwawani Hotel

Bwawani Hotel ndio hotel pekee ambayo SMZ inaweza kujisifia kwa namna ilivyojengwa na huduma ambazo zinatolewa na hoteli hiyo. Hotel hii ilijengwa katika miaka ya 70, ikiwa na vyumba 118 kwenye jengo la ghorofa nne. Ipo umbali wa kilometa nane toka uwanja wa ndege na ni mwendo wa dakika tano toka bandarini.

Pamoja na vitu vingine vinavyopatikana katika hotel kubwa, hotel hii ina viwanja wa Tennis ndani na nje, swimming pool ya ndani, ukumbi wa michezo( game room) na bwawa zuri upande wa mbele ya hotel hiyo.

Leo ningependa kuzungumzia juu ya bwawa la hoteli hiyo, ambapo pengine ndio lililo zaa jina la Hotel Bwawani. Bwawa ambalo hadi hoteli inakamilika katika miaka ya sabini, ujenzi wake ulikuwa bado kukamilika, hivyo kuto toa madhari halisi ya hoteli hiyo.

Katika miaka ya themanini, wakati SMZ ikiwa inajichanganya kuamua kufuata mfumo gani wa serikali za mitaa, toka serikali za majimbo, kulijitokeza wawekezaji ambao waliona kuwa upo umuhimu wa kuendeleza bwawa hilo. Katika kipindi hicho tayali madhari ya bwawa hilo ilikuwa ni ya kuchukiza zaidi kuliko kuvutia. Majani maji yalikuwa yakiongezeka kwa kasi kubwa.

Mapendekezo yaliyotolewa na wawekezaji wa miaka hiyo ya themanini ni kuhamisha bandari ya yatch iliyopo kwenye bandari ya Malindi hadi kwenye bwawa hilo, kujenga ofisi ya Meja wa Halmashauri ya Mji wa Zanzibar(Town Hall) katika kingo za bwawa hilo, toka katika Ofisi ya Halmashauri ya Mji katika barabara ya Benjamin Mkapa. Ofisi hiyo ya Meya licha ya kuwa na ukumbi wa mikutano ya Madiwani, pia ungekuwa na club ya yatch zinazotia nanga Kisiwani hapo toka sehemu mbalimbali hapa duniani.

Wazo hili lilipo pelekwa kwenye vyombo vya SMZ lilitupwa kando, licha la kuwa wazo bora kabisa katika kipindi hicho hadi leo na mpaka kesho. Kwani kinachoendelea katika bwawa hilo hivi sasa ni uchafu mtupu. Kwa upande mwingine iwapo wazo hili lingefanyika katika siku zile, matatizo ya kisaikolojia yanayowakuta Madiwani na Meya wao sasa yasingekuwepo. Kuwachanganya Meya na Madiwani wake katika jengo moja na Watendaji wa Manispaa ya Zanzibar kumesababisha kuwepo na miingiliano ya kiutendaji kila siku katika Manispaa hiyo.

Ukiachana na adha za madiwani hao, bwawa hilo ni makaazi ya ndege watokao kaskazini ya dunia wakati wa msimu wa baridi huko kaskazini, hivyo iwapo bwawa hilo lingeendelezwa na kutuzwa vema tungeweza kujifunza mengi kuhusu ndege hao na zaidi kingekuwa ni mojawapo wa kivutio cha utalii. Lakini hili nalo halipo ndani ya mawazo ya watendaji wa SMZ!

Kumekuwepo na mawazo mengi toka serikalini na katika Halmashauri ya Mji juu ya kuendeleza bwawa hilo. Lakini yote kwa upande mmoja ni kuchakaza tu bwala hilo au kuliondoa kabisa.

Katika miaka ya tisini msikiti(Msikiti Mabluu) ambao uliondolewa ili kupisha ujenzi wa bwawa hilo, ulijengwa upya. Ujenzi wa msikiti huo ulikuwa ni kutoa mfano wa mradi mpya wa ujenzi wa nyumba katika muda mfupi. Ujenzi wa msikiti ulikamilika ndani ya siku saba na siku ya nane ukatumika. Mawazo ya ajabu ajabu yakazidi kumiminika, moja wa Mameja alipendekeza kuwa sehemu yenye magugu maji ijazwe kifusi ili kupatikane nafasi ya kuweka makontena ya biashara! Meya mwengine alikuja na wazo kuwa bwawa hilo litumike kuwa jaa kuu la taka.
Pengine waliokuwa wanajitahidi kuliweka bwawa hilo katika hali ya usafi ni wafungwa, ambao kila mwaka kwa mamia hupita hapo kukata magugu maji.

Miaka ya elfu mbili Waziri kiongozi alitoa amri ya wafanyabiashara wa vinyago na batiki wapewe eneo hilo kwa biashara zao, agizo likatekelezwa na madhari ikazidi kuwa mbaya. Hata hivyo kutokana na kuwepo kwa msikiti wauza vinyago walijikuta wakiondolewa hapo.

Ukarabati wa kusuasua wa Bandari ya Malindi umeligeuza tena bwawa hilo kuwa sehemu ya kuhifadhia makontena ya bandarini, hiyo kuendelea kuchafua bwawa na zaidi hata kuziba madhari nzuri ya mbele ya hoteli hiyo. SMZ inadai kuwa uwekaji wa makontena katika eneo hilo ni wa muda tu, na hata bandari itakapokamilika makontena hayo yataondolewa. Cha kujiuliza hapo jee vifusi na michanga iliyojazwa katika bwawa ili kutoa ya uwekaji wa makontena yataondolewa au utakuwa ni mwanzo wa kuzaliwa wazo jingine la kutokomeza bwawa hilo?

Kwa maoni yangu wazo lilitolewa katika miaka ya themanini ya kukamilisha ujenzi wa bwawa na ujenzi wa ofisi ya Meya pembeni ya bwawa hilo, lilikuwa ni wazo pekee ambalo lingeweza kulinusuru bwawa hilo kuwa kichaka cha mawazo duni ya viongozi wa SMZ. Aidha kungesaidia kuendeleza bwawa hilo na kuwa sehemu ya kuvutia kabisa katika eneo la Mji Mkongwe zaidi ya Forodhani.

5 comments:

Aliko said...

mismanagement...

Egidio Ndabagoye said...

Dah kazi ipo.Mambo yanafanyika "kienyejienyeji" naona.Hakuna mipango endelevu kila kiongozi akiaj anakuja na mipango yake.

Hivi hii Hotel ya Bwawani nani ni mmiliki wake sas hivi?

Simon Kitururu said...

Inaonyesha kuwa mipango yakudumu haipo.Kila kiongozi ajaye anakuja na mpango mpya.Hili tatizo linzzingua sehemu nyingi za utendaji kazi bongo

Anonymous said...

Kamanda! tunakumissi hapa Suomi, vipi kiwanja cha huko? utengano wa kati ya wabara na wazenji hautaishi, labda wajukuu zetu ndio wataweza kutafuta muafaka wa swala hili...
Rupia

Kibunango said...

Huku salama, ila mambo sio ka tunavyosikia.. kipindo ni cha nguvu... Aidha kuhusu Wazenj na Wabara ni vema kukubali tofauti zetu...