Thursday, 24 May 2012

Nipo Zanzibar

Nipo Zanzibar sasa kwa takribani mwezi mmoja... siku zinakwenda kasi pasipo mfano! Mara ya mwisho kuja Visiwani hapa ni zaidi ya miaka sita sasa. Mengi yametokea katika kipindi hicho, ikiwa ni pamoja na kumpoteza baba yangu mzazi, ndugu na marafiki wengi! Safari yangu ya kuja Zaznibar ilikuwa ya ghafla mno na ninawashukuru sana watanzania wa Finland kwa kuniwezesha kusafari kwa wakati na kuwahi maziko ya baba yangu.

Bado nina tongotongo machoni juu ya mabadiliko mengi niliyokwisha yaona mpaka sasa.. Zanzibar imebadilika sana na bado kuna kila dalili za mabadiliko zaidi kutokea katika kipindi cha miaka mitatu ijayo. Sio rahisi sana kwa mwenyeji kuona tofauti kwa haraka kama kwa mgeni. Wenyeji bado wana kiu kubwa ya maendeleo zaidi,ambapo ni jambo la msingi kwa maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Kuna mipangilio mingi mipya na plan kadhaa mpya baadhi ni kama kuondoa ofisi za serikali kadhaa ndani ya Mji Mkongwe, kuwepo na udhibiti mzuri wa aina ya magari yaingiayo Mji Mkongwe, upanuzi wa barabara(baadhi)katika maeneo ya Ng'ambo, ujenzi wa barabara mpya kuunganisha Ng'ambo na Mashambani.

Huduma nyingi zimekuwa na mafanikio ya kiasi na makubwa. Zantel bado ina tatizo la upatikanaji katika maeneo kadhaa visiwani hapa, ili ni la kushangaza kidogo! Lakini ndivyo lilivyo! Mabadiliko katika bandarini yamezidisha misongamano kwa abiria na vyombo vya moto.... Nimesikia hili linafanyiwa kazi, ingawa wahusika wanataka kwanza kuboresha upakuaji wa bidhaa toka melini. Kwani kwa sasa bandari ya Malindi ina uwezo wa meli moja tu kufunga gati! Mipango mipya ni kuwa na bandari yenye uwezo wa kuchukua meli nne kwa pamoja!

Mafanikio mengine yapo kwenye suala zima la usafi, ambapo sio rahisi tena kuona mifuko ya plastiki ikipepea angani, sasa kuna matumizi makubwa ya mifuko ya khaki na magazeti. Awali nilitegemea kuwepo na Vikapu vingi vya ukili, ikiwa ni kuongeza ajira na vipato kwa watengenezaji wa vikapu hivyo. Hata hivyo kutokana na uwekezaji mkubwa katika mahoteli malighafi ya vikapu hivyo imekuwa adimu na inauzwa kwa bei kubwa mno kwa mwananchi wa kawaida.

Kwa sasa kila barza ya kahawa hadithi ni muamsho, wengi wanapenda kuwepo kwa muamsho ili kujitenga na Tanganyika na wengi bado wanapenda kuwapo na muungano. Hii itatoa changamoto kubwa katika tume ya katiba. Muamsho zaidi ya kutaka kujitoa kwenye muungano, bado hawapo wazi katika sababu kubwa ama tatizo kubwa la muungano.

Nilipita hapo Airport na kuona ujenzi mpya wa Airport, hata hivyo unaonekana umesimama kwa muda mrefu, zipo tetesi kuwa Serikali serikali na wajenzi wamekuwa wakipisha juu ya ujenzi huo kiasi cha kufikia hatua hiyo.

Anyway nipo hapa Mesi ya Jeshi(Migombani) na tayali zantel imeanza kugomagoma... nitaendelea na stori katika siku zijazo....