Thursday 13 February 2014

Makaburi ya Wakristo Mwanakwerekwe Yapo Hatarini Kutoweka....



Kumekuwepo na hujuma za makusudi za kuharibu eneo rasmi la makaburi ya kuzikia Wakristo wa Zanzibar, liliopo Mwanakwerekwe katika Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini/Magharibi.

Ni muda mrefu sasa kumekuwepo na vitendo vya ovyo kabisa vinavyofanyika katika eneo la makaburi hayo. Vitendo hivyo sio rahisi kuviona vikifanyika katika maeneo ya makaburi ya dini zingine ambazo makaburi yao yamepakana na haya ya Wakristo.

Kama inavyoonekana kwenye picha hapo juu, kuna hujuma za kulifanya eneo hilo kama Jaa la taka, kuna watu kwa makusudi kabisa wameligeuza eneo hilo kama sehemu ya kucimbia mchanga kwa ajili ya ujenzi wa nyumba zao.

Aidha vijana na watoto wanaoishi karibu na makaburi hayo, wao wameona eneo hilo linafaa zaidi kwa kuchezea mpira, huku waakazi wengine waishio karibu wameligeuza eneo hilo kuwa barabara ya kupitishia vipando vyao juu ya makaburi, huu ni utaarabu wa pekee ambao unaweza kuonekana Zanzibar pekee hapa duniani.

Kama vile haitoshi, wapo waliogeuza makaburi hayo kama sehemu ya kupata materials kwa shughuli zao za ujenzi, ambapo ubomoa zege katika misalaba na mifuniko ya makaburi ili kupata nondo, kumegua vigae (tiles) au kuchomoa misalaba ya mbao. Zaidi sio ajabu kukutana na mifugo ikuchungwa makaburini hapo.

Wakati huu udhalilishaji wa maeneo ya makaburi ya Wakristo ukizidi kuota mizizi na kuonekana kama ni jambo la kawaida serikali imeendelea kukaa kimya tofauti na hatua wanazochukua kwa makaburi ya Waislamu.

Mwishoni mwa mwezi wa kwanza, kupitia kwenye Baraza la Wawakilishi, serikali ilisema kuwa imepanga kulitumia eneo la Kama liliopo Wilaya ya Magharibi kwa ajili ya kuzikia watu.

Mpango huo unachukuliwa kutokana na eneo la makaburi ya Waislamu yaliyopo Mwanakwerekwe kuelekea kujaa. Hata hivyo Wawakilishi hawakuwa tayali kuzungumzia udhalilishwaji na hujuma zinazofanyika katika eneo la makaburi ya Wakristo ambalo lipo jirani tu na hayo yalioadiliwa.

Upofu na ukiziwi wa serikali juu ya yale yanayoendela katika makaburi hayo, ni moja ya sababu kubwa inayowatia kiburi baadhi ya watu ambao wameamua kuyahujumu makaburi hayo ya Wakristo.

Ni vema kwa serikali kutokimbilia kutafuta maeneo mapya kabla ya kudhibiti maeneo yanayo endelea kutumika. Kwani kwa kufanya hivyo bado hawatokuwa wametatua tatizo lilipo kwenye jamii.

Ikumbukwe kuwa hatua ya kutafuta eneo jipya la Kama, imetokana na kumwegwa na kubadilishwa kwa matumizi ya eneo la makaburi ya Waislamu, ambalo awali lilikuwa na ukubwa wa hekta 80 za mraba na sasa linakaribia kuwa na hekta 25 za mraba.

Kwa upande wa Wakristo wa Unguja mjini, ipo haja ya kuendelea na wazo lililotolewa na waumini wenzetu juu ya kulizungushia ukuta eneo hilo. Viongozi wa madhehebu yote yanayotumia eneo hilo itakuwa ni jambo la msingi iwapo mtakutana na kupanga namna ya kuweza kujenga uzio ili kuifadhi makaburi hayo na eneo lililobaki.

Ni jukumu letu kwa kiasi fulani kulilinda eneo hilo pasipo kutegemea sana serikali. Hii itasaidia kulitunza eneo hilo kwa muda mrefu. Tunaweza kuangalia na kuiga mfano wa Makaburi ya Wajerumani ya pale Mwembemadema, ambayo yamedumu kwa zaidi ya miaka 150, na tunaweza vilevile kuangalia jinsi makaburi yanavyoweza kuvamiwa kama ilivotokea kwa makaburi ya Wakatoliki hapo hapo Mwembemadema, ambapo baadhi ya watu walianza kuzika kabla ya kutiwa uzio.

Kisheria, maeneo ya makaburi yamekuwa na utata mwingi. Hakuna sheria rasmi juu ya udhibiti na utunzaji wa maeneo ya makaburi, zaidi ya ile iliyotungwa baada ya Mapinduzi ikitoa uhuru wa kubadili matumizi ya makaburi baada ya kupita miaka 40. Mfano wa karibu juu ya sheria hii ni pale ilipotumika katika makaburi ya kariakoo.

No comments: