Monday, 22 March 2010

Siku ya Maji Duniani: Zanzibar na mfumo mpya wa huduma ya maji.


Siku ya Maji Duniani: Zanzibar na mfumo mpya wa huduma ya maji

Kwa miaka mingi tumekuwa tukishuhudia ama kushiriki katika miradi kadhaa inayoanzishwa kwa lengo la kusukuma mbele maendeleo ya huduma kwa wananchi.

Hata hivyo miradi mingi imekuwa ikifa kabla ya kukamilisha malengo yake yaliyokusudiwa. Hali hii ilifanya kuwepo na tafiti mbalimbali kujua ni kwa nini miradi hiyo imekufa huku mingine ikiwa imegharimiwa kwa gharama kubwa sana.

Tafiti mbalimbali zilionyesha kuwa miradi hufa kutokana na kutokuwepo na ushirikiano wa dhati kati ya wenye wazo la mradi na wale ambao watanufaika na mradi huo tokea mwanzo wa maandalizi ya mradi hadi ukamilishaji wake. Kutokuwepo kwa ushirikiano ama uhusishwaji wa jamii husika katika miradi hiyo kulielezwa kuchangia kufa ama kuzorota kwa miradi mingi.

Nimeshawahi kuzungumzia jinsi ya kuondokana na kadhia hii katika baadhi ya mabandiko yangu yaliyopita. Aidha kwa leo nitaendelea kuangalia hatua moja kubwa na muhimu iliyofikiwa katika kusimamia miradi inayoanzishwa. Hatua hii ni kwa wananchi kupewa uwezo wa moja kwa moja wa kutoa taarifa juu ya uendelevu wa mradi husika kwa asasi husika.

Mapema mwaka huu, Shirika la Umoja wa Kimataifa la Maakazi UN-HABITAT, Google, Zantel, ADB na ZAWA, walianzisha huduma ya kuwashirikisha wananchi kutoa taarifa kutokana na huduma ya maji wanayopata. Hii ni hatua moja muhimu sana katika kuona uendelevu wa huduma hiyo muhimu.

Leo hii wakati dunia nzima wakisherehekea siku ya maji, kuna vituo vipya hamsini vya maji vilivyojengwa katika maeneo ya shule, zahanati na sehemu nyingine muhimu za kijamii katika kisiwa cha Unguja, ambavyo vinasimamiwa na wananchi wenyewe. Wananchi wa maeneo hayo wananwajibika kutoa taarifa za upatikanaji wa maji, ubovu wa mabomba na matatizo mengine yoyote yanayoendana na huduma hiyo kwa kutumia njia ya simu.

Katika dunia hii ambayo kuna zaidi ya watu bilioni 2 ambao hadi sasa bado wanaendelea kusubiri kupata huduma ya maji, hii mimi ninaona ni hatua muhimu sana ya kuwawezesha wananchi kuona mradi huo kama ni sehemu ya maisha yao. Utoaji wa taarifa kwa huduma hiyo ni sawa na kukabidhi moja moja usimazi wa huduma hiyo kwa wananchi hao. Hii itawapa changamoto kubwa katika kuhifadhi na kuendeleva huduma hiyo. Zaidi hatua zingine zilizoanzishwa sambamba na mradi huu zinapaswa kufahamishwa kwa wananchi wa maeneo husika sambamba na kuwashirikisha ili kuwepo na uendelevu wa miradi hiyo.

Hapana shaka lengo lililokusudiwa la kuwezesha wananchi kulinda na kusimamia huduma hiyo litafanikiwa, kwa asasi husika kutekeleza taarifa wanazopokea juu ya uendelevu wa huduma hiyo.

No comments: