Friday, 23 July 2010

Umuhimu wa Kura ya NDIO hapo Julai 31, 2010


Sio siri tena kwamba siasa za umimi,chuki na utenganao hazina nafasi tena katika visiwa vya Zanzibar. Hii ni kutokana na muafaka wa kihistoria uliofikiwa na Rais anayemaliza muda wake hapo Zanzibar Mhe. A. Karume na Mhe. Maalim Seif, ambao kwa pamoja waliona uhumimu wa kuwa na Zanzibar moja yenye kuelewana licha ya tofauti za kisiasa.

Utengano wa Zanzibar na hasa kijografia umesababisha kuwepo kwa mikwaruzo mingi kwa watu wa visiwa hivyo licha ya baadhi yao kuwa na maingiliano ya kifamilia. Tatizo la utengano huu lilitokana na Mapinduzi ambapo upande mmjoa wa visiwa hivyo kujiona kuwa unahusika zaidi na mapinduzi hayo kuliko upande mwingine wa visiwa hivyo. Hivyo basi utaona kuwa utengano huu ulijengeka zaidi kisiasa.

Imechukua zaidi ya miaka arobaini na sita kwa wanzazibari kuona kuwa kuna umuhimu wa kuelewana na hasa katika uwanja wa kisiasa, ambao umecheza nafasi kubwa katika mgogoro na mtafuruku wa utengano visiwani humu. Awali rais wa kwanza alikuwa akitamka hadharani nafasi ya wananchi wa kisiwa kingine katika uongozi wa juu visiwani hapa. Kauli zake hizo ni baadhi ya mizizi ya utengano visiwani.

Machafuko ya hali ya hewa mwanzoni mwa miaka ya themanini hayawezi kuwekwa kando katika mtafaruku huu. Kwani yalionyesha wazi ni kwa kiasi gani baadhi ya wanavisiwa wanavyochukuliwa katika hatima ya uongozi wa juu visiwani humu. Hii iliongeza mbolea katika utengano na chuki miongoni mwa wanavisiwa.

Kurudi kwa mfumo wa vyama vingi, ndio ilikuwa kilele cha utengano. Kwani kwa mara ya kwanza Watanzania wengi waliweza kujua nini kinaendelea katika visiwa hivi. Kauli nyingi za ajabu ajabu zilisikika katika kuona kuwa utengano wa kisiasa, itikadi na hadi kifamilia unaendelea visiwani hapa, hadi kusababisha kupoteza maisha ya baadhi ya wanavisiwa ambao walikuwa wamechoshwa na kadhia hizo.

Leo hii sio vyema kutupa lawama kwa upande wowote uliohusika na kujenga migogoro hii. Kwani pande zote kwa namna moja ama nyingine zimehusika kikamilifu katika kujenga utengano huu.

Hii ndio inafanya kuwa kila mpandae maelewano visiwani humu aone umuhimu wa kupiga kura ya NDIO. Kura hii ina umuhimu mkubwa sana katika maendeleao ya kijamii visiwani humu na kufuta kabisa historia chafu ya utengano na migogoro isiyokwisha ya kisiasa.

Matokeo ya kura ya NDIO yatawezesha wanavisiwa wote kufungua ukurusa mpya katika maisha yao ya kila siku. Ukurasa ambao utaweka historia miongoni mwetu na ulimwenguni kwa ujumla.

Napenda kusema kuwa hii ni nafasi adhimu iliyotukuta wanavisiwa, ya kuweza kujiamulia wenyewe hatima ya maisha yetu kisiasa kiuchumi na kujamii. Kumbuka kuwa hapo awali maamuzi yote makubwa juu ya maisha yetu yalikuwa yakitoka juu, kabla la hili la tarehe 31/07/2010.

Ni vema kwa kila mwananchi mwenye sifa ya kupiga kura siku hiyo kupiga kura ya NDIO, ili kuweza kuwa na visiwa venye umoja na kuelekea kwenye kuunda serikali ya umoja wa kitaifa mara baada ya Uchaguzi Mkuu.

Tatizo letu tunalijua na tiba yetu ni kura ya NDIO.

No comments: