Thursday 14 June 2007

Mahakama Kuu ni Kimeo....

Nimewahi kuandika kuhusu mashaka makubwa ya mahakama za zenj katika mabandiko yaliyopita, leo hii kumeibuka kadhia nyingine ambayo hapana shaka ipo kwa muda mrefu tu huko zenj..

Imeripotiwa kuwa mahakama za zenj, hasa Mahakama Kuu haina majaji wa kutosha hivyo kukosa hadhi ya kuitwa Mahakama Kuu kwa mujibu wa katiba ya visiwa hivyo. Tatizo la Majaji huko visiwani lipo kwa muda mrefu sana, ingawa kuna wakati smz ilijitia kifua mbele kwa kukodisha majaji toka nje ya visiwa hivyo(Mapopo).

Kwa mwananchi wa kawaida hawezi kuamini kuwa Visiwa hivyo havina majaji, kwani wao mtu yoyote afanyae kazi mahakamani basi ni jaji, kama ilivyokuwa katika hospitali zao kwa wafanyakazi wote huitwa ni madokta.

Pengine ujuha huu wa kushindwa kutofautisha mgawanyiko wa ngazi za wafanyakazi, upo ndani ya vibosile wa SMZ kiasi cha kujisahau kuwa hawana Majaji wa kutosha kuendesha kesi lukuki katika Mahakama Kuu. Udhaifu wa mahakama za zenj na hasa katika watendaji wake umekuwa ni gumzo kubwa katika kipindi hiki, wakati kuna fufunu ya uteuzi wa Jaji Mkuu mpya wa Tanzania,

Ukiachana na hayo ambayo yanatia kichefuchefu, Mahakama ya Mkoa wa Mjini Magharibi ina Mahakimu watatu tu, ambao kwa maneno mengine ndio Mahakimu wa Mikoa yote ya Zanzibar! kwani sio siri kuwa sijawahi kusikia Hakimu wa Mikoa mengine minne wakitajwa, licha ya kesi walizohukumu kuripotiwa...! Hao Mahakimu wa wilaya wapo kwa hesabu ya vidole, na wengi wao wapo katika Mahakama za wilaya ya Mjini na ile ya Magharibi... Nasikia huko Pemba kuna mahakama ya Mkoa vilevile, hata hivyo Hakimu wake kutwa yupo Vuga!

SmZ kupitia kwa ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali wanapaswa kuja na suluhisho la kudumu kuhusu kadhia hii, na sio kila siku kuwa ni watetezi wa uchovu wa SMZ. Iwapo wao ndio wanasimamia Mahakama na sheria zake, basi hawana budi kuwa na mipango madhubuti ili kuona kuwa vyombo vya haki visiwani humu vimekamilika kwa mujibu wa sheria na katiba ya visiwa hivyo. Kitendo cha kuwaondoa Wapopo katika Mahakama zetu kilikuwa kizuri kwa manufaa ya watu na uchumi wetu unaodorola, aidha ipo haja basi ya ofisi hiyo kupanda Jahazi hadi bara ili kupata Majaji wenye kujua sheria zetu na maadali ya Mtanzania.

Friday 8 June 2007

'Ongezeko la Uzaaji UK' Wazenj Hawako Nyuma....

Imeripotiwa kuwa kumekuwepo na ongezeko kubwa la uzaaji hapa UK, ikiwa ni ongezeko kubwa kwa miaka 26. Ongezeko hilo la uzaaji, limechangiwa na wahamiaji miongoni mwao wakiwa ni wazenj.

Moja kati ya watoto watano wanaozaliwa hapa, amezaliwa na mhamiaji, hivyo kufanya ongezeko la asilimia kumi kwa mwaka kwa watoto wanaozaliwa na wahamiaji. Mwaka 2006 walizaliwa watoto 669,531 kwa wastani wa kila mzazi wa 1.87 huku wahamiaji wakizaa asilimia 21.9 ya watoto wote waliozaliwa mwaka 2006. Wahamiaji wengi ni kutoka nchi za ulaya ya mashariki, wengi wao wakiwa ni Wapoland. Zaidi kumekuwepo na ongezeko kubwa watoto toka kwa wanawake wa Pakistan, India, Afrika na Mashariki ya Kati. Wachunguzi wa mambo wanasema tokea mwaka 1997 (labour ilipoingia madarakani) kiasi cha wahamiaji milioni 1.5 wamehamia UK.[1]

Wanawake wengi toka Zenj hawapo nyuma katika suala la uzaaji, wengi wa wanawake hao ni kinamama wa nyumbani. Nilipojaribu kuulizia zaidi kuhusu uzaaji huo wa kasi, wengi wao walisema ni kutokana na mafao mazuri ambayo hutolewa na serikali ya hapa, hivyo kutokuwa na wasiwasi juu ya malezi na usomeshaji wa watoto hao tofauti na kama ingekuwa huko Zanzibar, ambapo jukumu lote lipo kwa mzazi pekee..!



1.Source: Daily Mail, June 8 2007.

Saturday 19 May 2007

Madeleine wa Zenj

Wengi wetu sasa tunajua kutoweka kwa Madeleine, mtoto wa miaka minne, raia wa Uingereza aliyetoroshwa huko Ureno yapata siku kumi na sita sasa. Vyombo vya habari na hasa vya hapa UK vimekuwa vikitoa maendeleo ya sakata hilo katika kila habari zao. Hivyo kuweza kuwafikia watu wengi kadiri iwezekanavyo. Leo wakati Fainali ya Kombe la FA, kati ya Man Utd na Chelsea, video ya dakika nne ya Madeleine inategemewa kuonyeshwa.Hivyo kuweza kutazamwa na watu zaidi ya nusu bilioni duniani kote.

Huko Zenj kuna mtoto wa kike wa miaka kumi na sita ameripotiwa kutoroshwa na mwalimu wake yapata miezi mitatu sasa. Jeshi la polisi visiwani humo limeomba kusaidiwa na jeshi la polisi la kimataifa(interpol) katika kumtafuta mtoto ambae jina lake ni Maryam Farid Said.

Tofauti ya Maryam na Madeleine ni kubwa sana, Madeleine ni mtoto mdogo sana asiejua hili na lile, wakati Maryam ni msichana mkubwa ambae anajua nini anafanya. Cha kusisimua zaidi ni kuwa Maryam hii ni mara yake ya pili kutoroshwa na wanaume.

Msichana huyo ambae alikuwa ni mwanafunzi wa shule ya binafsi ya bweni huko Bububu Zanzibar ana undugu na Rais wa Tanzania Jakaya M. Kikwete hivyo kuweka utoroshwaji wake kuwa wa mvuto zaidi. Polisi wa visiwani hapo wanashuku kuwa mtoto huyo atakuwa ametoroshwa na mwalimu wake ambae ni raia wa Uganda.

Iwapo mtoto huyo akipatikana, wazazi wake ambao sasa wanamtafuta, itabidi wamkalishe kikao mtoto huyo, kwani hii ni mara ya pili kutoroshwa hivyo kujenga hofu juu ya tabia yake kwa ujumla. Hapana shaka kuwa mtoto huyo anashirikiana na hao wanao mtorosha hivyo kufanya utafutaji wake kuwa mgumu zaidi. Zaidi nawatakia kila la heri Wazazi wa mtoto huyo katika jitihada za kumtafuta mwanao. Hali kadhalika wanachi ambao kwa namna moja ama nyingine ambao watakuwa na habari yoyote ya kuweza kupatika kwa mshichana huyo watoe ushirikiano wao kwa kutoa taarifa katika vyombo husika.

Wednesday 16 May 2007

Wazenj wa UK na Vituko Vyao...

