Wednesday, 14 January 2009

Tukiwa bado kwenye wiki ya Sherehe za MapinduziWakati tuneendelea kujadili hotuba ya Mhe Prez wa Zenj wakati wa shehere za miaka 45 ya Mapinduzi na yale yote yaliyojili katika sherehe hizo,ambapo kama kawaida yamezua mazungumzo marefu sana sehemu mbalimbali hapa duniani...

Leo hebu tuangalie jina la mtaa maarufu wa Darajani, Jina hili limetokana na kuwepo na daraja katika eneo hilo. Zaidi daraja hilo lilikuwa limepambwa na taa za umeme na kulifanya kuvutia sana na kupitika hata wakati wa usiku. Kumbukumbu za kuwepo na taa hizo inakwenda nyuma mwanzoni mwa miaka ya 1900.

Hali ya sasa hapo darajani inasikitisha sana, umaridadi wake umepotea na imekuwa ni kadhia tu kupita katika mtaa huo sio mchana wala usiku. Eneo la darajani ambalo limepakana na barabara ya Benjamin Mkapa(greek road), kwa sasa halina taa na linategemea taa zenye mwanga hafifu toka kwenye maduka na makontena,huku yakiongezewa nguvu na kandiri za wauza vitambaa.

Kama kawaida sababu tele za kujaza pakacha la mkaa zinaweza kutolewa kutokana na uchakavu wa eneo hilo, pasipo kutoa hatua madhubuti ambazo zinaweza kuchukuliwa japo kuboresha eneo hilo maarufu kwa biashara.

Labda tuwasubiri Agha Khan wakimaliza kukarabati soko la chakula la jioni, labda watawakumbuka wauza vitambaa wa hapo darajani. Maanake sio Manispaa ya Mji wala hao wenye Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe wenye nia na uwezo wa kuboresha eneo hilo.

No comments: