Saturday, 2 January 2010

Mapacha Walioungana Wazaliwa Zenji...

Mwanamke mmoja mkazi wa Zanzibar, Farihati Maulid (18) amejifungua watoto pacha wa kiume walioungana.

Mwanamke huyo alijifungua kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Mnazi Mmoja jana saa tatu asubuhi na mapacha hao wako katika chumba cha uangalizi maalumu.

Mkunga wa hospitali hiyo, Halima Habiba Abdallah, na Dk. Mwana Omar ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Uzazi, wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema tukio hilo ni la kwanza kwa muda mrefu katika hospitali hiyo wanaendelea kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wengine wa afya.

Pacha hao wana moyo mmoja, na wameunganika kuanzia kwenye kitovu hadi kwenye mfupa wa kidari.

“Tunasubiri wataalamu kufanya uchunguzi zaidi, lakini kwa sababu wana moyo mmoja na wana uzito wa kilo 2.8 itakuwa ngumu kuwatenganisha na kupona, haijulikani ni viungo gani vingine kila mmoja anavyo vya peke yake,” alisema Dk. Omari.

Habari zaidi zinasema mama wa watoto hao ni mkazi wa Mwanyanya, Bububu katika Manispaa ya Zanzibar na mimba hiyo ilikuwa ya kwanza.

2 comments: