Wednesday 25 March 2009

Huu Ndio Wakati Muafaka wa Kumiliki gari la Waziri wa SMZ


Mara kadhaa nimewahi kuandika juu ya ubabe wa SMZ dhidi ya Mahkama za Zenj, zaidi ya SMZ hata wananchi wakati mwingine wamekuwa na ubabe dhidi ya maamuzi ya Mahkama za Zenj. Kumekuwepo na hukumu mbalimbali kila siku, ila zinazonipa mashaka ni zile hukumu za kesi za madai. SMZ kama mhimili wa Mahkama imekuwa kwa mara kadhaa ikishitakiwa katika kesi za madai kutoka na ubabe wake wa kushindwa kufuata sheria zake.

Kesi nyingi ambazo SMZ na asasi zake zimekuwa zikijikuta matatani zinatokana na matatizo ya ardhi na madeni yanayotokana na huduma mbalimbali wanazoomba kufanyiwa na hatimae kushindwa kulizipia. Mwaka 2006 niliwahi kuandika jinsi gani Mahakama za Zenj zinapoonja ubabe wa SMZ na wananchi wake kiasi cha mtu kujiuliza iwapo utakuwa na matatizo ambayo yanahitaji haki kutendeka utakimbilia wapi!

Mwaka huo wa 2006 kulikuwa na kesi mbili za muda mrefu ambazo zilipata hukumu yake, lakini zikakutana na ubabe wakati wa utekelezaji wake, kama inavyoelezwa kwa kirefu chini ya bandiko la "Mahakama za Zenj na Matatizo ya Ubabe"

SMZ kwa kujua au kwa makusudi kabisa imekuwa ikipuuza madai mengi ya wananchi wake dhidi ya asasi yake. Nakumbuka kesi nyingi katika hili lakini moja iliyonivutia ni ile ya asasi moja ya SMZ kuibeza amri ya Mahkama kuhusu uvunjaji wa mabanda ya biashara ili kupisha ujenzi wa soko katika eneo la Mwanakwerekwe.

Wengi wa wananchi wamekuwa na madai mbalimbali na wanapokimbilia katika vyombo vya SMZ ili kupata suluhisho, uvunjika moyo jinsi wanavyosumbuliwa na inahitaji moyo wa ziada kwenda Mahakamani ambako ni sawa na kumpa Nyani kesi ya Ngedere. Binafsi nimekuwa nikipigwa tarehe zaidi ya miaka tisa kwa madai ya haki yangu ambayo niliingia mkataba na SMZ.

Hatua ya Mahakama Kuu kupiga mnada magari ya SMZ kwa kushindwa kulipa deni lake la matengenezo ya ikulu ndogo huko Pemba ni ya kuungwa mkono sana. Amri hii iwapo itafanikiwa itakuwa ya kuigwa na kupigiwa mfano. Moja ya mali ambayo inaweza kupigwa mnada ni gari la Mh. Waziri ambae wizara yake inahusika moja kwa moja na kushindwa kufuata taratibu za kuheshimu mikataba. Nategemea jeshi la polisi visiwani humo kusimamia vizuri ushikwaji wa mali hizo za SMZ na hatimae kupigwa mnada. Hii inaweza kuondoa usingizi mzito kwa watendaji wa SMZ kuhusu kuheshimu mikataba wanayoingia.

No comments: