Wednesday 15 April 2009

Zenj kuondokana na mafuta ya kwenye Rambo




Japo mtaalamu wa uchunguzi wa kuwepo kwa mafuta katika visiwa vya Zenj alisema mafuta katika visiwa hivyo hayatoshi kwa uchimbaji wa kibiashara, Wawakilishi walimjibu kuwa hata kama ni kidogo kwa ujazo wa kinibu, mafuta hayo ni kwa ajili ya Wazenj na watagawana hivyohivyo! Mbaya zaidi kwa mtaalamu huyo kupendekeza kuwa mafuta hayo yawe chini ya Muungano, jambo ambalo lilizua jambo lingine kwa mahasimu wa siasa visiwani humo kukaa pamoja na kupinga kwa nguvu zote kauli ya mtaalamu huyo aliyejikusanyia vijisenti kadhaa baada ya kukamilisha ripoti yake.

Kadhia ya upitikanaji wa mafuta visiwani humo imekuwa ya muda mrefu licha ya kuwepo kwa vituo vya kutosha kwa ajili ya uuzaji wa mafuta hayo. Watumia vyombo wanajua usumbufu mkubwa wanaoupata wakati bidhaa hiyo adimu inapokosekana visiwani humo.Kiasi cha kufikia kununua mafuta vichochoroni tena yaliyohifadhiwa katika maplastiki na vifuko vya Rambo.Usumbufu huu hauishii kwa wenye vyombo tu bali utambaa na kuenea kwa kila mwananchi wa visiwa hivyo kwa namna moja ama nyingine.

Kauli ya Waziri Mansoor Yusuf Himid katika suala la mafuta aliyoitoa hivi karibuni, inabainisha wazi kuwa serikali ya muungano wa tz(SMT)kupitia shirika lake la TPDC limekuwa likifanya uchunguzi na utafutaji wa mafuta katika visiwa vya Zenj kinyume na makubaliano ya ndoa...Muungano wa Tanganyika na Zenj. TPDC kwa zaidi ya miaka kumi sasa imekuwa ikiingia mikataba na kampuni za uchunguzi wa mafuta katika maeneo ya kujidai ya visiwa hivyo kana kwamba suala la mafuta ni la Muungano. Wawakilishi kwa upande wao walisimamia kidete kuzuia TPDC kunusanusa uwepo wa mafuta katika visiwa hivyo, huku wananchi wa visiwani wakisuburi kwa hamu kujua ubavu wa SMZ dhidi ya SMT.
Waziri Mkuu wa SMT Mizengo Pinda, kwa kuona kuwa kuna tatizo hapo amekubaliana na Waziri Kiongozi wa SMZ Nahodha kuwa mafuta katika Zenj yafanyiwe uchunguzi na wazenj wenyewe na kuweza kuyachimba wao wenyewe hata kama ni kidogo kwa kuweza kujipaka mwilini kwa siku mbili tu. Ingawa kaurusha mpira kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano ili kutoa kauli ya mwisho juu ya mstakabala wa mafuta.

Kinachoshangaza hapo ni kwanini suala hili lipelekwe kwenye Bunge ilhali Bunge hilo haliyawahi kukaa hata siku moja na kusema kuwa mafuta ni suala la muungano? zaidi ya watendaji wa SMT kwa utashi wao binafsi kuliingiza suala hili ndani ya Muungano! Hiki ni kichekesho kikubwa katika kadhia za Muungano huu!

Kinachofurahisha ni jinsi gani SMZ mara hii ilivyoweza kukataa kuburuzwa na SMT. Kuna mambo mengi ambayo SMZ imekuwa ikipelekweshwa mbio na kuna mengi ambayo yamekuwa yakiingizwa kwenye SMT pasipo kuwashirikisha wazenj, ambapo uhambulia taarifa tu kuwa jambo fulani lipo kwanye Muungano!

Ili kulinda na kuendeleza Muungano huu ni vema kwa SMT kuacha tabia yake ya muda mrefu ya kujichukulia uwamuzi pasipo kuwashirikisha wenzao wa SMZ. Ni vema wakakumbuka kuwa Muungano huu ulifikiwa kwa makubaliano ya nchi mbili tena kwa mambo kadhaa na sio sahihi kuongeza mambo mengine bila ridhaa ya upande pili. Hali kadhalika SMT waache kujisahau kuwa wana nafasi sawa na SMZ katika hatima ya muungano huu na hivyo ni vema wakawa na heshima!

No comments: