Thursday 30 August 2007
Wednesday 29 August 2007
Kauli ya Nahodha ina Walakini
Waziri Kiongozi wa Zenj, ambae yupo mkoani Ruvuma ametoa kauli ya kusisitiza kuwa, Elimu ndio njia pekee ya kuwaletea maendeleo wakazi wa Mkoa huo,kutokana na mkoa huo kukosa Umeme wa kuhaminika na kuwa na barabara mbovu. Msisitizo wa kauli hiyo aliutoa kwa kufananisha ukuaji wa kasi wa uchumi wa Singapore na udodoraji wa maendeleo ya mkoa huo na Tanzania kwa ujumla.
Kauli hii ina utata mkubwa kwani elimu pekee haiwezi kuleta maendeleo yoyote iwapo njia zingine za kuleta maendeleo zitakuwa zimebanwa kwa wananchi. Mkoa wa Ruvuma unasifika kwa kuzalisha Mahindi, Kahawa, Tumbaku,Alizeti na mazao mengine. Kabla ya mwaka 1984, usafiri wa kwenda huko ulitegemea zaidi njia ya anga (ATC).Usafiri wa barabara ulikuwa ni wa usumbufu mkubwa na uliweza kuchukua muda mrefu kufika mkoani. Kufunguliwa kwa barabara ya Makambako - Songea katika kiwango cha lami, kulitoa fursa kubwa kwa mkoa huo kuvuma katika uzalishaji wa Mahindi. Barabara hii haikuja kutokana na elimu ya waakazi wa huko bali ni kutokana na umuhimu mkubwa wa taifa kupata Mahindi na Kahawa toka mkoani huko.
Mkoa wa Ruvuma kwa miaka mingi umekuwa ukitegemea umeme wa nguvu ya jenereta, ambao licha ya kuwa ni ghali kuuendesha, upatakanaji wake umekuwa ni wa kimgao kwa zaidi ya miaka ishirini sasa. Sasa hapa sijui elimu ya aina gani inatakiwa ili mkoa huo uunganishwe kwenye gridi ya taifa, ambayo inapita katika mikoa ya jirani zake.
Nimeshindwa kuelewa kauli ya Nahodha, kati ya kuwa na elimu na uwewezeshaji wa miundo mbinu na uchumi wa mkoa husika. Kwa mfano majumba ya michenzani huko Zenj hayakujengwa kwa kuwa waakazi wa zenj wote walikuwa ni wajuzi wa ujenzi. Yalijengwa kwa sababu uchumi wa Zenj kipindi hicho ulikuwa unaruhusu, na viongozi kwa kushirikiana na wananchi waliona upo umuhimu wa kufanya hivyo.
Kwa mkoa wa Ruvuma kuwaambia kuwa tatizo lao la umeme litatatuka kwa kuwa na elimu na sawa na kuwaondoa njiani tu...
Posted by Kibunango at 16:06 4 comments
Tuesday 21 August 2007
Umbeya Wenye Manufaa...
Hatua ya mradi wa Usimamizi wa Uhifadhi na Mazingira ya Ukanda wa Pwani "MACEMP" kanda ya Zenj kuanzisha mpango wa kuwafanya wavuvi kuwaripoti kwa siri wavuvi haramu ni mzuri kwa lengo la kuwajua wavuvi haramu. Hatua hii imechukuliwa ili kudhibiti uvuvi haramu ambao kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakiharibu mazingira ya baharini, pamoja na kuhatarisha maisha ya viumbe wa baharani.
Lengo kubwa la mradi huo ni kuhifadhi na kutunza mazingira ya pwani kwa kuondoa umaskini wa wavuvi. Malengo yao kwa kiasi fulani yamefanikiwa kupitia kwa kamati mbalimbali za wavuvi katika kisiwa hicho. Mradi huo umeshatoa boti,ndege,mikopo na nyavu kwa kamati mbalimbali ili kuondoa tatizo la uvuvi haramu huku ikikuza kipato cha wavuvi hao.
Hata hivyo pamoja na utoaji wa vifaa hivyo, tatizo la uvuvi haramu limekuwa likiendelea. Kuendelea kwa tatizo hilo kwa upande mwingine ni kuonyesha kuwa mradi huo bado kuwafikia wadau wote katika sekta ya uvuvi. Zaidi kuna tatizo ndani ya kamati za uvuvi ambao wamelalamikiwa na mradi kwa kuvujisha siri za mikakati ya kudhibiti uvuvi haramu.
Mradi huu ili kuwa endelevu unapaswa kuangalia tena malengo yake, na njia ambazo wanatumia kuwafikia wadau wake. ushirikishwaji wa kamati hizo za uvuvi na wavuvi wenyewe. Iwapo mojawapo wa malengo ni kuondoa umaskini wa wavuvi, hapana shaka basi wawatafutie au kuwaelekeza jinsi ya kupata soko la uvuvi wao(soko la ndani na nje), uhifadhi endelevu wa maeneo yanayotumika kwa uvuvi, maana na athari za uvuvi haramu.
Kutoa vifaa pekee sio njia ya kuweza kufanikisha kuondoa uvuvi haramu na hata umaskini wa wavuvi hao.
Ipo mifano mingi ya miradi ambayo ilipewa vifaa vingi kwa miradi hiyo lakini ikashindwa kuendelea na kuishia kufa baada ya muda mfupi. Hii ilitokana na wadau kutojiona kuwa wapo ndani ya miradi hiyo, na kujenga tabia kuwa maendeleo ya miradi hiyo sio yao bali ni ya serikali au watoa miradi hiyo.
Iwapo mradi wa MACEMP watataka mradi huu uwe endelevu, inawabidi kuangalia ni njia gani ambayo wataweza kuitumia kuhakikisha kuwa wadau wao wanajua umuhimu wa mazingira ya bahari ambalo ndio shamba lao la kuwaingizia kipato. Inawabidi wawafikie hadi wale wavuvi wa chini kabisa,zaidi ya kuishia kwenye kamati na wale wavuvi wanaojulikana huko vijijini. Zaidi ya kuwafikia itawabidi kuwapa elimu tosha ambayo itawafanya wathamini na kutambua umuhimu wa mradi huo kuwa upo kwa ajili ya kuwaondolea umaskini huku mazingira ya bahari na viumbe vyake yakiwa salama.
Posted by Kibunango at 13:04 0 comments