Sunday 9 February 2014

Matokeo ya Uchaguzi Kiembesamaki: CUF Watafute Sababu Nyingine Mpya.



Kama ilivyo ada kila baada ya uchaguzi, vyama vishiriki vimekuwa vikitoa maoni yao juu ya mwenendo mzima wa uchaguzi kuanzia wakati wa kampeni hadi upigaji kura. Maoni ya vyama vya siasa hivyo ni juu ya ushiriki wao na namna uchaguzi ulivyokwenda halikadhalika kujipima kufanikiwa kwao ama kutofanikiwa kwao katika chaguzi husika.

Mapema mwezi huu kulifanyika uchaguzi mdogo wa kuchagua mwakilishi mpya katika Jimbo la Kiembesamaki huko Unguja, ambapo chama cha CCM kilishinda uchaguzi huo kwa kupata asilimia 76 na mgombea wake Bw. Mahmuod Thabit Kombo kutangazwa mshindi.

Chama cha CUF ambacho ndio chama kikubwa cha upinzani visiwani humo kiliambulia asilimia 18, ikiwa ni asilimia ndogo sana kulinganisha na umaarufu wake na kukubaliwa kwake visiwani humo. Hii inatoa picha mbaya kwa wafuasi wa chama hicho na inatia kichefuchefu kwa uongozi wa chama hicho. Ikumbukwe kuwa chama hicho baada ya kutoridhisha na matokea mengi ya uchaguzi visiwani humo ilifikia hatua ya kutoitambua serikali na kususia shughuli zote za kiserikali ikiwa ni pamoja na ushiriki katika Baraza la Wawakilishi.

Kwa kifupi kila mtu anajua miafaka iliyokuwa ikiundwa kila baada ya chaguzi kutokana na chama cha CUF, kupinga matokeo ya uchaguzi. Hatima ya miafaka hii ilipelekea kuanzishwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa baada ya maafikiano na chama cha CCM.

Moja ya sababu kubwa ambayo imekuwa ikisikika tokea kurudi kwa mfumo wa vyama vingi nchini, ni ile ya uchaguzi kutokuwa huru na wa haki pamoja na kuporwa kwa demokrasia visiwani humo na chama cha CCM, zaidi lawama kwa Tume ya Uchaguzi. Sababu hizi zimekuwa zikirudiwa rudiwa kila baada ya uchaguzi na hasa katika matokeo ambayo chama cha CUF ikishindwa. Pale wanaposhinda hamna sababu hizi.

Baada ya maridhiano na kuja kwa serikali ya umoja wa kitaifa, wengi wetu tulitegemea kutosikia tena sababu hizi kutoka katika chama hicho, kwani sasa nao ni waundaji wa serikali ambayo hapo awali walikuwa wakiilalamikia. Kitendo cha katibu mkuu wa CUF Bw. Maalim Seif Hamad na Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Bw. Salim Bimani kuibuka kupinga matokeo ya uchaguzi mdogo wa Kiembesamaki kwa kauli zilezile za miaka nenda rudi kinatia shaka na kinatoa maswali mengi miongoni mwetu.

Akiwa huko Pemba Bw. Seif Sharif Hamad, amerudia kauli zake za kudai kuwa uchaguzi haukuwa huru na serikali hiyo hiyo anayoifanyia kazi imehujumu uchaguzi huo kwa kupandikiza mamluki wakati wa upigaji wa kura.

Alisema "Kama kuna wananchi wa Kiembesamaki waliokwenda kupiga kura basi hawazidi elfu moja, wengi walichukuliwa katika maeneo tafauti, kama vile Makunduchi, Mtende, Kitope na Bumbwini na wakapelekwa kupiga kura huku wakilindwa na vikosi vya serikali".

Nae Bw. Bimani alisema "Chama cha CUF kilibaini tokea mapema maandalizi ya fujo na matumizi mabaya ya nguvu za dola pamoa na vikosi vya serikali, ambavyo viliandaliwa kwa dhamira ya makusudi ya kuwapa haki waisostahiki na pia kuwanyima watu wengi haki yao ya kufanya maamuzi ya demokrasia".

Kauli hizi toka kwa viongozi hawa zinatia shaka juu ya ukweli wa malalamiko ya chama hiki kabla na baada ya kuja kwa serikali ya umoja wa kitaifa. Ni kauli ambazo zimeshazoeleka sana katika masikio ya wananchi wengi visiwani humo na nchini Tanzania kwa ujumla. Sina budi kujiuliza ni nini mafanikio ya CUF kuwepo katika serikali ilhali bado wanaendelea kuilalamikia serikali hiyo hiyo. Ni nini faida iliyopatikana kwa kuwepo na maridhiano iwapo kero ya ulalamishi wa hujuma katika chaguzi ipo pale pale?

Kwa upande mwingine nashindwa kuelewa kama viongozi hao wameshindwa kuona impact iliyotokea baada ya kuja kwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa wanachama na wapenzi na wapiga kura wao. Je bado wanachama wao wanaona kuna umuhimu wa kushiriki katika chaguzi ambapo matokeo yake hayatoweza kubadili nafasi ya chama hicho katika kuendesha serikali? Ni kwa kiwango gani chama hiki kina maamuzi katika kuendesha serikali ya maridhiano?

Ukiangalia vyama vingine ambavyo havipo kwenye serikali ya umoja wa kitaifa kama vile TADEA, ADS, SAU na kadhalika, wao wameyapokea matokeo haya kwa mikono miwili na zaidi wameendelea kuangalia kama kumekuwepo na mafanikio katika kushii na kukubaliwa na wananchi kupitia matokeo hayo. Zaidi wameonyesha kutokuwepo na hujuma yoyote wakati wote wa uchaguzi huo tofauti na madai yaliyozoeleka ya CUF.

Bw. Ali Mohamed Ali Mwenyekiti wa TADEA amekiri kutokuwepo kwa mamluki waliopata kupia kura katika vituo vyote vya uchaguzi huo, aidha waliopiga kura ni wananchi wa Kiembesamaki. Nini nafasi ya kauli ya Bw. Hamad hapa? TADEA ni mojawapo ya vyama vilivyoshiriki chaguzi zote visiwani humo tokea kuja kwa mfumo wa vyama vingi.

Ni vema kwa wakati huu chama cha CUF, kikajiangalia upya juu ya ushawishi wake kwa wanachama wake na nafasi yake kama chama kikubwa cha upinzani visiwani humo badala ya kuja na kauli rahisi rahisi kama hizi. Muda wa kufanya hivyo wanao na ni mwingi. Zaidi wapime nafasi yao serikalini na hatima ya chama chao.

No comments: