Tuesday 30 September 2008

Idd Mubaraka


Napenda kuwapa mkono wa idd wadau wote wa blog hii. Sikukuu njema

Monday 29 September 2008

Wanafunzi na Mazingira...Case: Mwanza





Mazingira ya shule ya Msingi Igoma. Shule hii ina klabu ya mazingira ya wanafunzi na moja ya kazi zake ni kutunza mazingira ya shule hiyo.




Wanafunzi wa shule ya Msingi Kirumba wakiandaa shimo kwa ajili ya utengenezaji wa mbolea kwa taka za jikoni. Klabu ya Mazingira katika shule hiyo hujishughulisha na usafishaji wa mazingira katika kata yao ya Kirumba.


Uandaji wa mashimo kwa ajili ya kutengeneza mboji kutokana na taka za jikoni, katika shule ya Msingi Isenga

Wednesday 24 September 2008

Chumbe...Na sifa zake





Chumbe ni kisiwa chenye ukubwa wa hekta 20 na kipo umbali wa kilomita 6 toka Mji Mkongwe - Zanzibar. Ni rahisi sana kukiona kisiwa hiki ukiwa unaingia ama kutoka Zanzibar kwa njia ya bahari... aidha iwapo unaingia kwa njia ya anga unaweza kukiona kisiwa hiki kilichojaliwa utajili wa mazingira ya baharini.

Umaarufu wa Chumbe kwa wakaazi wengi wa Zenj hautokani na umaarufu unaojulikana duniani kote katika mazingira ya kisiwa hicho, bali ni kutokana na kauli za viongozi wa kisiasa wa visiwa hivyo wakitumia kisiwa hicho kama mpaka wa mambo mengi ya kisiasa baina ya Zanzibar na Tanzania Bara. Viongozi wengi kuanzia Marehemu A.Karume, rais wa kwanza wa visiwa hivyo amehawi kunukuliwa akisema baadhi ya mambo ya Tanzania Bara mwisho wake ni Chumbe.... na wengi kwa wakati tofauti wamekuwa wakiendelea kutumia kisiwa hicho kutenganisha mambo ya SMZ na JMT.... Pengine hata sasa kwenye sakata la mgao wa mafuta wengi watadai kuwa JMT mwisho wao ni Chumbe...

Zaidi ya mambo ya kisiasa kisiwa hicho kinajulikana duniani kama ni kisiwa cha kwanza duniani kuwa na "Coral Park" inayomilikiwa kibinafsi, kisiwa cha kwanza katika Tanzania kuwa na "Marine Park" aidha ina hoteli ambayo ipo kwenye hoteli 20 bora duniani kimazingira "Eco Hotel". Zaidi, kisiwani humo unaweza kuwaona kobe kadhaa, na kuna kobe mwenye miaka zaidi ya 125 ndani ya kisiwa hicho.. Zaidi kisiwa hicho kimewahi kushinda tuzo ya British Airways- Tourism for Tomorrow, mwaka 2000

Saturday 20 September 2008

Jumba la Maajabu- Beit al Ajaib - House of Wonders....Ni kwanini likaitwa hivyo?



Ni rahisi kuliona unapoingia Zanzibar kwa njia ya bahari. Ni jumba lenye historia ndefu sana katika kisiwa cha Zenj. Leo hii Jumba hilo lenye zaidi ya nguzo 40 linatimiza miaka 125 tokea kujengwa kwake. Mengi yamelikuta jumba hilo kiasi cha kuwa mojawapo ya vivutio vya utalii katika Zanzibar.

Katika kusherehekea miaka 125 ya Jumba hilo ni vema kujikumbusha historia yake na umuhimu wake katika historia ya Zanzibar. Ubunifu wa jumba hili ulifanywa na askari wa meli toka Scottland na lilijengwa na surtan Barghash bin Said katika mwaka wa 1883, kwa ajili ya ofisi yake. Zaidi matumizi ya jumba hilo yamekuwa yakibadilika kadiri miaka ilivyokuwa ikienda na jinsi tawala zilivyokuwa zikibadilika visiwani humo.

Matumizi ya jumba hilo kati ya mwaka 1870-1888(miaka 120 nyuma)ilikuwa ni kwa ajili ya sherehe za kitaifa, kumbuka wakati huo Zenj ilikuwa chini ya utawala wa kisultan... Hadi kufikia mwaka 1913 Waingereza walilifanya jumba hilo kuwa ofisi ya serikali za mitaa. ofisi hizo zilidumu hadi wakati wa uhuru na baadae mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964. Kati ya mwaka 1964 na 1977 Jumba hilo maarufu lilitumika kama jumba la kumbukumbu za ASP na SMZ kwa ujumla... Kwa mfano ndio ilikuwa sehemu pekee ya kuweza kuona magari ya Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Abeid Karume.

Ilipoundwa CCM mwaka 1977, Jumba hili liliendelea kutumika kama makumbusho ya ASP na taifa na kama ofisi ya CCM, hali ya jumba haikuwa ya kuridhisha sana pamoja na kuwa na historia ndefu.


Kuja kwa mamlaka ya hifadhi na uendelezaji mji mkongwe kulifungua ukurasa mpya wa hifadhi ya mji mkongwe hii ilikuwa katika miaka ya mwisho ya 1988 hadi mwaka 1994 ambapo sheria ya mamlaka ya hifadhi na uendelezaji mji mkongwe ilipopata baraka za Baraza la wawakilishi na siginecha ya prezidenti.. Mwaka 1992 nilipata kufanya kazi na UNDP kaatika kukarabati Jumba hili na ni hapo nilipopata nafasi ya kuweza kuvinjari jumba hilo kwa mapana na marefu... ni wakati ambapo nilipenda kujua ni kwa nini jumba hilo likaitwa la maajabu, ni wakati ambapo nilipenda zaidi fani yangu ya ujenzi na nilikuwa na kila raha nafuraha ya kushiriki katika matengenezo/ukarabati wa jengo hilo...

Moja ya sifa kubwa ya ya jumba hili ni vita vilivyodumu kwa muda mfupi kabisa katika historia ya vita duniani! Vita hivi vilitokea mwaka 1896, na baada ya vita hivi ndio picha halisi ya jumba hilo kwa leo inavyoonekana. Hii ni baada ya kuunganisha mnara wa saa uliokuwa mbele ya jengo hilo na jengo lenyewe.

Lakini ni kwa nini likaitwa jumba la maajabu?... Wataalamu wa histori ya Zenj wanasema umarufu wa jengo hilo umejengwa kwa sifa zifuatazo;-
1. Ni jumba la kwanza Afrika ya Mashariki kuwa na Umeme.
2. Ni jumba la kwanza Afrika ya Mashariki kuwa na lifti( elevator)
3. Ni jumba la kwanza Afrika ya Mashariki kuwa na mfereji ndani ya nyumba( Bomba la maji)

Lakini kwa nini Jumba hilo sio maarufu sana miongoni mwa wakaazi wa visiwa hivyo? Hii inatokana na imani kuwa katika nguzo zaidi ya arobaini za jumba hilo ni makaburi ya watumwa waliozikwa wakiwa hai...