Monday, 2 February 2009

Mapenzi ya Tanzania Bara na Zanzibar mashakani...


Wengi wetu siku hizi tunapenda kufananisha muungano wa Tanganyika na Zanzibar na ndoa ya watu wawili wapendano. Ndoa huja baada ya wawili walioshibana kuamua kuishi pamoja kwa muda wote wa maisha yao. Zipo aina kadha wa kadha za ndoa zote hizo huwa na lengo moja la kuunganisha wale wapendanao.

Mapenzi siku zote uzaliwa na kukua na hatimae kupevuka, siku zote mapenzi hukuzwa na wapendanao kwa kujaribu kuheshimu yale apendayo mwenza wake. Hii ni kwa kila upande na sio jukumu la mmoja tu ndani ya hayo mapenzi. Yapo mambo mengi ambayo ufanyika kwa lengo la kudumisha na kuendeleza mapenzi. Na haya yote hufanyika kwa moyo wa dhati ili mradi tu kuona penzi linakuwa kila siku.

Tofauti ndogo ndogo siku zote uwepo katika mapenzi, na wale ambao hupenda kuona mafanikio na kudumisha mapenzi yao hupenda kuzijadili tofauti hizo kungali mapema ili kuzuia tofauti hizo kuwa tatizo baina yao. Hii ni mojawapo ya vitu vya msingi sana katika ndoa zinazojali mapenzi.

Ndoa ya Tanzania Bara na Zanzibar sasa ipo kwa muda mrefu kiasi cha kusema kuwa imekomaa ila mapenzi katika ndoa hii muhimu yamekuwa yakipungua kila siku na katika spidi kubwa kiasi cha kuhatarisha ndoa yenyewe.Vitu vyote muhimu katika kukuza penzi zimewekwa kando badala yake chuki na kusingamana vimechukua nafasi.

Katika nyakati tofauti tumeshuhudia mambo kadha wa kadha yakifanyiwa marekebisho ili mradi kulienzi penzi na kudumisha ndoa, tokea wakati ule wa kusafiri kwa passport hadi kuongezwa kwa mambo kadhaa ndani ya ndoa hiyo. Hata hivyo kwa upande mmoja wa wanandoa hawa amekuwa akiburuzwa mno, mambo mengi amekuwa akinyang'anya tokea kuwa na sauti ya pili kwa ukuu ndani ya ndoa hiyo hadi sasa ambapo hana sauti yoyote, hata uhalali wake umeanza kuhojiwa, mbaya zaidi pamoja na kukubali kufutwa kwa kutumia karatasi baina ya nchi mbili hizi, inashangaza sana kuona kuwa makaratasi yameondolewa kwa binadamu tu.Iwapo una gari ukitokea upande wa Visiwani, gari hilo linabidi kuwa na karatasi ili liweze kutembea upande wa pili wa ndoa.

Kuna kero zingine zinachosha sana, na wala hazisaidii kurutubisha ndoa zaidi ya kuitia ubovu ambao mwisho wake ni kuvunjika tu.

No comments: