Wednesday 14 February 2018

Uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Kuhojiwa Mahakamani...



Bwana Rashid Salum Adiy wa Kikwajuni Zanzibar, na wenzake 39,999 wamefungua shauri katika mahakama ya Afrika Mashariki kuhoji uhalali wa Muungano wa Tanzania.

Watakaohojiwa katika shauri hilo ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi Zanzibar na Mwanasheria Mkuu wa Jamhuri ya Muungano Tanzania.

Shauri hilo limepangwa kusikilizwa tarehe 8 ya mwezi wa 3 mwaka 2018.

Sunday 4 February 2018

Asiyetaka Kuishi Unguja Atoke!


  • Karume Amwambia Balozi wa Iran.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Tanzania Bw. Karume amesema kuwa Zanzibar itafuata azimio lake la kwanza la mwaka 1964 lililofanywa baada ya Mapinduzi kuwa " Yeyote ambaye hakubaliani na hali ilivyo nchini, anaweza kuondoka wakati wowote".

Bwana Karume amesema hayo alipokutana na Balozi wa Iran aliye nchini Ethiopia ambaye kwa wakati huu anatembelea nchini Tanzania Bw. M.E Moghadom. Walizungumza juu ya wasichana Waajemi walioozwa Zanzibar wiki iliyopita.

Bw. Karume amesema hakuweza kusema chochote juu ya wasichana wane Waajemi ambao wameolewa kwa vile walikuwa wakiishi na mabwana zao  "Wanafurahia sana" alitamka.

Bw. Karume alisema "Hatuwezi kufuata vile watu wengine wanafanya kwa kuwa sisi ni watu huru".

Aliongeza "Tunajivunia kusema kuwa tunaishi kwa furaha".

Alimwambia Balozi huyo kuwa wasichana wamekwishaolewa na kwamba walikuwa wakiishi kwa furaha na mabwana zao.

Kuhusu sheria za ndoa, Bw. Karume alisema zilifanywa ili kuwezesha kila raia kuoa bila kubaguliwa.

Alisema yale yaliyotokea katika magazeti yalikuwa jitihada za mabeberu na kuongeza; "Ninaposema mabeberu sisemi weupe peke yao lakini wote wanaofuata amri zao".

Alisema kuwa nchi zilizo jirani haziwezi kufahamu hila na maarifa ya mabeberu lakini sisi tunazijua hatuna hofu kwa sababu hivi karibuni watajulikana.

Bw. Karume aliongeza kusema kuwa habari hizo zote zilikuwa zikitoka kwa watu ambao hawakupendezwa na maendeleo yaliyokuwa yakifanyika nchini.

"Tutawezaje kuishi kwa udugu ikiwa tutakubali wengine kufikiri kuwa watu wa chini?" Aliuliza Bw. Karume.

Alisema wajibu wa kwanza wa Chama cha Afro-Shiraz Party ulikuwa kuondoa ukabila na kufanya watu kujisikia wenye furaha na kufurahia uhuru walioupata kwa shida.

Aliongeza kusema kuwa mafungu mafungu ya watu yalimalizika katika Zanzibar na kusema " Watu watawezaje kufurahia uhuru wao ikiwa ukabila unaendelea  katika Jamii?"

Bw. Karume alisema ulikuwa wajibu wa watu wote waliostaarabika kuondoa kabisa ubaguzi na shida miongoni mwa watu.

Aliuliza " Tutawezaje kuwa na umoja ikiwa hatuwezi kuoana?"

Bw. Karume alimwambia Balozi aliyetembelea kuwa alikuwa huru kukutana na Waziri wa wasichana walioolewa katika State House na akakutana nao.


Chanzo: Gazeti la Baraza 
Toleo: Namba 1623
Tarehe: Alhamisi Oktoba 1, 1970
Bei: Senti 35 Kenya, Senti 40 Tanzania na Uganda 

Friday 2 February 2018

Safari za Dr Shein nje ya nchi zinawakera nini jirani zetu?





Kila pale Dr Ali Mohamed Shein, Rais wa Zanzibar anapofanya safari nje ya nchi yake ya Zanzibar, lazima panuke kidudumtu. Hii ni mara ya pili mfululuzo Dr Shein amekuwa ziarani huku Zanzibar fitina nyengine imezuka. Hivi hizi fitna haziji wakati mwenye akiwa yupo hapa nchini!

Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Muuungano, Dr John Pombe Magufuli kwa mamlaka aliyonayo amesimamisha usajili wa meli za nje, ambalo ni suala lililo chini ya mamlaka ya serikali ya mapinduzi (SMZ).

RaisMagufuli alimwita waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji wa Zanzibar na kumpa maagizo hayo ya kusitisha kama vile yeye Waziri Ali Karume anawajibika kwa Rais Magufuli. Ingawa Waziri Ali Karume ameteuliwa na Rais wa Zanzibar Dr Ali Mohamed Shein, lakini ndani ya katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuna sura maalumu inayozungumzia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hivyo kumfanya Rais Magufuli kutumia nguvu hii kunukisha kidudumtu.

Wakati Dr Shein yupo ziarani nchini Emirates, Rais Magufuli kachukuwa uamuzi wa kusitisha usajili wa meli za nje zinazofanywa na Zanzibar kupitia wakala wake. Huku Zanzibar ikiamini kuwa ni kuingiliwa kwenye anga za mamlaka yake, kwani usajili wa meli sio suala la Muungano. Kitendo hichi kimemchukiza sana Dr Shein na kutowa maelezo mara tu alipowasili uwanja wa ndege.

Dr Shein alisema “Sisi tulianzisha wenyewe Kampuni yetu ya Usajili wa Meli, Hili la kusajili Meli si jambo jipya, na nchi Duniani haya yanafanyika, Na mimi sidhani kama Zanzibar itazuiliwa kuregister, sidhani kama lipo hivyo, Mimi sijasikia hivyo, Mimi ninachojua kuna timu za Wizara za Serikali mbili zinazungumza na mazungumzo yatakavyo kwenda mimi nitayajua. Sidhani kama Zanzibar itaambiwa Isisajili”.

Katika mwezi wa March 2017 wakati Rais wa Zanzibar Dr Shein yupo ziarani nchini Indonesia, Rais Magufuli alitowa agizo kwa shirika la Tanesco kuikatia umeme Zanzibar kutokana na kutolipa madeni yake. Akijuwa fika kuwa suala la umeme linaendeshwa kisiasa pia ni suala la kibiashara baina ya kampuni mbili, Rais Magufuli hakuyazingatia hayo wakati wa kutoa kauli yake.

Rais Magufuli alisema “”ninaambiwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar haijalipa Sh121 billion. Ninyi (Tanesco) si wanasiasa…mnapaswa kuzingatia majukumu yenu ya kitaaluma…kata huduma ya umeme. Nimesema hata kama ni Ikulu, polisi, jeshi ama shule , hakuna mwenye deni anaepaswa kuachwa”

Amri hii iliwakera sio tu Dr Shein bali Wazanzibar wote kwa ujumla, kwani waliona ni udhalilishwaji uliopitiliza. Ikiwa nchi mbili zimeungana kwa umoja na upendo, wakati wa neema ziwe pamoja na wakati wa shida pia ziwe pamoja. Ilikuwa kinyume chake, wakati wa neema ni zetu sote lakini wakati wa shida ni zenu peke yenu.

Dr Shein alichukizwa na hatua ya kutishiwa kuzimiwa umeme na kusema hatishwi na vitisho vya TANESCO vya kuikatia umeme Zanzibar kwa sababu ya deni la Umeme kwani deni sio la leo, deni lina zaidi ya miaka 20. Alisema wote wanafahamu Zanzibar inadaiwa, na anaimani hamna anayeweza kuikatia umeme Zanzibar lakini kama wakitaka kukata wakate tu, tutawasha Vibatali.

Hapo ndio utaona picha kuwa Rais Magufuli kama anachukizwa na hizi ziara za Dr Shein anazofanya nje ya nchi. Inawezekana kuwa hapendelei Dr Shein asafiri kwa vile yeye mwenyewe amefuta safari za nje. Pia amepiga marufuku kwenda nje kiholela. Na yule atakayekwenda nje lazima apate kibali kutoka kwake. Inaweza, pia, hafurahii ziara za nje anazokwenda Dr Shein kwa vile ni zenyesura na maslahi kwa Zanzibar. Dr Shein anapokwenda nje ya nchi anakwenda kwa cheo cha Rais wa Zanzibar, hivyo haiwakilishi Tanzania hata aisemee.

Miongoni mwa sababu ambayo sitaki niipigie chapuo ni kukuwa na kuwepo tofauti baina ya viongozi wawili hawa tokea kabla na baada ya kumalizika uchaguzi wa viongozi wa ccm. Ikumbukwe marekebisho ya katiba ya chama yalipofanyika yalipitishwa na wote wakiyaridhia. Wakijuwa fika yanampa madaraka zaidi


Source: Jamii Forums

Tuesday 4 October 2016

Ashauri Mahari Ilipiwe Kodi ...



MWALIMU wa somo la biashara katika skuli ya sekondari ya Chasasa Wete Pemba Ali Hamad Nondo, amezishauri Mamlaka ya Mapato Tanzania ‘TRA’ na Bodi ya Mapato Zanzibar ‘ZRB’ kuchukua kiwango cha fedha (VAT) kwenye vyeti vya ndoa, ikiwa ni njia nyengine ya kukuza pato la taifa.

Alisema hata mahari nayo yamekuwa yakipanda siku hadi siku, na wakati wa kufungishwa kwa sunna hiyo, hutolewa cheti cha ndoa baada ya maharia kulipwa, hivyo ni yema kukawa na kiwango cha fedha kinachoingia serikalini.

Mwalimu huyo, ametoa ushauri huo alipokuwa akichangia mada kadhaa kwenye semina ya siku moja ya kuelezea umuhimu wa kulipa kodi, kwa wanafunzi na waalimu wa skuli hiyo.

Alisema kama bado TRA na ZRB hawachukua ‘VAT’ kwenye cheti cha ndo, wakati umefika sasa kufanya hivyo, maana kwenye taratibu hizo huwepo kwa cheti cha ndoa kutoka mamlaka za kiserikali.

“Mimi nauliza kwenye cheti cha ndoa kuna VAT, kama jawabu hakuna sasa anzisheni hiyo, ili mfuko wa serikali ukuwe, maana nayo mahari yanapanda kila siku’’,alishauri.

Akijubu hoja hiyo, Afisa Uhusiano wa Bodi ya Mapato Zanzibar ‘ZRB’ Khamis Makame Mohamed, alisema kwa sasa wao hawakusanyi hata shilingi moja kwenye cheti cha ndoa, ili kama jamii ikiridhia ni jambo jema.

“Hili ni jambo jema, sisi tutalichukua na kulifikisha kwa wenzetu, lakini kwa sasa pamoja na mahari kuonekana kupanda juu, lakini hatuna kodi, maana kwanza ni jambo la kiimani linataka ufafanuzi wa kina”,alieleza.

Nae Afisa Elimu kwa walipa kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA ofisi ya Zanzibar, Saleh Haji Pandu, alisema kwa sasa mamlaka hiyo, inakusanya ushuru wa forodha na kodi ya mapato pekee na wala sio kwenye cheti cha ndoa.

Mapema akizungumza kwenye semina hiyo, Afis huyo wa elimu kwa walipa kodi, aliwataka wanafunzi na waalimu hao kuwa wa mwanzo kuwadai risiti za bidhaa wafanya biashara mara wapato huduma.

“Nyinyi muwe mabalozi kwa wafanyabiashara kwamba mkishanunua bidhaa msisite kuwataka wawape risiti, maana kama hakutoa huyo ni ehemu ya kukwep kuliopa kodi.

Wakichangia mada kadhaa kwenye semina hiyo, washiriki hao walipendekeza iwepo taasisi moja pekee ya kukusanya kodi ili kuwapungizi usumbufu wafanyabiashara.

Mwanafunzi Yasseir Hamad Ali, alisema itakuwa jambo la busara kama kutakuwa na chombo kimoja cha kukusanya kodi ili iwarahisishie wanaopaswa kulipa kodi moja kwa moja.

Semina kama hiyo juzi walifanyiwa waandishi wa habari na wafanyabiashara kwa lengo la kukuza uwelewa wa ulipaji kodi kupitia TRA na ZRB.
………………………………..