Showing posts with label mwezi wa ramadhani. Show all posts
Showing posts with label mwezi wa ramadhani. Show all posts

Thursday 4 September 2008

Huu ni mwezi mgumu kwenda Zanzibar


Seagull ikishusha abiria hapo Zenj wakitokea Dar mwishoni mwa wiki iliyopita.


Sea Express ikushusha abiria tokea kisiwa cha pili


Msongamano wa abiria wa kwenda Zenj kabla ya mfungo wa Ramadhani katika bandari ya Dar.


Kwa wale ambao husafiri mara kwa mara kati ya Zenj na Dar au Zenj na Kisiwa Cha Pili watakubaliana nami kuwa sasa kwenye boti kuna viti vya kulala na ni tofauti kabisa na siku kadhaa zilizopita au kwa maneno mafupi kabla ya kuanza kwa mwezi wa Ramadhani. Kwa kawaida mwezi wa Ramadhani abiria wa boti na hata ndege hupungua sana kati ya Zenj-Dar na Pemba.

Sababu kubwa ya kupungua kwa wasafiri ipo wazi, kwani huu ni mwezi ambao wengi hufunga na hasa wakaazi wa visiwa hivi viwili, Hivyo wengi wao hawapendi kusafiri ili kuepuka adha ya kupata futari na misukosuko mingine ambayo inaweza kuwasababisha kufuturu kabla ya wakati. Zaidi waumini wengi utumia muda huu kuhudhuria sala zote za siku ili kukamilisha funga yenye uhakika na iliyokamilika.

Wageni ambao hupenda kufakamia kila wakati, nao ujiepusha kwenda Zenj ama Kisiwa cha Pili, kwani kuanzia mama lishe, migahawa na hoteli hufungwa hivyo kuwafanya kuwa katika hali ngumu sana ya kushawishi matumbo yao kuwa hakuna chakula asubuhi wala mchana... Hii uwakuta hata watalii ambao zaidi ya kukimbia kutofunga hata mavazi yao huwa hayana nafasi visiwani humo.

Hata hivyo, baada ya futari hakuna sehemu nyingine hapo Bongo ambayo unaweza kufaidi misosi ya nguvu kama Zenj... Kwani sehemu nyingi hufunguliwa na kuuza misosi ya nguvu hadi saa sita ya usiku. Maduka huwa wazi usiku na hata zile baa zinazojificha mchana na kuuza ulabu kwa mlango wa nyuma huwa wazi. Kwa ufupi Usiku huwa kunachangamka sana kuliko usiku wa miezi ya kawaida. Wengi ambao hawapendi kuamka alfajili kwa kuwahi daku hupenda kushindilia misosi hiyo hadi mishale ya saa sita na akilala inakuwa imetoka.

Friday 29 August 2008

Mwezi wa gharama wakaribia huko Zenj...

Unapokaribia mwezi mtukufu wa Ramadhani, Jiji la zenj hujaa pilikapilika nyingi mno, ni rahisi sana kutofautisha jinsi watu wanavyoishi kabla ya mwezi huo kwani kila mtu huwa kwenye pilika za hali ya juu, tofauti kabisa na miezi mengine yoyote katika mwaka.

Kijana mmoja aliwahi kunilalamikia kuwa ingependeza kama kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikawa kama fainali za kombe la dunia kutokea mara moja kwa miaka minne tena katika nchi tofauti. Akiwa na maana iwapo itakuwa zamu ya Tanzania kufunga mwaka huu nchi zingine hazitofunga mpaka zamu yao ikifika....! Sikupata picha kamili ingekuaje kwa nchi zaidi ya mia mbili duniani humu.. Mawazo kama haya uzaliwa kichwani mwa mtu kutokana na majukumu mengi katika mwezi huo.

Kabla ya mwezi kufika wengi hupata mialiko ya kuhudhuria shughuli za arusi, hii yote ni katika kujiandaa na mfungo, kwani wengi hupenda kufuturu majumbani mwao, hivyo vijana wengi hupenda kufunga ndoa katika kipindi kama hichi ili mradi tu awe na uhakika wa kupata futari murua akiwa kwake.

Hali halisi ya Zenj na hasa katika kuandaa futari husababisha ugumu mkubwa katika mwezi huu. Bei za bidhaa hupanda maradufu hivyo kuwa usumbufu mkubwa kwa waakazi wengi wa kipato cha kati visiwani hapo. Ikiwa bado siku kadhaa kabla mwezi huo kuanza bei ya nyama kwa kilo sasa ni zaidi ya sh. 5,000 huu ni mzigo mkubwa. Ikumbukwe bidhaa za vyakula kisiwani humo nyingi hutoka Bara na Pemba, hata hivyo uonekana kama havitoshi pamoja na ukubwa wa gharama.

Sina hakika kama kisiwa cha pili bado wataendeleza mgomo wao wa kutopeleka vyakula huko Zenj, baada ya muafaka kurudishwa tena mezani, na sina hakika hali itakuaje baada ya kasheshe za karibu miezi mitatu kuhusu Zenj kama nchi zitaathiri vipi mfungo wa mwaka huu. Kawaida pamoja na rais wa Zenj kutembelea kwenye markiti akiwaomba wauzaji kupunguza bei, bei hubaki palepale. Safari hii rais atavuka hatua ya kwenda markiti, kwani itabidi kuwashawishi waletaji bidhaa kufanya hivyo na kuweka siasa kando katika mwezi huu.

Ikumbukwe kuwa wananchi hao hujiandaa kwa muda wa miezi kumi kuja kufunga kwa mwezi mmoja, kwani bila ya kujiandaa na kujiwekea akiba unaweza kuja kuumbuka katika kutafuta futari hivyo kuufanya mfungo kuwa mgumu zaidi. Zaidi ya wao wenyewe kujiandaa, ndugu wengi waishio nje ya Zenj na hasa nje ya Afrika wamekuwa mstari wa mbele kusaidia kupunguza makali ya mwezi huu, kwa kujaza wazenj wengi katika ofisi za west union. Kwani pamoja na kujiandaa na futari pia ni mwanzo wa maandalizi ya sikukuu ya Idd ambayo usheherekewa kwa muda wa siku nne mfululizo. Sherehe hizo ni kubwa sana hasa kwa watoto ambao uwakera wazazi wao kwa kudai nguo mpya na maridadi, toys na kadhia zingine ziendanazo na sherehe hizo.

Mie binafsi napenda kuwatakia Wafungaji wote Mfungo mwema....