Saturday, 15 February 2014

Maoni ya Mzanzibari kwa Wajumbe wa Zanzibar Kwenye Bunge la Katiba

Enyi Waheshimiwa Wabunge,

Kama tunavyojua kuwa Bunge la Katiba linakaribia kuanza na nyinyi ndio munaokwenda kupeperusha bendera ya Zanzibar kwenye bunge hilo linalobeba mustakabali wa taifa hili kwa miaka mingi ijayo. Wito wangu wa kwanza kwenu ni kwamba muende mukaangalie maslahi ya nchi badala ya vyama vya siasa. Najua wito huu mumeshatolewa na wengi, na nyinyi wenyewe huwa kila mukipata nafasi munatwambia kuwa hivyo ndivyo munavyokwenda kufanya. Lakini mimi nikiwa Mzanzibari, nina wajibu pia wa kuwakumbusha tena na tena.

Ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambao pia utatumika kama ukumbi wa Bunge la Katiba.
Ukumbi wa Bunge la Jamhuri ya Muungano ambao pia utatumika kama ukumbi wa Bunge la Katiba.

Jukumu lenu kubwa ni kuangalia namna madhubuti ya kutatua mfumo butu wa serikali mbili usio na mbele wala nyuma. Kwenye katiba hii, nyinyi hamuna kubwa zaidi ya hilo, maana mengine yaliyo nje ya hapo yameshaelezwa kwenye Katiba yenu ya Zanzibar.

Nendeni bungeni mukikumbuka kwamba si haki kwa Wazanzibari kuwazuilia Watanganyika kurejesha nchi yao itakayoongozwa na wao wenyewe kupitia bunge lao wenyewe, bajeti zao wenyewe na ukusanyaji wa mapato yanayotokana na jasho lao wenyewe.

Kumbukeni kuwa mfumo wa Serikali Mbili ndio umegeuka kuwa fitna baina ya jamii mbili zenye uhusiano mkubwa wa kidugu na uliodumishwa kwa misingi ya ufahamiano na heshima na sio utawala wenye malengo tafauti na azma nzima ya kuungana

Iangalieni Katiba ya Zanzibar kila mara mukiwa kwenye vikao vya bunge hilo. Ilindeni na muiheshimu. Musije mukaruhusu kuharibiwa kwa misingi ya Katiba hiyo.

Mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010 yameonyesha wazi kwamba Zanzibar ni nchi inayoongozwa kwa misingi ya mihimili ya serikali, bunge na vyombo vya sharia. Wakati Wazanzibari tulipoipitisha, hatukutaka kuweka kimeme katika hadhi ya Zanzibar kama nchi katika Muungano na tukaweka wazi madaraka hata ya kuigawa nchi kwa mhusika mkuu wa Serikali ya Zanzibar badala ya mfumo wa zamani wa kuomba ruhusa kwa mlango wa pili, kutoka kwa Rais wa Muungano.

Nyinyi hamuna uwezo wa kuiviza azma kama hii iliyomo kwenye Katiba yetu na ambayo iliidhinishwa na asilimia zaidi ya 60 ya wananchi. Nyinyi hamuwezi mukawa wa mwanzo kuuzuia upande wa pili kujichomoza kwa visingizo vya kuulinda Muungano. Muungano ulikuwepo na utakuwepo, pawe au pasiwe na katiba mpya, kwani misingi ya Muungano huu ni udugu na mafahamiano makubwa baina yetu, watu wa Tanganyika na watu wa Zanzibar.

Nendeni mukapinge hoja za matumizi makubwa katika Mfumo wa Serikali Tatu kwani ni dhaifu. Chukuweni data za mapato zilizokusanywa kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bodi ya Mapato ya Zanzibar (ZRB) na hata tafiti nyingi kutoka taasisi za ndani na nje ambazo zinaonyesha wazi mgawanyo wa mapato ya Muungano na nchi husika na hata uchangiaji wake katika shirikisho kuendana na hali halisi ya wakaazi na maeneo yao. Waulizeni wanaopinga Serikali Tatu, hivi mambo matano ya Muungano yatakuwaje ghali kuliko 32 ya sasa yenye kero lukuki?

Vunjeni hoja za kwamba wapenda Serikali Tatu ni wapenda madaraka, maana nayo pia ni potofu. Semeni kwamba Bunge la Shirikisho linalopendekezwa kwenye Rasimu ya Pili ya litakuwa na wajumbe 20 tu kutoka Zanzibar. Sasa hayo madaraka yanayopendwa na wapenda mabadiliko yako wapi, wakati leo hii Zanzibar ina takribani wabunge 100 kwenye Bunge la Muungano? Maana ubunge ni cheo na cheo ni madaraka kwa kuwa kwake na fursa za mwenye madaraka. Sasa je unapopunguza wajumbe, ni kupenda madaraka au kupunguza madaraka?

Huenda mukaambiwa kuwa hoja ni kwamba Bara nao watahitaji wabunge wao wa serikali yao. Ulizeni cha ajabu hapo ni kipi? Mbona hatujasikia kelele za kuwa Baraza la Wawakilishi, kwamba nalo pia lina gharama kwa Wazanzibari na Serikali ya Zanzibar? Wazanzibari wanalipa kodi kuigharamikia serikali, mahakama na baraza lao la wawakilishi. Waacheni ndugu zetu wa Tanganyika nao walipe kodi kwa ajili ya taasisi zao za utawala.

Urahisi wa mbili kwa tatu labda ni kwa mantiki ya hisabati tu, maana ni kweli mbili ni ndogo kuliko tatu katika mfumo wa mfuatano. Lakini kwenye suala la gharama, wasiwajie na maelezo ya mantiki ya hisabati bila ya ushahidi, kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wanawatumieni nyinyi kuhahalisha uoza wa miaka 50, huku tukiendelea kujidanganya eti kunahitajika marekebisho madogo madogo.

