Friday, 25 September 2015

Mch. Mtikila na Maoni Yake Juu ya Tafiti zilizofanywa na Twaweza na Synovate...

MIJADALA - SEPT.25.2015 | STAR TV

Mwenyekiti wa DP azungumzia tafiti zilizofanywa na SYNOVATE pamoja na TWAWEZA juu ya nani ana nafasi ya kushinda uraisi katika uchaguzi mkuu.

Posted by Simu.TV on Friday, 25 September 2015

Saturday, 19 September 2015

Dr. Ali Mohamed Shein...

Umoja ni Ushindi...

ILANI YA CCM KWA AJILI YA UCHAGUZI MKUU WA MWAKA 2015 - UTANGULIZIUtangulizi

1. Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 wa kuwachagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais wa Zanzibar, Wabunge, Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na Madiwani imeandaliwa ikiwa ni mkataba kati ya CCM na wananchi. Ilani hii imeandikwa kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2025 na Mwelekeo wa Sera za CCM zenye lengo na nia ya kuendelea kuwatumikia wananchi kwa kipindi cha miaka mitano ijayo (2015-2020).

2. Ilani hii ni tamko maalumu kwa wapiga kura kuhusu nia ya CCM ya kuendelea kushika dola na kuwaongoza Watanzania kwa njia ya kidemokrasia, na hasa kuendelea kudumisha amani, umoja wa Kitaifa, usawa, ustawi wa wananchi, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

3. Nia na uwezo wa CCM wa kuendelea kuongoza Taifa hili unajidhihirisha katika uzoefu ambao tumeupata kwa miaka 38 tangu kuanzishwa kwake na kuwa madarakani, ambapo katika kipindi chote hiki kimeiwezesha nchi yetu kupata mafanikio makubwa katika nyanja za kiuchumi, kisiasa na kijamii.

4. Katika miaka mitano ijayo (2015-2020), CCM ikiwa madarakani, itazielekeza Serikali zake kutumia nguvu zake zote kuendelea kupambana na changamoto kubwa nne:-
Kwanza kuondoa umaskini; pili kupunguza tatizo la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana; tatu kuendeleza vita dhidi ya adui rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma; na nne kuendelea kudumisha amani, ulinzi na usalama wa maisha ya wananchi na
mali zao.

Kupambana na Umasikini
5. Pamoja na mafanikio ya kukua kwa uchumi na ongezeko la huduma za kijamii yaliyopatikana katika kipindi hiki, bado ipo changamoto kubwa ya umasikini wa kipato na usio wa kipato. Takwimu zinaonesha kwamba asilimia 28.2 ya Watanzania ni masikini. Wengi wa wananchi hao wanaishi vijijini (asilimia 75) na wanategemea kilimo katika maisha yao. Wapo pia wananchi masikini wanaoishi mijini ambao wanaendesha maisha yao kupitia shughuli za biashara ndogo ndogo zisizo rasmi.

6. Katika kupambana na changamoto hii, CCM itazielekeza Serikali zake kuboresha
maisha ya wananchi wote na hususan wa vijijini, kwa kuchukua hatua zifuatazo:-
(a) Kuhamasisha kilimo kupitia kauli mbiu ya Kilimo Kwanza kwa kuwawezesha wakulima kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa, pembejeo, zana za kisasa na wataalamu wa ugani pamoja na mbinu za kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao;
(b) Kuongeza kasi ya kupima ardhi yao na kuwapatia hati miliki za kimila ambazo watazitumia kama dhamana ya kuwawezesha kupata mikopo ya kuendeleza shughuli zao za kilimo, ufugaji na uvuvi;
(c) Kuendeleza juhudi za kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo elimu, afya, maji, umeme na ujenzi wa nyumba bora; na
(d) Kuongeza kasi ya kurasimisha biashara na kuwapatia wafanyabiashara wadogo maeneo ya kufanyia biashara, leseni na fursa za kupata mikopo yenye masharti
nafuu.

7. Mafanikio ya utekelezaji wa masuala haya yote kwa pamoja yanatarajiwa kuleta mabadiliko makubwa ya kimaendeleo mijini na vijinini, na hivyo kupunguza kwa kiwango kikubwa hali ya umasikini nchini.

Ajira kwa Vijana

8. Suala la ukosefu wa ajira kwa vijana ni moja ya changamoto zinazolikabili Taifa letu na dunia yote kwa ujumla. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita yapo mafanikio yaliyopatikana katika kuongeza ajira. Hata hivyo, mafanikio katika upanuzi wa elimu ya Sekondari na Vyuo yameongeza mahitaji ya ajira ya vijana wasomi kila mwaka ikilinganishwa na nafasi zinazokuwepo.

9. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo jitihada za kulipatia ufumbuzi tatizo la ajira nchini zitaendelezwa. Kipaumbele kitakuwa katika kukuza na kuanzisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vilivyo na uwezo wa kuajiri watu wengi na vyenye kuzalisha bidhaa zinazotumiwa na watu wengi wa ndani ya nchi na zile za kuuza nchi za nje. Aidha, kwa upande wa Tanzania Zanzibar, mikakati ya kuongeza ajira kwa vijana itazingatia mazingira maalamu ya fursa za uchumi wa visiwa.

10. Katika kipindi cha 2015-2020, sekta za uzalishaji mali kama kilimo, ufugaji, uvuvi, viwanda vikubwa na vidogo na huduma za kiuchumi kama vile miundombinu ya nishati, uchukuzi na ujenzi zitaelekeza mipango yao katika kupunguza umasikini na kuanzisha ajira hususan kwa vijana. Aidha, huduma za jamii za elimu, afya na maji
zitajielekeza kusaidia kuondoa umasikini na kuongeza ajira.

Vita dhidi ya Rushwa

11. Jitihada za kuinua uchumi na kuongeza huduma za jamii hazitaleta manufaa kwa wananchi na kuondoa umasikini iwapo adui rushwa ataendelea kulitafuna Taifa letu.
Rushwa ni adui wa haki pia ni adui wa maendeleo na ustawi wa wananchi, hivyo ni moja ya changamoto kubwa inayoikabili nchi yetu na dunia kwa ujumla.
12. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, CCM itazielekeza Serikali zake kuendeleza mapambano dhidi ya adui rushwa kwa nguvu zake zote na kuendelea kuziba mianya ya rushwa katika taasisi za umma; kuchukua hatua kali na za haraka kwa wale wote watakaobainika kuendeleza rushwa Serikalini na katika sekta binafsi; na kuimarisha
vyombo na taasisi zinazohusika na kuzuia na kupambana na rushwa; ikiwa ni pamoja na kuanzisha Mahakama Maalumu kwa ajili ya makosa ya rushwa na uhujumu uchumi.

13. Sambamba na kupambana na tatizo la rushwa, Serikali pia zitatakiwa kushughulikia kwa ukali zaidi tatizo la ubadhirifu na wizi wa mali ya umma, matumizi mabaya ya madaraka, ukiukwaji wa maadili ya uongozi na utumishi wa umma, kuchelewesha kutoa maamuzi yenye maslahi kwa umma na kusimamia uwajibikaji katika kutekeleza masuala yenye maslahi kwa umma.

Ulinzi na Usalama

14. Nchi yetu imepata mafanikio makubwa ya kuwa na amani na utulivu tangu tupate uhuru mwaka 1961 na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964. Imekuwa kimbilio la watu wa Mataifa ya jirani kila wapatapo matatizo ya uvunjifu wa amani katika nchi zao. Hata hivyo, siku za karibuni vimeanza kuonekana viashiria vinavyoleta hofu ya usalama wa wananchi, hasa vitendo vya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino), kuuawa kwa vikongwe, ukatili dhidi ya wanawake na watoto na tishio la vitendo vyenye mwelekeo wa kigaidi.

15. Katika kipindi cha miaka mitano ijayo, CCM itazielekeza Serikali zake kuendelea kuimarisha vyombo vyote vya ulinzi na usalama kwa kuviongezea raslimali fedha, raslimali watu, maslahi, zana za kisasa na mafunzo. Aidha, elimu kwa umma itatolewa ili kukomesha imani potofu za kishirikina zinazosababisha mauaji ya albino na vikongwe na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya wale wote watakaobainika kujihusisha na vitendo vya mauaji ya makundi hayo.

Utekelezaji wa Ilani

16. Kazi kubwa ya Serikali za CCM katika kipindi cha miaka mitano ijayo itakuwa ni kuendeleza mapambano dhidi ya umasikini, ukosefu wa ajira, rushwa; na kudumisha umoja, amani, ulinzi na usalama. Ili kutimiza azma hiyo, CCM itazielekeza Serikali zake zisiwe kubwa, zenye watumishi weledi, waadilifu na wawajibikaji. Serikali zisizo na urasimu unaokwamisha na kuchelewesha maamuzi na utekelezaji. Serikali zitakazongeza maradufu au hata zaidi ukusanyaji wa mapato yake ili zijitegemee kadri inavyowezekana kwenye bajeti zake.

17. Vile vile katika kipindi cha Ilani hii, Chama Cha Mapinduzi kitaziagiza Serikali zake kuendeleza na kuimarisha mfumo wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN na BRP) katika kutekeleza Ilani na kusimamia utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kipaumbele unaozingatia nidhamu ya utekelezaji katika muda uliopangwa, ufuatiliaji makini na wa kina, pamoja na kupata ufumbuzi wa vikwazo na changamoto za utekelezaji.

#HapaKaziTu