Thursday 6 November 2008

"Migogoro ya Kisiasa katika SMZ"- Hayo ni Mavuno...

Hivi karibuni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Kiongozi, alinukuliwa akisema kuwa migogoro ya kisiasa katika SMZ imekuwa chanzo cha ucheleweshaji wa mipango ya maendeleo ya wananchi wake. Kauli hii sio ngeni miongoni mwa wananchi wa visiwa vya Zenj hali kadhalika kwa maelfu ya watendaji wa vyombo mbalimbali ya SMZ. Migogoro inayozungumziwa na Mhe. huyo ni matokeo ya sera za umimi na uwale zilizozaliwa wakati Visiwa hivyo vilipoanza kuingia katika mfumo wa vyama vingi mapema katika miaka ya tisini.

Siasa katika vyombo vya SMZ ilikuwa ni kwa manufaa ya chama tawala, hii ni kwa watendaji wote kuanzia wa ngazi za chini hadi za juu. Kila mfanyakazi aliaminika kuwa ni mwanachama wa chama tawala na ameajiliwa ili kutekeleza sera za chama. Hii ilikuwa inadhibitisha na ushirika wa asasi za SMZ katika shughuli za kichama ambapo ilifikia hatua za kufunga ofisi kabla ya muda wake ili kutoa nafasi kwa wafanyakazi kushiriki katika mikutano ya hadhara ya chama tawala. Nahisi katika kipindi hicho hadi sasa ni shurti uwe mwanachama wa chama tawala kabla ya makablasha yako ya uombaji kazi kujadiliwa.

Hata hivyo kuingia kwa mfumo wa vyama vingi kulibadilisha mtazamao wa wafanyakazi kuhusu umuhimu wa kuwa katika chama tawala ili kuendelea kuwatumikia wananchi. Mabadiliko haya yaliguza wafanyakazi katika ngazi zote. Wafanyakazi wa ngazi za juu ambao wengi walikuwa katika nyadhifa zingine chamani, huku wakipata misukumo toka chamani, bila kujijua walianza kupandikiza mbegu mbaya mno ndani ya vyombo vya SMZ.

Katika moja ya mikutano ya kampeni ya 1995 Kiongozi wa ngazi ya juu chamani na katika SMZ alitamka maneno ya kejeli mno kwa watendaji wa SMZ ambao wamehusu kisiwa cha pili. Hotuba yake hiyo ilijukuwa imejaa ubaguzi na shutuma nyingi kwa wafanyakazi na wananchi toka katika kisiwa cha pili haikuweza kujenga bali ilikuwa ndio mwanzo wa migogoro katika Idara zote za SMZ, ambapo Mhe. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri kiongozi anazungumzia.

Nakumbuka siku mbili baada ya hotuba ile, mmoja wa mfanyakazi katika idara ya kutoa huduma ambae alikuwa ni rafiki yangu aliniambia kuwa pamoja na kuwa na mapenzi ya muda mrefu na chama tawala lakini maneno yaliyozungumzwa na kiongozi huyo ni matusi makubwa kwao watokao kisiwa cha pili, hivyo anajitoa rasmi katika chama tawala, na yupo tayali kwa lolote ambalo litamtokea kwa hatua hiyo yake.

Mbaya zaidi, baada ya hotuba hiyo wafanyakazi wengi waliohusu kisiwa cha pili ambao walionyesha mapenzi tofauti walijikuta wakipoteza kazi zao, wengine wakinyanyaswa na kutegwa kwa sababu za kisiasa tu na tena kwa sababu ya SMZ kuunganisha siasa na serikali.

Haya aliyozungumza Mhe. Waziri hayana kificho, kwani katika moja ya miafaka ilikubalika kuwarudisha makazi wale wote ambao walifukuzwa kazi kwa tofauti za kisiasa. Ni wajibu wake iwapo anataka kuona migogoro hiyo inakwisha kuchukua hatua za vitendo katika kuona kuwa siasa katika Idara za SMZ zinawekwa kando, ikiwa ni pamoja na kuwarudisha wale wote ambao walitimiliwa kwa ajili ya mitazamo yao ya kisiasa. Kwa upande wa ajila mpya zisiangalie siasa bali uwezo wa mfanyakazi.

Zaidi Mhe anatakiwa kuona kuwa utengano katika idara za SMZ unakwisha ili kuweza kuongeza kasi ya kutoa huduma na kuleta maendeleo kwa wananchi wa visiwa hivyo.