Sunday, 20 January 2008

Kuta za Mji Mkongwe na Watalii....


Friday, 18 January 2008

Mambo ya Mapinduzi....


Tukiwa bado tunasheherekea Mapinduzi ya Zenj, nimeona bora leo tujikumbushe baadhi ya misukosuko ya wakati ule wa mapinduzi........

Monday, 14 January 2008

Wazenj na Mechi za Bure...

Tangu kuchukua nafasi ya Ukurugenzi wa wa timu ya Miembeni, Amani Makungu amekuwa akitoa ofa kadhaa kwa washabiki ya soka visiwani humo kwenda kuona mechi bure. Miembeni ni mojawapo ya timu kongwe visiwani, ambayo imewahi kuwa na mafanikio makubwa kisoka miaka ya nyuma, kabla ya kudorora na kupotea katika ramani ya soka hasa kipindi cha ufadhili cha miaka ya tisini.

Timu hiyo ambayo ipo kwenye kitongoji cha Miembeni ambacho kinajulikana sana visiwani humo kwa makasheshe, ilitwaa ubingwa wa visiwa hivyo mara ya mwisho yapata miaka ishirini(1987). Mwaka jana imefanikiwa tena kuchukua ubingwa wa ligi visiwani humo chini ya ukurugenzi wa A. Makungu na kocha Suleiman Mahmoud Jabri.

Ufadhili wa Mkurugenzi huyu umewawezesha wapenda soka na washabiki wengi wa timu hiyo kuweza kuona mechi kubwa ya klabu hiyo bila ya viingilio. Mechi yakaribuni ya bure ni ile ya kombe la mapinduzi ambapo Miembeni iliweza kutwaa kombe hilo baada ya kuifunga timu ya Polisi kwa mabao 2-1. Mechi hiyo ya dezo ilihidhuriwa pia na Mh. Aman Karume Rais Zanzibar.

Wengi wamenufaika na hili, lakini ni vema vilevile kuangalia nini athari zake kwa soka la visiwa hivyo. Baada ya wadhafili wakubwa kujitoa kugharamia timu kubwa huko visiwani, soka la visiwani lilianguka sana, kuanzia katika mechi za ndani hadi za kimataifa. Ukiangalia nyuma kidogo kama miaka kumi iliyopita hasa katika kipindi cha miaka ya 1996-1998, kulikuwa na upinzani mkubwa wa vilabu kutokana na utajili wa wafadhili wao. Timu ambazo zilikuwa zikivuma kipindi hicho ni Mlandege, Malindi na Shangani, ambazo zote zilikuwa chini ya ufadhili wa wafanyabiashara. Timu kama ya Malindi iliweza hata kusajili wachezaji toka Ulaya ya Mashariki na Afrika vilevile. Klabu kama Miembeni, Kikwajuni na Small Simba ambazo hazikuwa na wafadhili ziliporomoka vibaya katika kiwango cha soka visiwani humo.

Lakini nini kilitokea baada ya wafadhili kujitoa kwenye klabu hizo? Ni kufanya vibay kwa timu hizo, kuwepo na migogoro na kadhia zingine. Sasa klabu zinazomilikiwa na asasi za serikali zikanza kuibuka upya. Timu kama KMKM ambayo ilikuwa tishio katika miaka ya 80 ikarudi tena, huku timu ya Polisi ikiibuka na kuchukua ubingwa wa Zenj na kujiwekea historia yake. Mafanikio ya kablu hizi ni kutokana na wachezaji wake kuwa ni waajiliwa wa asasi hizo.

Miembeni inawapasa kutofumba macho katika suala la kuona timu hiyo inabaki kung'ara kama zamani. Ni wajibu wa kila mwanachama, mpenzi na shabiki wa klabu hiyo kukuna kichwa ni kwa namna gani anaweza kuchangia kuona timu hiyo inakuwa na maendeleo endelevu, badala ya kuendelea kumtazama mtu mmoja akifanya kila kitu kwa klabu hiyo kongwe visiwani. Matokea ya ufadhili wa mtu mmoja/mfanyabiashara yapo wazi kwa kablu kadhaa za visiwani humo. Hivyo ni vema kujifunza kutokana na makosa yaliyofanyika katika kablu hizo. Huu usiwe muda wa kuchekelea kuingia uwanjani bure, bali uwe muda wa kuangalia ni kwa vipi timu hiyo itaweza kukaa katika chati ya juu na kufanikiwa kisoka bila ya kutegemea ofa.

Saturday, 12 January 2008

Leo ni Miaka 44 ya Mapinduzi ya Zenj

Kila la heri kwa wanamapinduzi wote wa Visiwa vya Zenj, hali kadhalika kwa wasomaji wote wa blog hii...

Mapinduzi Daima...

Katika moja ya vituko vilivyotokea katika shehere za mwanzo za kusherherekea Mapinduzi ya Zenj ni pale Marehemu A. Karume alipokuwa akitoa hotuba yake ambayo ilikuwa ikielezea mafanikio na faida za Mapinduzi hayo. Kwa sauti yake nzito sawa na kilo kadhaa za Nyati, ambayo kwa upande fulani iliwafanya wasikilizaji wake kuwa na kauoga fulani, alitamba kuwa serikali ya mapinduzi (wakati ule) ina fedha nyingi za kigeni(us dollar)zaidi ya idadi ya waakazi wa visiwa hivyo. Aliendelea kwa kusema kuwa fedha hizo ni nyingi kiasi kwa anaweza kumpatia kila mwananchi dola mia za kimarekani na bado fedha ikabaki.

Kijana mmoja kiasi cha miaka kumi na mbili hivi, alinyosha mkono ili aweze kuuliza swali,Wazee waliokuwa karibu yake walijaribu kumzuia kijana huyo kutonyosha mkono. Purukushani hizo zilivuta idadi kubwa ya watu kutazama upande wao, badala ya kuendelea kusikiliza hotuba. Hali hii ilimfanya Marehemu Karume kumruhusu kijana huyo aulize swali lake. Huku akijiamini sana kijana huyo aliuliza hivi..

"Mhe. mimi naomba kupatiwa dola zangu mia sasa hivi..."

Friday, 11 January 2008

Wazenj na Kuzamia Ulaya

Kwa miaka mingi kumekuwepo na njia mbalimbali zilizotumiwa na vijana kwenda kutafuta kile wanachodai ni maisha bora. Njia ambazo zilipata umaarufu mkubwa ni ile ya kuzamia kwenye meli.Hii ilikuwa ni katika ile miaka ya themanini ambapo soko la ubaharia lilikuwa kubwa kwa vijana wa kiafrika. Vijana wa Zenj nao hawakuwa nyuma katika hili, wengi waliacha shule na kukimbilia kuzamia meli kwa lengo la kufika ulaya.

Mwishoni wa miaka ya themanini na mwanzoni miaka ya tisini, njia ya kwenda ulaya ilibadilika toka kuzamia meli na kupanda pipa (ndege). Hamu ya kwenda ulaya ilizidi kuwa kubwa mno miongoni wa vijana, na wengine walidiriki hata kuteka ndege(ATC)ili tu waweze kufika huko ulaya. Zaidi wengi waliweza kutumia njia nyingi za kulaghai familia zao au kuiba ili tu waweze kufika huko Ulaya.

Miaka ya tisini, wasomi wa kizenj nao wakaingia katika anga ya kuzamia huko Ulaya na Marekani. Ushawishi mkubwa ulitokana na wingi wa vijana kukimbilia ulaya na hasa Uingereza kwa madai ya ukimbizi kutokana na mfumo wa vyama vingi. Wasomi wengi ambao walibahatika kusomeshwa na SMZ asilimia kubwa wameamua kutorudi tena Zenj na sasa wanaendelea na kutafuta maisha yao huko Ulaya na Marekani. Katika kundi hili wapo pia wale walioacha kazi zao muhimu katika SMZ na mashirika ya SMZ.

Katika karne hii mpya imeibuka njia nyingine ya kuzamia huko ulaya, hii ipo katika uwanja wa michezo na utamaduni. Baada ya mwanamasumbi wa Tanzania Bara kuzamia huko Australia katika michuano ya jumuiya ya madola mwaka 2006, wachezaji wawili wa Zenj Heroes nao waliingia mitini, hii ilikuwa ni mwaka 2007. Mwaka huu nao imeripotiwa kuwa wasanii wawili nao wameingia mitini baada ya kumaliza masomo yao huko nchini Norway.

Kwa ufupi hizo ni njia mbalimbali ambazo wazenj wameona ndio nzuri kabisa ili kuweza kufika huko ulaya. Zaidi kumekuwepo na mafanikio katika ngazi ya kifamilia kwa baadhi ya wazenj waliokimbilia huko ulaya. Wengine wamekutana na maadhibu makubwa ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa nchi yao, kiasi kwamba kwa sasa wanaweza kuja nchini mwao kwa kuomba viza. Wapo ambao wametekwa na mambo ya huko ulaya ambayo hayana faida yoyote kwao zaidi ya mashaka makubwa ya afya zao. Hawa ni wale waliojiingiza katika kutumia madawa ya kulevya na ukahaba.Wapo vile vile wauzaji wa madawa ya kulevya ambao wanaendelea kuwaangamiza wenzao watumiayo madawa hayo.