Tuesday 21 August 2007

Umbeya Wenye Manufaa...

Hatua ya mradi wa Usimamizi wa Uhifadhi na Mazingira ya Ukanda wa Pwani "MACEMP" kanda ya Zenj kuanzisha mpango wa kuwafanya wavuvi kuwaripoti kwa siri wavuvi haramu ni mzuri kwa lengo la kuwajua wavuvi haramu. Hatua hii imechukuliwa ili kudhibiti uvuvi haramu ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakiharibu mazingira ya baharini, pamoja na kuhatarisha maisha ya viumbe wa baharani.

Lengo kubwa la mradi huo ni kuhifadhi na kutunza mazingira ya pwani kwa kuondoa umaskini wa wavuvi. Malengo yao kwa kiasi fulani yamefanikiwa kupitia kwa kamati mbalimbali za wavuvi katika kisiwa hicho. Mradi huo umeshatoa boti,ndege,mikopo na nyavu kwa kamati mbalimbali ili kuondoa tatizo la uvuvi haramu huku ikikuza kipato cha wavuvi hao.

Hata hivyo pamoja na utoaji wa vifaa hivyo, tatizo la uvuvi haramu limekuwa likiendelea. Kuendelea kwa tatizo hilo kwa upande mwingine ni kuonyesha kuwa mradi huo bado kuwafikia wadau wote katika sekta ya uvuvi. Zaidi kuna tatizo ndani ya kamati za uvuvi ambao wamelalamikiwa na mradi kwa kuvujisha siri za mikakati ya kudhibiti uvuvi haramu.

Mradi huu ili kuwa endelevu unapaswa kuangalia tena malengo yake, na njia ambazo wanatumia kuwafikia wadau wake. ushirikishwaji wa kamati hizo za uvuvi na wavuvi wenyewe. Iwapo mojawapo wa malengo ni kuondoa umaskini wa wavuvi, hapana shaka basi wawatafutie au kuwaelekeza jinsi ya kupata soko la uvuvi wao(soko la ndani na nje), uhifadhi endelevu wa maeneo yanayotumika kwa uvuvi, maana na athari za uvuvi haramu.
Kutoa vifaa pekee sio njia ya kuweza kufanikisha kuondoa uvuvi haramu na hata umaskini wa wavuvi hao.

Ipo mifano mingi ya miradi ambayo ilipewa vifaa vingi kwa miradi hiyo lakini ikashindwa kuendelea na kuishia kufa baada ya muda mfupi. Hii ilitokana na wadau kutojiona kuwa wapo ndani ya miradi hiyo, na kujenga tabia kuwa maendeleo ya miradi hiyo sio yao bali ni ya serikali au watoa miradi hiyo.

Iwapo mradi wa MACEMP watataka mradi huu uwe endelevu, inawabidi kuangalia ni njia gani ambayo wataweza kuitumia kuhakikisha kuwa wadau wao wanajua umuhimu wa mazingira ya bahari ambalo ndio shamba lao la kuwaingizia kipato. Inawabidi wawafikie hadi wale wavuvi wa chini kabisa,zaidi ya kuishia kwenye kamati na wale wavuvi wanaojulikana huko vijijini. Zaidi ya kuwafikia itawabidi kuwapa elimu tosha ambayo itawafanya wathamini na kutambua umuhimu wa mradi huo kuwa upo kwa ajili ya kuwaondolea umaskini huku mazingira ya bahari na viumbe vyake yakiwa salama.

No comments: