Wednesday 25 March 2009

Huu Ndio Wakati Muafaka wa Kumiliki gari la Waziri wa SMZ


Mara kadhaa nimewahi kuandika juu ya ubabe wa SMZ dhidi ya Mahkama za Zenj, zaidi ya SMZ hata wananchi wakati mwingine wamekuwa na ubabe dhidi ya maamuzi ya Mahkama za Zenj. Kumekuwepo na hukumu mbalimbali kila siku, ila zinazonipa mashaka ni zile hukumu za kesi za madai. SMZ kama mhimili wa Mahkama imekuwa kwa mara kadhaa ikishitakiwa katika kesi za madai kutoka na ubabe wake wa kushindwa kufuata sheria zake.

Kesi nyingi ambazo SMZ na asasi zake zimekuwa zikijikuta matatani zinatokana na matatizo ya ardhi na madeni yanayotokana na huduma mbalimbali wanazoomba kufanyiwa na hatimae kushindwa kulizipia. Mwaka 2006 niliwahi kuandika jinsi gani Mahakama za Zenj zinapoonja ubabe wa SMZ na wananchi wake kiasi cha mtu kujiuliza iwapo utakuwa na matatizo ambayo yanahitaji haki kutendeka utakimbilia wapi!

Mwaka huo wa 2006 kulikuwa na kesi mbili za muda mrefu ambazo zilipata hukumu yake, lakini zikakutana na ubabe wakati wa utekelezaji wake, kama inavyoelezwa kwa kirefu chini ya bandiko la "Mahakama za Zenj na Matatizo ya Ubabe"

SMZ kwa kujua au kwa makusudi kabisa imekuwa ikipuuza madai mengi ya wananchi wake dhidi ya asasi yake. Nakumbuka kesi nyingi katika hili lakini moja iliyonivutia ni ile ya asasi moja ya SMZ kuibeza amri ya Mahkama kuhusu uvunjaji wa mabanda ya biashara ili kupisha ujenzi wa soko katika eneo la Mwanakwerekwe.

Wengi wa wananchi wamekuwa na madai mbalimbali na wanapokimbilia katika vyombo vya SMZ ili kupata suluhisho, uvunjika moyo jinsi wanavyosumbuliwa na inahitaji moyo wa ziada kwenda Mahakamani ambako ni sawa na kumpa Nyani kesi ya Ngedere. Binafsi nimekuwa nikipigwa tarehe zaidi ya miaka tisa kwa madai ya haki yangu ambayo niliingia mkataba na SMZ.

Hatua ya Mahakama Kuu kupiga mnada magari ya SMZ kwa kushindwa kulipa deni lake la matengenezo ya ikulu ndogo huko Pemba ni ya kuungwa mkono sana. Amri hii iwapo itafanikiwa itakuwa ya kuigwa na kupigiwa mfano. Moja ya mali ambayo inaweza kupigwa mnada ni gari la Mh. Waziri ambae wizara yake inahusika moja kwa moja na kushindwa kufuata taratibu za kuheshimu mikataba. Nategemea jeshi la polisi visiwani humo kusimamia vizuri ushikwaji wa mali hizo za SMZ na hatimae kupigwa mnada. Hii inaweza kuondoa usingizi mzito kwa watendaji wa SMZ kuhusu kuheshimu mikataba wanayoingia.

Tuesday 24 March 2009

Agha Khan na Mji Mkongwe....

Agha Khan Development Network kwa zaidi ya miaka kumi sasa imekuwa ikifanya ukarabati mkubwa katika baadhi ya Majengo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar. Na hivi karibuni walikuwa katika hatua za mwisho mwisho za kukamilisha ukarabati wa Forodhani Park.
Leo nitaangalia majengo mawili, nikianzia na Stone Town Culture Centre maarufu kama Old Dispensary ambalo ni mojawapo ya majengo yaliyofanyiwa ukarabati na AKDN baada ya kutupwa na SMZ. Aidha jengo lingine lililolembewa na SMZ ni Extelcom, ambalo leo hii kuingia ndani ya jengo hilo inabidi uwe nazo mfukoni.

Old Dispensary.

Jengo hili ujenzi wake ulikamilika mwaka 1894 chini ya ushauri wa kihandisi toka Uingereza. Michoro na mafundi wa jengo hili ni kutoka India ambako ndipo alipotoka mwenye jengo Bw. Tharia Topan ingawa hakuweza kuona kukamilika kwa ujenzi wa jengo hilo.

Mjane wa Topan aliweza kuendeleza ujenzi na baadae kuliuza. Lengo la Topan lilikuwa kujenga shule na zahanati, ambapo mmiliki wa mwisho wa jengo hilo aliweza kufanya sehemu ya chini ya jengo hilo kuwa zahanati na sehemu ya juu kuwa sehemu ya makaazi yake. Huu ndio ukawa mwanzo wa jina maarufu la Old Dispensary.

Miaka 70 baadae jengo hilo likawa tupu, na kuendelea kuwa tupu huku likiendelea kuchakaa na kuharibika ni hadi pale Agha Khan walipopewa ruhusa ya kulifanyia ukarabati ili kunusuru ufundi mkubwa uliotumika katika ujenzi huo kupotea na hasa nakshi zake za kihindi.


Miaka 100 baadae Agha Khan waliweza kupata kibali cha ukarabati wa jengo hilo, zaidi walipewa mkataba mpya wa kukodishwa jengo hilo na SMZ chini ya muda maalumu. Pichani hapo juu ni old dispensary baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa .


Extelcom
Jengo lingine ambalo lilikuwa chini ya SMZ na kuachwa bila aina yoyote ile ya usimamizi hadi pale walipotokea tena agha khan na kuamua kuligeuza toka ofisi hadi kuwa hoteli ya kitalii. Sasa jengo hili linajulikana kama Serena Inn

Thursday 19 March 2009

Movie...Hobbie iliyokwisha huko Zenj


Jengo hili sasa halitumiki tena kama jumba la Sinema..!

Wednesday 18 March 2009

Amin Salmin Amour, aonja tamu ya siasa

Ni baada ya kushindwa kutamba kwenye kura za awali za kumtafuta mgombea kwa tiketi ya CCM katika jimbo la Magogoni huko Zenj. Amin ambaye ni mtoto wa rais mstaafu wa Zenj Salmin Amour maarufu kama Komandoo, alikuwa ni miongoni wa wagombea 10 wa CCM waliojitokeza kuwania nafasi hiyo.

Umaarufu wa Amin unakwenda nyuma zaidi kipindi cha kwanza cha Komandoo Salmin alipokuwa madarakani,umaarufu wake ulijengeka kwa kuwa mjasirimali zaidi ya siasa na kwa kujaribu kila aina ya biashara za muda mfupi! Hatua yake ya kuingia kwenye siasa kwa wengi ilikuwa ni karata yake muhimu ya kujinyanyua tena baada ya kushindwa kudumu katika sekta ya biashara.

Kwa habari zaidi tembelea hapa