Wakumbusheni historia ikiwa wameisahau. Kwamba marais waliotangulia kwa Zanzibar ni sita na kwa Muungano ni wanne. Hivi tuseme marais hao hawakuwa na hamu ya kweli ya utatuzi kwa miaka 50 hata ikawa kila mmoja anamrithisha mwenziwe kero bila ya utatuzi? Kimewashinda nini kwa muda wote huo, hata hii leo iwe rahisi kutatua hizo kero? Kwani serikali si ndio hii hii ya chama tawala, CCM?

Waonesheni ukweli ulio mbele ya macho yao lakini wasiouona. Kwamba hata ndani ya vyama vya siasa, ambavyo kikatiba ni vya Muungano, mfumo ni huu huu wa Tatu: vyama vina mwenyekiti mmoja na makamo wawili wa pande mbili, manaibu katibu wa pande. Kwa nini isiwe kwa mjengeko wa serikali?

Niwaambieni kitu kimoja, waheshimiwa wabunge wangu. Hizi kelele na khofu za gharama zinalengwa zaidi kwamba kutakuwa na rais wa pande mbili na rais wa shirikisho. Lakini wanapaswa kujua hao kuwa unapopenda boga, upende na uwa lake. Ikiwa wameutaka Muungano, wasikhofie gharama. Sisi Zanzibar, tuna wakuu wa serikali wanaotazamwa na serikali yenyewe. Sasa kwa nini iwe gharama kwa wakuu wa serikali ya Tanganyika kutazamwa na serikali yao wenyewe? Kwa nini wasiwaweke wakuu hao kuwa wachache tu wanaostahili kutokana na mamlaka na kazi zao kutazamwa na serikali ya shirikisho yenye mchango wa pande zote?

Wanaosema Zanzibar hatuwezi kuchangia Serikali Tatu, wambieni wawapeni hoja sio maneno matupu. Watumbatu hunasema “Mkono mtupu haulambwa.“ Musije mukatishwa na watu waliojivalisha majokho ya udaktari na uprofesa wa kila fani, wakawafanya kuwa mazuzu musioweza kuhoji.

Mukitaka kujuwa kuwa hao hawana hoja, angalieni upofu wa hoja yao ya mchango wa Zanzibar kwenye Muungano isivyoweza hata kuchanganuwa kwamba watu milioni 1.5 na milioni 44 ni tafauti. Kwamba uchangiaji wa Wazanzibari milioni 1.5 utakwendana na mambo matatu muhimu – idadi ya watu wetu, ukubwa wa maeneo na matumizi yetu katika taasisi husika.

Uchangiaji wa bajeti ya trilioni 400 usikutisheni. Munalotakiwa mufikiri kwanza ni kwamba kuna mantiki gani ya kupewa mapato ya 4.5% kutoka mgawo wa Muungano hata tushindwe kuchangia kwa mantiki ya namna hiyo hiyo? Waje na uthibitisho sio ngonjera zisizokwisha, maana sisi Wazanzibari tumeshachoka na kero za kujitakia. Tumechoshwa na chuki na fitna za kupandikizwa na mfumo butu wa sasa.

Wengine watawaambieni kuwa hoja ni kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere. Waambieni basi ni bora wote warudi kwenye Vijiji vya Ujamaa na Azimio la Arusha. Waambieni warudi kwenye mfumo wa chama kimoja aliouunda. Waambieni Mwalimu Nyerere angelitunzwa zaidi kama kungeundwa serikali moja tu kwa vile ndio hasa ndoto yake na kauli mbiu yake ya “Mbili kwenda Moja”.

Watakeni wawapeni sababu za msingi za kuendelea na mfumo wa sasa, kwani sisi Wazanzibari wa wa kizazi cha leo ni watu wa kuhoji. Sisi sio wa mbembelezo wa asili za wazee wetu ikawa ndio sababu ya kukubali makosa tukayawacha yaendelee.

Pelekeni ujumbe wetu wa wazi kwenye Bunge la Katiba. Kwamba sisi Wazanzibari tumewatuma mukapitishe mfumo wa Serikali Tatu kama ulivyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba. Hapana shaka, mutatakiwa kuufanyia marekebisho hapa na pale kidogo, lakini kwa vyovyote hamutarudi hapa na mfumo huu wa serikali mbili ambao una kila chembechembe za watu wachache, wabinafsi, wanaofaidika nao.

Si tumeona wakati Baraza la Wawakilishi likizuia na kupinga ongezeko kubwa la mafao na mishara yao, Bunge la Muungano lilikubali ongezeko kubwa la mafao kwa wanaomaliza mihula yao? Hizi ndizo gharama tunazosema hatutaweza kuzibeba.

La mwisho kabisa, ninawanasihi kwamba nendeni mukidumisha heshima ya Zanzibar, Uzanzibari na Wazanzibari. Musije mukarogwa na mukarogeka na kirusi cha ufisadi kinachoimun’unya Tanganyika hivi sasa. Kwa mfano, kwa lipi kubwa munalokwenda hata kila mmoja kati yenu akalipwe posho ya shilingi 700,000 kwa siku? Laki saba hizo zinaweza kutumika kuwanunua na kuiuza tena Zanzibar kama ambavyo imekuwa ikichuuzwa siku nenda siku rudi.

Hapana. Nyinyi musije mukawa wachuuzi wa Zanzibar. Umma utawaona, utawalaumu. Utawahukumu.

Wakatabahu,

Farrel Foum Jr.

No comments: