Thursday 14 January 2010

Maridhiano na Mustakbali wa Zanzibar


MARIDHIANO NA MUSTAKBALI WA ZANZIBAR

Na Seif Sharif Hamad

UTANGULIZI

Zanzibar inapita katika mojawapo ya vipindi muhimu sana vya historia yake ya kisiasa. Nuru mpya ya matumaini imechomoza kupitia Maridhiano ya Wazanzibari. Hatua hii imekuja kufuatia mkutano na mazungumzo ya kihistoria kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dk. Amani Karume, na mimi nikiwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) huko Ikulu ya Zanzibar , Novemba 5, 2009 yaliyokuwa na lengo la kujenga mustakbali mpya wa siasa Zanzibar .

Mazungumzo hayo yalifuatiwa na hatua ya kijasiri ya CUF ya Novemba 7, 2009 ya kwenda hadharani kutangaza kumtambua Rais Karume na Serikali anayoiongoza na kukubali kushirikiana na kufanya naye kazi pamoja kwa maslahi ya Zanzibar na watu wake.

Pamoja na hatua hiyo kuonekana kuwachanganya wana-CUF pale ilipotangazwa kwao kwa mara ya kwanza, lakini viongozi wa CUF tukiongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Prof. Ibrahim Lipumba, hatukuyumba wala kurudi nyuma na tukaamua kufanya kazi kubwa ya kuwaelimisha wanachama kupitia mikutano ya hadhara na vikao vya ndani hadi kufikia hatua ya sasa ambapo wana-CUF takriban wote sasa wanakubaliana na hatua zinazochukuliwa. Ushiriki mkubwa na wa aina yake wa wana-CUF katika kilele cha sherehe za miaka 46 ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 zilizofanyika kisiwani Pemba ni ushahidi tosha wa hali hiyo ninayoieleza. Nataka nitumie fursa hii kuwashukurukwa dhati wana-CUF wote kwa kutuelewa na kutuunga mkono katika hatua zetu hizi tunazozichukua.

Kwa upande wake, Rais Amani Karume naye amehutubia mkutano wa hadhara wa CCM Novemba 22, 2009 na kutoa hotuba iliyotoa mwelekeo mpya wa mahusiano ya kisiasa hapa Zanzibar . Pamoja na mambo mengine, alitangaza kwamba milango iko wazi kuweza kuzungumza jambo lolote lenye maslahi na Zanzibar na watu wake. Hotuba zake za hivi karibuni alipokuwa katika ziara rasmi kisiwani Pemba na baadaye katika matukio mbali mbali ya Sherehe za Mapinduzi zimeendelea kusisitiza azma yake ya kujenga Zanzibar mpya yenye umoja, maelewano, mshikamano, amani, utulivu na maendeleo kwa watu wake wote.

Nafurahi kuona hotuba zetu, mimi na Rais Karume, tukiwa ndiyo viongozi wakuu wa kisiasa hapa Zanzibar zimesaidia kuyazamisha maridhiano haya katika nyoyo za wafuasi wa vyama vya CCM na CUF na pia katika nyoyo za Wazanzibari wote. Zanzibar inashuhudia hali ya matumaini ambayo haijapata kuonekana kwa miaka mingi.

Kiwango cha kuaminiana kimekuwa cha juu kabisa na hatua ya karibuni ya Rais Amani Karume kutangaza kuwateua viongozi wawili waandamizi wa CUF, Mhe. Juma Duni Haji na Mhe. Nassor Ahmed Mazrui, kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi imepokelewa kwa furaha kubwa kuwa ni hatua sahihi katika kuimarisha maridhiano yaliyofikiwa.

Umuhimu wa hatua tunazochukua umeonekana kutokana na kauli mbali mbali za viongozi wa ndani na hata nje ya nchi, taasisi zisizo za kiserikali na jumuiya mbali mbali za kiraia, wasomi, viongozi wa dini na wengine wengi za kupongeza hatua hizo. Nachukua fursa hii kuwashukuru wote hao kwa kutuunga mkono katika hili. Lakini na mimi pia naungana na Rais Karume katika kumpa shukrani nyingi na za pekee Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania , Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, kwa salamu zake za pongezi kwetu ambazo siyo tu zilibeba ujumbe mzito kwa wale wote wanaobeza hatua tuliyochukua lakini pia zilikuwa zimeambatana na ahadi yake kwamba anatuunga mkono kwa hatua tunazochukua na kwamba tutegemee kila msaada tunaouhitajia kufanikisha yale tuliyoyakusudia. Binafsi nimefarijika sana na ahadi yake hiyo kwani hapana shaka yoyote kwamba msaada wake unahitajika sana .

Ukiacha salamu hizo za pongezi, Wazanzibari wengi wameifurahia hatua tuliyochukua na wana matumaini makubwa kuwa itafungua milango mikubwa zaidi ya mashirikiano. Bila shaka wapo pia vidudu mtu wachache ambao wanafanya kila juhudi kutaka kuturudisha kule kule tulikotoka kwa sababu tu ya kujali maslahi yao . Natoa wito kwa wananchi wote kwamba wawapuuze na nawahakikishia kwamba mimi na Rais Karume tumekubaliana kuwa hakuna kurudi nyuma katika hatua tuliyoianzisha. Ni nia yetu kuona kuwa tunaitumia fursa hii kuirudisha Zanzibar katika nafasi yake iliyokuwa nayo huko nyuma ambayo ilipotea kutokana na kuendekeza kwetu tofauti zetu badala ya yale yanayotuunganisha. Time has come to make Zanzibar great and proud of herself again.

ZANZIBAR ILIKOTOKA

“Ipigwapo zumari Zanzibar , hucheza walioko katika Maziwa Makuu.” Huu ni usemi wa kihistoria unaoeleza nafasi kubwa viliyokuwa nayo visiwa vyetu katika kusarifu na kushawishi mwenendo wa mambo katika eneo la Afrika Mashariki na Kati. Hizo zilikuwa zama za Zanzibar kuvuma kutokea upande huu wa magharibi ya Bahari ya Hindi kuelekea ndani ya Bara la Afrika hadi mashariki ya Congo na pia kuelekea sehemu za kaskazini kwenda Bara Arabu, Bara Hindi na Mashariki ya Mbali na pia kupenya hadi Ulaya na Marekani.

Udogo wa visiwa vya Zanzibar haulingani na umuhimu wake katika historia ya Afrika Mashariki, Bahari ya Hindi, Arabuni hadi Mashariki ya Mbali. Umuhimu huo ulitokana na maendeleo makubwa yaliyokuwa yamepigwa Zanzibar katika nyanja mbali mbali za maisha. Na hali hiyo haikuja kwa bahati mbaya bali ilitokana na ustaarabu uliojengeka karne nyingi sana zilizopita. Inatambulika, kwa mfano, kwamba Zanzibar , au Dola ya Zinj, ndiyo dola kongwe kuliko zote katika eneo lote la Afrika kusini ya jangwa la Sahara .

Watu wa visiwa vya Zanzibar walitoka sehemu mbali mbali: Afrika ya Mashariki na Kati , Iran , Arabuni, Bara Hindi, Ngazija, Mashariki ya Mbali, Ulaya n.k.

Zanzibar inaelezwa kutajwa kwa majina tofauti tangu miaka 500 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (a..s.). Uvumbuzi wa karibuni wa mapango ya watu wa kale katika ukanda wa Mashariki Kusini wa kisiwa cha Unguja unaonesha kuwepo kwa makaazi ya watu tokea zama za mawe ziitwazo kama ‘Stone Age’. Katika kitabu maarufu chenye kumbukumbu za wasafiri wa kale wa Ugiriki waliotembelea mwambao wa Afrika Mashariki kiitwacho Periplus of the Erythrean Sea kilichoandikwa mwaka 100 A.D. (kabla ya Nabii Issa), Zanzibar imetajwa kwa jina la ‘Menouthias’ ikiwa tayari ni nchi yenye watu mchanganyiko tena walio na ustaarabu wakiwa wanavaa nguo za hariri. Huko Oxford, imeonekana ramani ya wasafiri wa Kiarabu iliyotayarishwa Karne ya 11 ambayo inaonesha visiwa vya Zanzibar na mji mkuu wake ukiwa Unguja Ukuu.

Kwa muda mrefu, Zanzibar ilikuwa imegawanyika katika falme mbali mbali, mpaka ilipofika mwaka 1500 ulipoanzishwa utawala wa Mwinyi Mkuu akiwa ndiyo alama ya utawala wa kienyeji Visiwani. Mwinyi Mkuu wa mwisho, Ahmed bin Muhammed bin Hassan el-Alawy alifariki 1873. Mwaka 1503 Wareno waliivamia Zanzibar kupitia Unguja Ukuu na wakaitawala kwa muda mrefu wakifanya vitimbi vya kila aina. Waomani kwa maombi ya wenyeji walikuja katika Dola ya Zinj na kupambana na Wareno na hatimaye wakafanikiwa kuwatimua. Sayyid Said bin Sultan alifika Zanzibar mwaka 1828, na kutokana na kuvutiwa na mandhari yake mwaka 1832 akaifanya Zanzibar kuwa makao makuu ya utawala wake badala ya Muscat .

Katika kipindi hiki Zanzibar iliweza kujitambulisha na kutambuliwa kama Dola huru katika ulimwengu. Zanzibar ikawa kituo muhimu cha kisiasa, kiuchumi na kibiashara katika Afrika Mashariki na Bahari ya Hindi.. Kutokana na umuhimu wake, Madola makubwa yalifungua Ofisi za Kibalozi mjini Zanzibar : Marekani (1837), Uingereza (1841), Ufaransa (1844), na baada ya hapo Ureno, Utaliana, Ubelgiji na Ujarumani zikafuata.

Madola ya Ulaya yalipoanza njama za kinyang’anyiro cha Afrika kwa lengo la kuigawanya kuwa katika makoloni yao , Zanzibar iligombaniwa baina ya Waingereza na Wajarumani. Baada ya vuta nikuvute, mwaka 1890 iliwekwa chini ya Himaya ya Kiingereza (Protectorate) katika Mkataba uliotiwa saini kati ya Mfalme wa Kiingereza na Sayyid Ali bin Said na kwa kutambua hadhi tofauti ya Zanzibar , masuala yake yalikuwa yakiendeshwa kupitia Wizara ya Mambo ya Nje (Foreign Office) ya Uingereza. Mwaka 1913, masuala ya utawala wa Zanzibar yalihamishwa kutoka Ofisi ya Mambo ya Nje (Foreign Office) na kupelekwa rasmi Ofisi ya Makoloni (Colonial Office).

Kidogo kidogo, harakati za kuanzisha mfumo wa Utawala wa sura ya kikoloni zikaanza pale ilipotungwa Sheria (Order-in-Council) ya 1926 iliyoanzisha Baraza la Kutunga Sheria (LegCo) na Baraza la Utawala (ExCo). Ni katika kipindi hicho ambapo mfumo wa uwakilishi wa kikabila ulianzishwa ukiwaweka kando Waafrika na Washirazi na hivyo kupanda fitina za mifarakano chini ya sera ya Waingereza ya ‘wagawe uwatawale’ (divide and rule). Ilichukua miaka 20, hadi mwaka 1946, ambapo Mshirazi wa kwanza, Sheikh Ameir Tajo, aliteuliwa kuingia katika Baraza la Kutunga Sheria akifuatiwa na mwenzake, Sheikh Ali Shariff Mussa, aliyeteuliwa mwaka 1948.

Miaka ya 50 ilishuhudia harakati za kudai uhuru kwa kuundwa vyama vya ukombozi: Zanzibar Nationalist Party (ZNP) kilichoasisiwa 1955 na Afro Shirazi Party (ASP) kilichoundwa 1957. Katika kipindi cha miaka saba ya mchuano mkali wa nani anafaa kukabidhiwa Uhuru wa Zanzibar, kulifanyika chaguzi nne ambazo ni Julai 1957, Januari 1961, Juni 1961 na Julai 1963. Chaguzi hizo zilishindwa kuwaweka pamoja Wazanzibari na badala yake zikawa chachu ya kugawika kwa jamii kati ya mapande mawili yenye nguvu takriban sawa sawa. Hali ikazidi kukorogeka pale vyama hivyo vikuu navyo vilipopasuka ambapo Afro Shirazi Party ilimeguka na kupelekea kuanzishwa Zanzibar and Pemba Peoples Party (ZPPP) mwaka 1959 na Zanzibar Nationalist Party nayo ikapasuka na kupelekea kuanzishwa Umma Party mwaka 1963. Zanzibar ikawa inaelekea katika Uhuru ikiwa ni jamii iliyogawanyika.

Uingereza ilikabidhi Uhuru kwa Zanzibar tarehe 10 Desemba 1963 chini ya Sultani na Serikali ya ZNP/ZPPP. ASP hawakuubali Uhuru huo na tarehe 12 Januari, 1964 ilifanya Mapinduzi na Zanzibar ikatangazwa kuwa Jamhuri.

Haya niliyoyaeleza ni mukhtasari tu wa historia ya Zanzibar unaoonesha vipindi mbali mbali ambavyo nchi ilipitia katika ujenzi wa Taifa.

Lakini pamoja na misukosuko ya kisiasa tuliyokumbana nayo, ni vyema ikaeleweka na hususan kwa vijana wa leo kwamba Zanzibar hii imeweka rekodi mbali mbali za kujivunia na kutoa mchango mkubwa katika maendeleo ya binadamu na ustaarabu. Ni vijana wangapi leo hii wanaojua kwamba mji wa Zanzibar ulikuwa wa mwanzo kuwasha taa za umeme za barabarani na mitaani (zikiitwa taa za stimu) kabla ya miji ya London na New York ? Balozi wa Marekani aliyemaliza muda wake mwaka jana, Bwana Mark Green, wakati akitoa hotuba yake ya kuaga, alisema meli za Marekani zilikuwa zikitia nanga katika bandari ya Zanzibar kuja kununua mafuta ya nyangumi kwa ajili ya kwenda kuwashia taa zao za barabarani wakati Zanzibar ikiwa inatumia umeme. Sayyid Said bin Sultan alipeleka Balozi wa kwanza wa Zanzibar nchini Marekani, Ahmed bin Nu’man mwaka 1840.

Zanzibar ilikuwa nchi ya kwanza kuwa na sarafu yake katika Afrika kusini ya Sahara zilizoanzishwa wakati wa Tawala za Kishirazi ambazo zilichimbuliwa katika maeneo ya Unguja Ukuu, Mkumbuu na Mtambwe Mkuu katika miaka ya tisini. Baadaye katika mwaka 1908, ikawa tena nchi ya kwanza katika eneo hili kuanzisha sarafu za noti zake wenyewe (rupia za Zanzibar ) ambazo ziliendelea kutumika hadi 1936 ilipoanzishwa sarafu ya shilingi ya Afrika Mashariki chini ya Bodi ya Sarafu ya Afrika Mashariki.

Zanzibar ilikuwa nchi ya kwanza katika eneo hili kufunga mikataba ya kibiashara na nchi za Marekani, Uingereza, Ufaransa na Jiji la Hamburg (kabla ya kuanzishwa kwa Shirikisho la Ujarumani). Zama hizo, nchi yetu pia ilikuwa na mahusiano ya kibiashara na nchi za Arabuni , India , China , Malaysia na visiwa vya Java na Sumatra (ambavyo sasa ni Indonesia ) na kupitia mahusiano hayo, iliweza kujenga utamaduni na ustaarabu wa kipekee.

Wakati Zanzibar inapata uhuru wake, ilikuwa nchi ya pili katika Afrika kwa ukubwa wa wastani wa pato la wananchi wake, na ya tatu kwa kiwango cha elimu na pia ikiwa na taasisi 17 za fedha zikiwemo benki na kampuni za bima.

Haya yalikuwa katika kipindi cha kabla ya Mapinduzi ya 1964 lakini hata baada ya Mapinduzi, nafasi ya Zanzibar katika Afrika haikupotea. Ilikuwa nchi ya kwanza katika Afrika kusini ya Jangwa la Sahara kuanzisha televisheni ya rangi na pia ikitoa huduma zote muhimu za jamii bure kwa wananchi wake. Ilifikia wakati ambapo Rais wa kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar , Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, alitangaza hadharani kwamba hakukuwa na nchi yoyote iliyokuwa ikiidai Zanzibar bali Zanzibar ndiyo iliyokuwa ikizidai baadhi ya nchi malimbikizo ya madeni yanayotokana na uuzaji wa karafuu zake.

Nimeamua kuchukua muda mrefu kidogo kuyadondoa haya ili tujue wapi nchi yetu ilikotoka na kwa vipi migogoro ya kisiasa iliyokuja kuvigubika visiwa vyetu na wananchi wake ilikuja kutuathiri vibaya na kuyapoteza mengi kati ya haya.


CHAGUZI: SUMU YA UMOJA WA WAZANZIBARI

Sina haja ya kurejea historia ya chaguzi mbali mbali zilizofanyika hapa Zanzibar kabla na baada ya Mapinduzi ili kuthibitisha hoja yangu kwamba chaguzi zimekuwa ndiyo sumu ya umoja wa Wazanzibari.

Ni bahati mbaya sana kwamba maendeleo ya kisiasa ya harakati za kudai uhuru wa Zanzibar yaliyoshika kasi kuanzia uchaguzi mkuu wa mwanzo visiwani wa 1957 yaliibua hisia kali zinazotokana na matukio ya vipindi mbali mbali vya historia ambavyo viliambatana na mapambano ya kitabaka na hivyo kupelekea siasa za wakati huo kugubikwa na wimbi la chuki, hasama na kutoaminiana lililokuwa limejikita kwa miongo kadhaa. Vyama vya siasa vilipokuja kuundwa havikuweza kukwepa athari hii na matokeo yake yakawa ni mapambano ya vuta nikuvute ambayo yalipelekea vurugu na fujo zilizoambatana na roho za watu kupotea. Kila kitu katika maisha ya Mzanzibari kikawa ni siasa. Shughuli zote za maisha ya kila siku zikawa zinafanywa kwa misingi ya vyama vya siasa. Jamii ya Zanzibar ikawa imegawanyika kati kati.

Bila shaka mbali na matukio hayo ya kihistoria, pia kulikuwa na athari mbaya za baadhi ya nchi jirani na za mbali ambazo zilikuwa na khofu kubwa na umaarufu wa Zanzibar , nchi ambazo ziliamua kujipenyeza katika siasa zetu na kuchochea na hata kuikoleza mifarakano iliyokuwepo.

Kabla ya Mapinduzi, chaguzi zikitegemea wingi wa viti ili kupata mshindi wa kuunda serikali. Wingi wa kura haukuwa kigezo cha ushindi. Pamoja na kwamba utaratibu huu ulilalamikiwa na ASP kwa kule kupata kwake viti vichache wakati ikiwa na kura nyingi, wingi huo bado ulionesha kwa wastani mgawanyiko wa takriban nusu kwa nusu ya ushindi wa vyama vya wakati huo.

Katika mtiririko wa historia ya kisiasa ya Zanzibar , kielelezo kikubwa cha ukosefu wa kuaminiana kinaonekana katika uendeshaji wa uchaguzi na matokeo yake. Kama nilivyoeleza kabla, Zanzibar ilifanya chaguzi nne kabla ya Mapinduzi ya 1964 ambazo ni zile za Julai 1957, Januari 1961, Juni 1961 na Julai 1963 na imeshafanya chaguzi tatu tokea mfumo wa vyama vingi uliporudishwa yaani 1995, 2000 na 2005.

Katika chaguzi hizo zote zilizowahi kufanyika Zanzibar , ukiacha uchaguzi wa mwanzo wa 1957, hakujawahi kutokea uchaguzi wowote ambao washiriki wake waliridhika kikamilifu na uendeshaji wake na wakayapokea kwa moyo mkunjufu matokeo yake. ASP ililalamikia uendeshaji na matokeo ya chaguzi za Januari 1961, Juni 1961 na Julai 1963 na katika kipindi hiki cha kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi tokea mwaka 1992, CUF imelalamikia uendeshaji na matokeo ya chaguzi za 1995, 2000 na 2005. Kikubwa kinachokosekana ni imani kwa taasisi zinazoendesha na kusimamia chaguzi.

Ikiwa tunakubaliana na ukweli huu, ni wazi kwamba bila ya kushughulikia kiini hiki cha migogoro isiyokwisha katika siasa zetu basi ufumbuzi wa dhati na wa kudumu wa migogoro ya kisiasa hautapatikana.

Naamini kwa dhati kabisa njia mojawapo ya kujengeana imani kati ya kambi mbili kuu za kisiasa visiwani Zanzibar ni kuzifanya kambi hizo zifanye kazi kwa pamoja katika uendeshaji wa nchi.

Tafakuri ya kina ya hali ya mambo inavyokuwa wakati wa uchaguzi na pia dalili za kheri zilizooneshwa na Rais Amani Abeid Karume za kutaka kujenga mustakbali mpya wa kisiasa Zanzibar zilitufanya tuone haja ya kushirikiana naye ili kuwaunganisha Wazanzibari wawe kitu kimoja huku tukiamini kwamba katika umoja, tutaweza kuyafikia yale makubwa ambayo tumeshindwa kuyafikia kwa kule kufarikiana kwetu.


MARIDHIANO: FURSA ZILIZOKO MBELE YETU

Mmojawapo wa Marais wa Marekani anayeheshimika sana katika nchi yake na duniani kwa jumla, Abraham Lincoln, aliwahi kusema kuwa ‘A house divided against itself cannot stand’ yaani ‘Nyumba iliyogawanyika haiwezi kusimama’. Haya ni maneno yenye hekima kubwa sana . Ni wazi kwamba Zanzibar imepiga hatua kubwa za maendeleo katika sekta mbali mbali lakini ni jambo lisiloweza kupingika kwamba kama tutaendeleza umoja na mshikamano tunaouonesha hivi sasa na kufikia hatua ya kufanya kazi pamoja basi kuna faida na fursa nyingi na kubwa sana zinazoweza kutumiwa vyema kwa ajili ya kuiendeleza mbele zaidi nchi yetu na watu wake. Miongoni mwa faida za wazi za Maridhiano ni pamoja na:

1. Kisiasa: Kuondosha siasa za utengano, chuki, ubaguzi, uhasama, ugomvi na visasi miongoni mwa wananchi wetu na kuleta siasa za umoja, maelewano na mashirikiano.

2. Kiusalama: Kuondoa khofu na wasiwasi kwa kufuta viashiria vinavyoweza kuwa chanzo cha fujo na ghasia na ambavyo vingeweza kutumiwa hata na maadui wa Tanzania kuhatarisha usalama wetu na badala yake kuleta hali ya amani na usalama ambayo inavifanya hata vyombo vyetu vya ulinzi na usalama kufanya kazi zao katika hali ya utulivu na ushirikiano na wananchi wote.

3. Kiuchumi: Kuondoa hali iliyokuwepo ya sehemu ya wananchi kujiona hawashirikishwi au hawapaswi kushiriki katika harakati za ujenzi wa nchi na kuwaleta pamoja wananchi wote ili kwa pamoja tushiriki katika ujenzi wa Zanzibar mpya.

4. Kijamii: Kuondoa hali ya utengano na kutoaminiana miongoni mwa wafuasi wa vyama tofauti vya siasa na kuwafanya wapendane na washirikiane katika shughuli zote za kijamii wakijua kuwa wote ni wananchi wa nchi moja.

Tukizitumia vyema faida hizo zilizoletwa na maridhiano, tutaweza pia kuzitumia vizuri fursa zilizopo mbele yetu ili kuyabadili maisha ya watu wetu. Binafsi naamini kuwa sasa ile ndoto yetu ya muda mrefu ya kuifanya Zanzibar kuwa ni Hong Kong ya Afrika Mashariki itaweza kutimia ndani ya muda mfupi kabisa. Naamini Wazanzibari wote sasa watakunjua nyoyo zao na kila mmoja atapigana kikumbo na mwenzake katika kuona anatoa mchango mkubwa zaidi wa kuikwamua Zanzibar katika umasikini ambao hauna sababu ya kuwepo. Ubunifu na ari ya kutenda ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Mzanzibari.

Zanzibar ina utajiri mkubwa wa watu wake wenye vipaji na nafasi kubwa kubwa katika kila pembe ya dunia. Hawa tukiwatumia vyema na kuwapa fursa wanaweza kutoa mchango mkubwa kwa kushirikiana na Wazanzibari wenzao walio ndani kuijenga upya Zanzibar .

Tukijituma na kujitutumua itakiwavyo, Zanzibar inaweza kurudia nafasi yake ya kuwa kituo kikuu cha biashara na harakati za uchumi katika Afrika Mashariki na Bahari ya Hindi. Zanzibar ina nafasi ya kuwa kituo kikuu cha huduma katika eneo hili. Tunataka kuona Uwanja wa Ndege na Bandari ya Zanzibar zinakuwa tena mlango wa kuingilia na kutokea Afrika Mashariki. Tunataka na tunapaswa kuona ndege za mashirika ya kimataifa zikitua na kuruka kutokea Zanzibar na pia meli zikitia nanga na kung’oa kupitia Zanzibar . Tunaweza kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuja kuwekeza Zanzibar kwa kuanzisha viwanda ambavyo vitatoa ajira kwa vijana wetu na pia kusaidia kuifanya Zanzibar izalishe na kuuza nje bidhaa. Tukizitumia vyema fursa zilizopo Zanzibar itakuwa johari na siyo tena jeraha katika Afrika. Vijana wetu wasio na ajira watapata ajira zenye kipato cha kuwatosha wao na familia zao. Mababu zetu waliweza huko nyuma na sisi tunaweza tena ikiwa tutaikumbatia fursa ya maridhiano tuliyo nayo. Tusiruhusu kidudu mtu yeyote akaingia kati kuturudisha kule tulikotoka.


MARIDHIANO NA CHANGAMOTO ZAKE

Wakati tukizungumzia faida na fursa hizo, tuna pia changamoto kadhaa zinazoyakabili maridhiano haya. Miongoni mwa changamoto hizo ni pamoja na:

1. Matumaini makubwa yaliyojengwa na Wazanzibari bila ya kujali vyama vyao wakiamini kwamba hatua ya viongozi wawili wakuu wa kisiasa kukutana na kukubaliana kuzika tofauti zao itapelekea mabadiliko makubwa katika maisha yao na ujenzi wa mustakbali mpya wa nchi yao .

2. Viongozi wabinafsi kutoka pande zote mbili wanaojali maslahi yao zaidi kuliko maslahi ya nchi na watu wake ambao wameanza kufanya fitina zenye lengo la kuyavuruga mafanikio yaliyopatikana.

3. Muda mfupi uliopo kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu ujao ambapo Maridhiano yanapaswa yawe yamejengewa msingi wa kuhakikisha kuwa yanaimarika na kuendelezwa..

Binafsi nimekuwa nikitafakari sana changamoto hizi na naamini tunapaswa kuzitafakari na kuzijadili kwa lengo la kuona tunazikabili vipi. Ni maoni yangu kuwa tukifanya haraka ya kukimbilia uchaguzi ambao nilishaeleza hapo awali kwamba umekuwa ndiyo chanzo cha kuvurugika kwa umoja wetu, kuna hatari ya kuyapoteza yote niliyoyaeleza.. Hatuwezi kukwepa uchaguzi maana ndiyo njia ya kidemokrasia ya kuwapata viongozi wetu lakini tumeshafanya chaguzi saba za vyama vingi Zanzibar , nne kabla ya Mapinduzi na tatu tokea 1992, na zote zimeshindwa kutupa umoja. Kwa Zanzibar na katika kipindi hiki, maridhiano ni muhimu zaidi kuliko uchaguzi. Tutapaswa kwenda katika uchaguzi lakini naamini tutakuwa na uchaguzi mzuri zaidi baada ya kufanikiwa kujenga msingi madhubuti wa maridhiano.

Hatuwezi kukwepa ukweli kwamba wapo watu wanaokodolea macho fursa ya kutaka kuchukua madaraka ya juu ya Zanzibar , yaani nafasi ya Urais na ambao hawayapendi maridhiano. Miongoni mwao wako wanaotumia vyombo vya habari kukuza habari za kuleta chokochoko na kuzibana taarifa zenye mtazamo wa umoja. Wako pia waliotuma ujumbe kwenda Tanzania Bara kueneza uzushi kwamba lengo la maridhiano haya ni kuvunja Muungano. Watu wa aina hii hawawezi kuisaidia Zanzibar na kwa hakika ni maadui wa umoja wa Wazanzibari.

Kwa msingi huo basi, na baada ya kutafakari, mimi binafsi naungana na wale wanaotoa wito wa kuchukuliwa hatua ya kusogeza mbele kidogo uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mwaka huu kwa kipindi cha kati ya mwaka mmoja au miaka miwili ili kutoa nafasi kwa Rais Amani Karume kuchukua hatua zaidi za kukamilisha kazi njema aliyoianza. Naelewa mwenyewe juzi katika hotuba yake ya kilele cha sherehe za Mapinduzi amesema kwamba anakamilisha kipindi chake na Katiba ya Zanzibar hairuhusu kipindi cha tatu. Nakubaliana naye na sipendekezi kuondolewa kwa ukomo wa vipindi viwili kwa mtu anayeshikilia madaraka ya Urais wa Zanzibar . Ila namuomba sana akubaliane na matakwa ya Wazanzibari walio wengi kama yalivyokwisha oneshwa kupitia taarifa na kauli mbali mbali kwamba kipindi chake cha pili tukiongeze muda kidogo ili tusiipoteze fursa ya kihistoria ambayo ameianzisha yeye.

Natoa wito kwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wa pande zote mbili, Serikali na Upinzani, kulitafakari hili na kutupa Wazanzibari kile tunachokitaka. Kwa upande mwengine, nawaomba Wazanzibari tuungane pamoja kumtaka Rais Amani Karume aweke upande dhamira yake ambayo najua anaiamini sana ya kuondoka madarakani mwaka huu na badala yake akubaliane nasi juu ya haja ya kuendelea kuubeba mzigo huu tunaotaka kumtwisha na atuvushe pale ambapo waliomtangulia walishindwa kutuvusha.

Ahsanteni sana.


Source: Jamii Forums

No comments: