Friday, 19 April 2013

Mwaka Mmoja wa Kumbukumbu ya Brigadier General Adam Clement Mwakanjuki


Umetimia mwaka mmoja sasa tokea Brigedia Jenerali Mwakanjuki kufariki dunia. Familia, ndugu, jamaa na marafiki wanaendelea kumkumbuka marehemu. Marehemu alizaliwa Oktoba 17, 1939 katika mtaa wa Kikwajuni, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar. Hadi kifo chake marehemu alikuwa ana umri wa miaka 73.

Brigedia Jenerali alipata elimu yake ya msingi katika skuli iliyokuwa ikijulikana kwa jina la St Paul - Kiungani katika mwaka 1947-1954.

Mwaka 1954-1959, Marehemu alipata fursa ya kujiunga na masomo ya sekondari katika skuli ya St Andrew ya Minaki jijini Dar es Salaam.

Mwaka 1960-1962, alijiunga na chuo kikuu cha Frizt Heckert Ujerumani ya Mashariki, na kupata fursa ya kusomea masomo ya juu ya siasa.

Baada ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar mwaka 1964, Marehemu Mwakanjuki alikuwa ni mmoja wa viongozi wa Umoja wa wafanyakazi wa Zanzibar.

Aidha, kuanzia mwaka 1964 hadi 1968 aliajiriwa na kufanya kazi katika idara ya Mambo ya Nje ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akishikilia wadhifa wa Afisa Mambo ya Nje.

JWTZ na JKT

Marehemu alijiunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ)tarehe 24 Juni, 1969 akiwa na wadhifa wa Mwalimu wa Siasa katika Jeshi la Kujenga Taifa(JKT).

Baadae Marehemu aliendelea na utumishi katika JWTZ katika nyadhifa mbalimbali kama ifuatavyo:-
-Mwaka 1972 - 1979: Alikuwa Mkuu wa Vikosi(CO)vya JWTZ, JKT na Mwenyekiti wa Tawi la CCM Jeshini.
-Mwaka 1980-1981: Kamisaa wa Divisheni ya 20 ya Jeshi(JWTZ)
-Mwaka 1982 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Siasa Makao Makuu ya Jeshi- Dar es Salaam.

Mafunzo Kazini
Marehemu Mwakanjuki alipata fursa mafunzo mbalimbali:
-Mwaka 1975: Mafunzo ya Afisa Mwanafunzi(Officer Cadets Course)katika chuo cha Mafunzo ya Maofisa - Mgulani Dar Es Salaam.
-Mwaka 1976: Mafunzo ya Ukamanda wa Kombania(Company Commanders Course) katika chuo cha Taifa cha Uongozi-Monduli, Tanzania.
-Mwaka 1977: Mafunzo ya Ukamanda wa Vikosi(Battalion Commanders Course) katika chuo cha Taifa cha Uongozi- Monduli, Tanzania.

Marehemu Mwakanjuki alifanikiwa kupandishwa vyeo Jeshini katika ngazi tofauti kama ifuatavyo:-
-01.07.1975: Cheo cha Meja.
-05.05.1977: Cheo cha Luteni Kanali(lieutenant Colonel)
-25.02.1980: Cheo cha Kanali(Full Colonel)
-10.04.1988: Cheo cha Brigadia Jenerali(Brigadier General), cheo alichoendelea kuwa nacho hadi alipostaafu jeshi mwezi Juni, tarehe 30 mwaka 1994.

Medali
Medali alizowahi kutunukiwa katika uhai wake ni pamoja na ujasiri wake akiwa kazini, Marehemu alipata heshima zingine zikiwemo:-
-Medali ya Uhuru.
-Medali ya Muungano
-Medali ya Vita.
-Medali ya Kagera.
-Medali ya Miaka 20 ya JWTZ.
-Medali ya Utumishi Mrefu Tanzania.
-Medali ya Utumishi Uliotukuka Tanzania.

Siasa
Katika siasa Brig Jenerali Mstaafu Mwakanjuki, alijiunga na Chama cha Afro-Shiraz(ASP)mwaka 1958, akiwa mwananfunzi wa skuli ya sekondariya Minaki. Aidha, katika mwaka 1958-1959, alikuwa kiongozi wa Chama cha Wanafunzi wa Kiafrika wa Zanzibar.

Kutokana na hekima, busara na uwezo mkubwa aliouonesha katika masuala ya siasa, ASP ilimuamini na kumkabidhi nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya chama hicho.

Aidha, Uongozi wa Chama ulimteua ili akiwakilishe Chama katika shughuli muhimu mbalimbali zilizofanyika ndani na nje ya nchi yetu, miongoni mwake, mwaka 1962 alishiriki katika Mkutano Mkuu wa Kwanza wa kupitisha Muundo wa Katiba ya ASP.

Mwaka 1963, alishiriki katika mkutano wa Afro-Asian(The Afro- Asian Solidarity Conference)uliofanyika Moshi, Tanzania.

Mwaka 1961-1964 alikuwa akitumikia katika shughuli za Chama cha Wafanyakazi katika kazi mbalimbali za chama kama vile matayalisho ya Uchaguzi, Uenezi wa Siasa, Kuhudhuria mikutano ya kisiasa inayofanyika ndani na nje ya Taifa letu, pamoja na kushiriki kikamilifu katika harakati za Mapinduzi ya Zanzibar ya 12.01.1964.

Baada ya kuungana kwa Vyama vya TANU na ASP mwaka 1977, Marehemu alijiunga na Chama cha Mapinduzi kupitia tawi la Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa(MMJKT)liliopo mkoani Dar es Salaam, mnamo tarehe 01.04.1977.

Mwaka 1982 alichaguliwa kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kwa tiketi ya Jeshi baadae mwaka 1983 aliteuliwa kuwa Katibu wa Mkoa wa Ruvuma kabla ya kuhamishiwa Mkoa wa Singida Mwaka 1987- 1990. Marehemu aliendelea kuwa mjumbe wa Halmshauri Kuu ya Taifa hadi alipofariki dunia mwaka 2012.

Uongozi Serikalini
Brigedia Jenerali Mstaafu Mwakanjuki alishika nyadhifa mbali mbali za Uongozi katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

-1990-1992: Waziri asiye na Wizara Maalumu.

-1992-1995: Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais Tawala za Mikoa na Vikosi vya SMZ.

-1995-2000: Waziri wa Kilimo na Mifugo.

-2001-2004: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Katiba na Utawala Bora.

-2004-2010: Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi.


Imeandaliwa na Mwantanga Ame - Zanzibar Leo. 2012

Imeeditiwa na Che Guevara Mwakanjuki.
2 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Kumbukumbu nzuri...astarehe kwa amani

Anonymous said...

Na watoto kaacha wangapi?