Saturday 30 August 2008

Zenj yakaribia kuanza kusahau Metakelfin, Chloroquine.....

Akiwa katika ziara yake huko USA, Prez wa TZ Jakaya Mrisho Kikwete, akimshukuru Prez G. W Bush, alisema kuwa huko Zenj wapo karibu kabisa kutokomeza ugonjwa wa malaria. Aliendelea kwa kusema pale sipitali ya Mnazi Mmoja kesi za malaria zimepungua kwa kasi toka asilimia 30 hadi asilimia 1.

Mpaka leo hii Malaria ndio ugonjwa unaouwa watu wengi duniani. Kila mwaka zaidi ya watu milioni moja hufariki kutokana na ugonjwa huu. Hivyo juhudi zozote za kuondfoa ugonjwa huu hazipaswi kupitwa bila kuungwa mkono na kama sio kuzipongeza.

Zenj kwa miaka mingi kupitia misaada mbalimbali imekuwa ikijitahidi kuangamiza mazalio ya mbu ambao husababisha malaria. Hali ya hewa ya visiwa hivyo ni nzuri sana kwa mbu wengi kuzaliana na hivyo kusababisha kuwepo kwa malaria. Njia iliyokuwa ikitumika ni kunyunyuzia dawa za kuangamiza mazalio ya mbu katika kila kona ya mji wa zanzibar, toka mji mkongwe hadi ng´ambo, vita hivyo vya kuangamiza mazalio ya mbu ilibaki kidogo kufanikiwa na ilikuwa ni katika ile miaka ya sabini, hadi hivyo haikuweza kufanikiwa. Kurudi kwa mradi huu katika miaka ya hivi karibuni kulitoa tena faraja kwa wengi katika vita hivi.

Malaria na hasa vijidudu visababishao ugomjwa huu hatari kabisa wamekuwa wajanja na kuendelea kubadilika badilika na kushindana na kinda pamoja na dawa za kutibu ugonjwa huu. Kwangu mimi kesi ya kwanza kabisa ya malaria ilinipata kisiwani Zenj karibu miaka ishirini na tano iliyopita. Dozi ya kwanza kupewa ilikuwa ni Chloroquine, haikuweza kupambana na malaria yangu, baada ya wiki mbili bila mafanikio nilipatiwa dozi nyingine ya Quinine ambayo niliitumia kwa kipindi kingine cha wiki mbili na ilifanikiwa kunitibu. Miaka kumi baadae nikapata tena malaria nikiwa huko huko visiwani,dozi ya kwanza kupewa ilikuwa ni Metakelfin, baada ya wiki vidudu vya malaria vilikuwa bado vikitamba, dr. akanipa Phansider nayo ikashindwa kufanya kazi tena baada ya kuirudia katika wiki mbili mfulurizo. Mwishoe nikaambia nijaribu Halfan.. hapo nikapona

Tatizo la malaria katika nchi za Afrika kwa upande mwingine limefungua mlango wa watengenezaji wa madawa yasio pimwa madhara yake kwa binadamu, na kuuuzwa kwetu Afrika... kwa kisingizio kuwa dawa hizo ni za bei nafuu. Kila kukicha kunatangazwa dawa mpya za kutibu malaria na nyingi kati ya hizo huwa zina side effect kubwa mno kwa mtumiaji.

Vyandarua kwa upande mmoja zimesaidia sana katika vita hivi, ingawa sio wananchi wengi wenye uwezo wa kumudu kununua vyandarua, lakini mchango wake ni muhimu sana . Hili la kuangamiza mazalio ya mbu ndio la msingi. Na iwapo takwimu za ugonjwa huu zinaanza kushuka katika zahanati na sipitalini ni dalili nzuri kuwa kuna mafanikio. Cha msingi ni kwa wananchi wote kuunga mkono juhudi hizi ili kutokomeza kabisa ugomjwa huu wa malaria.

Habari ndio hiyo...

Friday 29 August 2008

Mwezi wa gharama wakaribia huko Zenj...

Unapokaribia mwezi mtukufu wa Ramadhani, Jiji la zenj hujaa pilikapilika nyingi mno, ni rahisi sana kutofautisha jinsi watu wanavyoishi kabla ya mwezi huo kwani kila mtu huwa kwenye pilika za hali ya juu, tofauti kabisa na miezi mengine yoyote katika mwaka.

Kijana mmoja aliwahi kunilalamikia kuwa ingependeza kama kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikawa kama fainali za kombe la dunia kutokea mara moja kwa miaka minne tena katika nchi tofauti. Akiwa na maana iwapo itakuwa zamu ya Tanzania kufunga mwaka huu nchi zingine hazitofunga mpaka zamu yao ikifika....! Sikupata picha kamili ingekuaje kwa nchi zaidi ya mia mbili duniani humu.. Mawazo kama haya uzaliwa kichwani mwa mtu kutokana na majukumu mengi katika mwezi huo.

Kabla ya mwezi kufika wengi hupata mialiko ya kuhudhuria shughuli za arusi, hii yote ni katika kujiandaa na mfungo, kwani wengi hupenda kufuturu majumbani mwao, hivyo vijana wengi hupenda kufunga ndoa katika kipindi kama hichi ili mradi tu awe na uhakika wa kupata futari murua akiwa kwake.

Hali halisi ya Zenj na hasa katika kuandaa futari husababisha ugumu mkubwa katika mwezi huu. Bei za bidhaa hupanda maradufu hivyo kuwa usumbufu mkubwa kwa waakazi wengi wa kipato cha kati visiwani hapo. Ikiwa bado siku kadhaa kabla mwezi huo kuanza bei ya nyama kwa kilo sasa ni zaidi ya sh. 5,000 huu ni mzigo mkubwa. Ikumbukwe bidhaa za vyakula kisiwani humo nyingi hutoka Bara na Pemba, hata hivyo uonekana kama havitoshi pamoja na ukubwa wa gharama.

Sina hakika kama kisiwa cha pili bado wataendeleza mgomo wao wa kutopeleka vyakula huko Zenj, baada ya muafaka kurudishwa tena mezani, na sina hakika hali itakuaje baada ya kasheshe za karibu miezi mitatu kuhusu Zenj kama nchi zitaathiri vipi mfungo wa mwaka huu. Kawaida pamoja na rais wa Zenj kutembelea kwenye markiti akiwaomba wauzaji kupunguza bei, bei hubaki palepale. Safari hii rais atavuka hatua ya kwenda markiti, kwani itabidi kuwashawishi waletaji bidhaa kufanya hivyo na kuweka siasa kando katika mwezi huu.

Ikumbukwe kuwa wananchi hao hujiandaa kwa muda wa miezi kumi kuja kufunga kwa mwezi mmoja, kwani bila ya kujiandaa na kujiwekea akiba unaweza kuja kuumbuka katika kutafuta futari hivyo kuufanya mfungo kuwa mgumu zaidi. Zaidi ya wao wenyewe kujiandaa, ndugu wengi waishio nje ya Zenj na hasa nje ya Afrika wamekuwa mstari wa mbele kusaidia kupunguza makali ya mwezi huu, kwa kujaza wazenj wengi katika ofisi za west union. Kwani pamoja na kujiandaa na futari pia ni mwanzo wa maandalizi ya sikukuu ya Idd ambayo usheherekewa kwa muda wa siku nne mfululizo. Sherehe hizo ni kubwa sana hasa kwa watoto ambao uwakera wazazi wao kwa kudai nguo mpya na maridadi, toys na kadhia zingine ziendanazo na sherehe hizo.

Mie binafsi napenda kuwatakia Wafungaji wote Mfungo mwema....