Nilipofika hapa UK yapata mwezi sasa, nilikuwa na hamu kubwa ya kukutana na watz wanaishi huku, zaidi kuonana wa Wazenj wa huku ili niweze kubadilishana nao mawazo kuhusu vituko, vioja na kadhia kadha wa kadha za huko Zenj.
Well haikuwa kazi kubwa kabisa kuwatafuta wazenj, kwani nilipofika mwenyeji wangu alikuwa ametingwa sana na kazi zake za kila siku, hivyo alinitaka radhi kuwa hataweza kunipikia chakula cha jioni. "nikahisi sasa ndio kuna kulala na njaa" Hata hivyo alinitoa hofu kuhusu kupata kwa msosi, kwa kuniambia kuwa tayali ameshatoa oda ya msosi, ambao anahisi kuwa utanifaa na kunikumbusha huko bongo, na hasa katika soko la usiku la chakula huko Zenj(Forodhani).
Muda si mrefu tokea kuingia ndani kwa mwenyeji wangu, chakula cha jioni kikaletwa! MMhm nikaamini maneno yake, kwani ulikuwa ni msosi ambao nimeukasa kwa muda mrefu sasa... Chapati, samaki waliokaangwa kwa viuongo rukuki vya kisiwani, mchuzi mzito maandanzi, na mazagazaga mengine kibao.. ile harufu yake ilipofika puani mwangu, mate kibao yalijaa mdomoni. Baada ya kufakamia msosi ule wa jioni, mwenyeji wangu aliniambia kuwa umetoka kwa Wazenj ambao wao wamefungua mgahawa bubu wa kupika vyakula kwa order.
Asubuhi yake niliamua kuingia mitaani kuangalia hili na lile, baada ya kutembea tembea bila dira maalumu nilijikuta naingia kwenye sehemu ya kukatia nywele. Hapo niliamua kupunguza nywele zangu. Hata hivyo kulikuwa na watu wengi, hivyo nikabidi kusubiri. Vinyozi walikuwa kama wanne hivi wakiendelea na kazi zao... baadae walianza kuongea kwa lugha ya kiswahili yenye rafudhi ya mwambao, nikahisi hapana shaka watakuwa ni Wazenj, hivyo nikajiweka sawa kuwasikiliza. Hata nafasi ya kunyolewa ilipopatikana nilikaribishwa kwa lugha ya Kiingereza... mimi nikajibu kwa lugha ya Kiswahili. Nikanyolewa huku tukiongea hili na lile na hasa mambo ya Zenj. Nilipomaliza nikawauliza sehemu ambayo ninaweza kukutana na Watz wengi kwa wakati mmoja. Wakanielekeza.
Ni jioni, nikaamua kwenda kutembelea sehemu ambayo nitakutana wa Watz wengi kwa wakati mmoja. Ni baa maridadi kabisa na ya kisasa. Nilipoingia ndani ilikuwa imejaa watu kibao wa kila rangi. Baa ya kuchukua bia yangu, nikaanza kutafuta sehemu nzuri ya kukaa. Nikaona bora nokae karibu na meza moja iliyokuwa imejaa weusi kibao amboa walionekana wakifurahia vinywaji vyao ipasavyo. Nilipoangalia vizuri meza hiyo nikaona kuna kijana ambae niliwahi kuishi nae Malaysia ambae ni Mzenj. Nikamwita na kumkumbusha, kwani alionekana kunisahu. Baada ya kunikumbuka alinikaribisha kwa furaha tele kwenye meza yao. Akanitambulisha kwa rafiki zake, ambapo niligundua kuwa wote ni kutoka Zenj...Baada ya glass mbili hivi nikamuuliza kama kuwa Watz wa bara katika baa hiyo. Akanionyesha kwa kidole kuwa wamekaa kule... Well nikamwambia wacha nikawasalimu nao pia.
Baada ya kukaa kwa Wabongo kwa muda kadhaa nikahisi kuwa kuna kitu kinaendelea kati ya Wazenj na Wabongo... kwani ninapotoka sijawahi kuona utengano wa aina hii. Well sijui ni nani aliyeanzaa. Ila kwa haraka haraka nikahisi kuwa ni Wazenj ambao walikuwa na vituko ambavyo vimepelekea kuwepo na utengano huu... Hata hivyo nitazidi kuchimbachimba ili nijue vituko vyao.....