Sunday, 26 April 2009

Muungano unazidi kukua, miaka 45 sio mchezo...


Katika kusherehekea miaka 45 ya Muungano nimejikuta nikikumbuka sana shoki shoki, matunda yenye radha ya aina yake ni maarufu sana hapo Zenj. Anyway lengo ni kusherekea muungano, miaka 45 sio mchezo! Muungano huu ambao ulizaliwa na mambo kumi na moja, sasa una mambo 38 na bado una kero ambazo kuchwa zinapigiwa kelele! Sasa cha kujiuliza muungano huu unakua au unapolomoka. Ukiangalia idadi ya mambo yanayounganisha nchi mbili hizi utaona kama unakua na kama unakuwa unaelekea upande gani? Kuunganisha kila jambo na kuwa na serikali moja?

Hata hivyo dalili zinaonyesha kuwa mengi kati ya hayo 38 yameingizwa kwa upande mmoja kuburuzwa na upande mwingine, ndio maana kumezaliwa neno kero za muungano! Kwa hali ya sasa dalili za kukua kwa muungano huu ni kidogo kuliko kukua kwa kero zake! Nini kifanyike? yarudishwe yale 11 ya mwanzo au haya ya sasa yajadiliwe kwa kina na kuondoa hizo kero. Je ni upande mmoja tu wa muungano ambao unaona kuna kero? na kama ni hivyo upande mwingine wa muungano unajisikia vipi kukaa kimya na kutosikiliza kero za upande mwingine? Ni kiburi ama dharau? Au kuna ajenda ya siri?

Nawatakiwa kila heri watanzania wote katika siku hii muhimu ya kuzaliwa kwa Tanzania.

Saturday, 18 April 2009

Kisauni Airport kuongezwa kwa mita 560


Zanzibar International Airport maarufu duniani kama Kisauni Airport inatazamiwa kuongezwa urefu wa njia yake kwa mita 560. Ni katika mradi uliopatiwa fedha na Benki ya Dunia.
Uwanja wa Kisauni umekuwa ukifanyiwa matengenezo mara kwa mara, ili kukidhi ongezeko la matumizi ya uwanja huo na hasa baada ya kukua kwa sekta ya utalii visiwani humo.

Matengenezo haya yatajumuisha ukarabati wa jengo la uwanja pamoja na utiaji wa uzio katika baadhi ya maeneo ya uwanja huo ambayo yapo hatarini kuvamiwa kwa ujenzi wa nyumba za kuishi. Aidha kampuni itakayofanyia matengezeno uwanja huo Sogea Satom ya Ufaransa imenukuliwa ikisema kazi hiyo itachukua muda wa mwaka mmoja na miezi mitatu kukamilika.Wednesday, 15 April 2009

Zenj kuondokana na mafuta ya kwenye Rambo
Japo mtaalamu wa uchunguzi wa kuwepo kwa mafuta katika visiwa vya Zenj alisema mafuta katika visiwa hivyo hayatoshi kwa uchimbaji wa kibiashara, Wawakilishi walimjibu kuwa hata kama ni kidogo kwa ujazo wa kinibu, mafuta hayo ni kwa ajili ya Wazenj na watagawana hivyohivyo! Mbaya zaidi kwa mtaalamu huyo kupendekeza kuwa mafuta hayo yawe chini ya Muungano, jambo ambalo lilizua jambo lingine kwa mahasimu wa siasa visiwani humo kukaa pamoja na kupinga kwa nguvu zote kauli ya mtaalamu huyo aliyejikusanyia vijisenti kadhaa baada ya kukamilisha ripoti yake.

Kadhia ya upitikanaji wa mafuta visiwani humo imekuwa ya muda mrefu licha ya kuwepo kwa vituo vya kutosha kwa ajili ya uuzaji wa mafuta hayo. Watumia vyombo wanajua usumbufu mkubwa wanaoupata wakati bidhaa hiyo adimu inapokosekana visiwani humo.Kiasi cha kufikia kununua mafuta vichochoroni tena yaliyohifadhiwa katika maplastiki na vifuko vya Rambo.Usumbufu huu hauishii kwa wenye vyombo tu bali utambaa na kuenea kwa kila mwananchi wa visiwa hivyo kwa namna moja ama nyingine.

Kauli ya Waziri Mansoor Yusuf Himid katika suala la mafuta aliyoitoa hivi karibuni, inabainisha wazi kuwa serikali ya muungano wa tz(SMT)kupitia shirika lake la TPDC limekuwa likifanya uchunguzi na utafutaji wa mafuta katika visiwa vya Zenj kinyume na makubaliano ya ndoa...Muungano wa Tanganyika na Zenj. TPDC kwa zaidi ya miaka kumi sasa imekuwa ikiingia mikataba na kampuni za uchunguzi wa mafuta katika maeneo ya kujidai ya visiwa hivyo kana kwamba suala la mafuta ni la Muungano. Wawakilishi kwa upande wao walisimamia kidete kuzuia TPDC kunusanusa uwepo wa mafuta katika visiwa hivyo, huku wananchi wa visiwani wakisuburi kwa hamu kujua ubavu wa SMZ dhidi ya SMT.
Waziri Mkuu wa SMT Mizengo Pinda, kwa kuona kuwa kuna tatizo hapo amekubaliana na Waziri Kiongozi wa SMZ Nahodha kuwa mafuta katika Zenj yafanyiwe uchunguzi na wazenj wenyewe na kuweza kuyachimba wao wenyewe hata kama ni kidogo kwa kuweza kujipaka mwilini kwa siku mbili tu. Ingawa kaurusha mpira kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano ili kutoa kauli ya mwisho juu ya mstakabala wa mafuta.

Kinachoshangaza hapo ni kwanini suala hili lipelekwe kwenye Bunge ilhali Bunge hilo haliyawahi kukaa hata siku moja na kusema kuwa mafuta ni suala la muungano? zaidi ya watendaji wa SMT kwa utashi wao binafsi kuliingiza suala hili ndani ya Muungano! Hiki ni kichekesho kikubwa katika kadhia za Muungano huu!

Kinachofurahisha ni jinsi gani SMZ mara hii ilivyoweza kukataa kuburuzwa na SMT. Kuna mambo mengi ambayo SMZ imekuwa ikipelekweshwa mbio na kuna mengi ambayo yamekuwa yakiingizwa kwenye SMT pasipo kuwashirikisha wazenj, ambapo uhambulia taarifa tu kuwa jambo fulani lipo kwanye Muungano!

Ili kulinda na kuendeleza Muungano huu ni vema kwa SMT kuacha tabia yake ya muda mrefu ya kujichukulia uwamuzi pasipo kuwashirikisha wenzao wa SMZ. Ni vema wakakumbuka kuwa Muungano huu ulifikiwa kwa makubaliano ya nchi mbili tena kwa mambo kadhaa na sio sahihi kuongeza mambo mengine bila ridhaa ya upande pili. Hali kadhalika SMT waache kujisahau kuwa wana nafasi sawa na SMZ katika hatima ya muungano huu na hivyo ni vema wakawa na heshima!

Tuesday, 7 April 2009

Leo ni siku ya Karume


Watanzania leo wanaungana na ndugu zao wa Zenj katika siku hii muhimu ya kumbukumbu ya A.Karume rais wa kwanza wa Zanzibar na Muasisi wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.