Friday 9 July 2010

Je Huu ni Mwisho wa Siasa za Makundi hapo Zenj?


Wapenda muafaka katika mstakabala wa siasa za visiwani, watakuwa wamefarijika sana kwa Dr. Shein kuongoza katika matokeo ya wagombeaji wa urais visiwani Zanzibar. Ingawa hakuwa wazi juu ya muafaka kama mgombea mwingine wa urais huo Ali Karume, kupita kwa jina la Dr. Shein kunafungua ukurasa mpya katika utawala visiwani humo.

Cha msingi hapa ni kujua ni kwa namna gani anaweza kulinda na kusimamia hatua za awali za kuondoa mpasuko wa kijamii visiwani humo. Sifa kubwa ya nje ya Dr. Shein ni kutojulikana msimamo wake, zaidi ni kuwa amehusu kisiwa cha pili, hivyo kuwepo na uwezekano mkubwa kuweza kusimamia maendeleo ya kuwepo na serikali ya mseto.

Tofauti na Dr. Bilal na Waziri Kiongozi, Dr Shein anaonekana kutokuwa na makundi yenye lengo la kuzoretesha jitihada muhimu zilizofikiwa hivi karibuni juu ya utaifa wa Zanzibar. Hii ni silaha yake kubwa na inabidi aitumie vizuri ili kuweza kutibu gonjwa la muda mrefu la siasa za visiwani hapo.

Kwa kuchaguliwa kwake kwa kura nyingi, kunaondoa dhana iliyojengeka miaka mingi juu ya utawala wa ngazi za juu huko Visiwani, ambao ulitokana na mtazamo wa rais wa kwanza wa serikali ya Mapinduzi. Kuchaguliwa kwa Dr. Shein kutaboresha mambo mengi ambayo yalikuwa yanaidhoofisha Zanzibar,na atafanikiwa tu iwapo ataweza kuendesha serikali bila kujali makundi.

Kwa upande mwingine Dr. Bilal amekumbwa na laana ya ubaguzi ambayo ilianza kumwandama mapema baada ya Dr. Salmin kumaliza muda wake wa uongozi. Ukimya wake wa kutoweka msimamo wake wa wazi juu ya siasa za chuki kisiwani hapo, ndio huo ambao umeendelea kumwondoa katika nafasi hiyo ambayo amejaribu kuigombania mara kadhaa bila mafanikio.

Waziri Kiongozi, kwa mtazamo wangu nae tayali alishaanza kujenga makundi katika safari yake ya kuelekea kuchukua urais visiwani humo. Misimamo yake katika masuala yenye kusumbua zaidi visiwa hivyo hakuweza kuyaweka bayana, hivyo kuashiria kusimamia baadhi ya makundi fulani. Ilikuwa ni njia nyepesi kwake kuweza kuchukua nafasi ya urais, kwani ameitumikia nafasi yake kwa miaka kumi hivyo kumwezesha kumrithi rais Karume.

No comments: