Wednesday, 3 September 2008
Saturday, 30 August 2008
Zenj yakaribia kuanza kusahau Metakelfin, Chloroquine.....
Akiwa katika ziara yake huko USA, Prez wa TZ Jakaya Mrisho Kikwete, akimshukuru Prez G. W Bush, alisema kuwa huko Zenj wapo karibu kabisa kutokomeza ugonjwa wa malaria. Aliendelea kwa kusema pale sipitali ya Mnazi Mmoja kesi za malaria zimepungua kwa kasi toka asilimia 30 hadi asilimia 1.
Mpaka leo hii Malaria ndio ugonjwa unaouwa watu wengi duniani. Kila mwaka zaidi ya watu milioni moja hufariki kutokana na ugonjwa huu. Hivyo juhudi zozote za kuondfoa ugonjwa huu hazipaswi kupitwa bila kuungwa mkono na kama sio kuzipongeza.
Zenj kwa miaka mingi kupitia misaada mbalimbali imekuwa ikijitahidi kuangamiza mazalio ya mbu ambao husababisha malaria. Hali ya hewa ya visiwa hivyo ni nzuri sana kwa mbu wengi kuzaliana na hivyo kusababisha kuwepo kwa malaria. Njia iliyokuwa ikitumika ni kunyunyuzia dawa za kuangamiza mazalio ya mbu katika kila kona ya mji wa zanzibar, toka mji mkongwe hadi ng´ambo, vita hivyo vya kuangamiza mazalio ya mbu ilibaki kidogo kufanikiwa na ilikuwa ni katika ile miaka ya sabini, hadi hivyo haikuweza kufanikiwa. Kurudi kwa mradi huu katika miaka ya hivi karibuni kulitoa tena faraja kwa wengi katika vita hivi.
Malaria na hasa vijidudu visababishao ugomjwa huu hatari kabisa wamekuwa wajanja na kuendelea kubadilika badilika na kushindana na kinda pamoja na dawa za kutibu ugonjwa huu. Kwangu mimi kesi ya kwanza kabisa ya malaria ilinipata kisiwani Zenj karibu miaka ishirini na tano iliyopita. Dozi ya kwanza kupewa ilikuwa ni Chloroquine, haikuweza kupambana na malaria yangu, baada ya wiki mbili bila mafanikio nilipatiwa dozi nyingine ya Quinine ambayo niliitumia kwa kipindi kingine cha wiki mbili na ilifanikiwa kunitibu. Miaka kumi baadae nikapata tena malaria nikiwa huko huko visiwani,dozi ya kwanza kupewa ilikuwa ni Metakelfin, baada ya wiki vidudu vya malaria vilikuwa bado vikitamba, dr. akanipa Phansider nayo ikashindwa kufanya kazi tena baada ya kuirudia katika wiki mbili mfulurizo. Mwishoe nikaambia nijaribu Halfan.. hapo nikapona
Tatizo la malaria katika nchi za Afrika kwa upande mwingine limefungua mlango wa watengenezaji wa madawa yasio pimwa madhara yake kwa binadamu, na kuuuzwa kwetu Afrika... kwa kisingizio kuwa dawa hizo ni za bei nafuu. Kila kukicha kunatangazwa dawa mpya za kutibu malaria na nyingi kati ya hizo huwa zina side effect kubwa mno kwa mtumiaji.
Vyandarua kwa upande mmoja zimesaidia sana katika vita hivi, ingawa sio wananchi wengi wenye uwezo wa kumudu kununua vyandarua, lakini mchango wake ni muhimu sana . Hili la kuangamiza mazalio ya mbu ndio la msingi. Na iwapo takwimu za ugonjwa huu zinaanza kushuka katika zahanati na sipitalini ni dalili nzuri kuwa kuna mafanikio. Cha msingi ni kwa wananchi wote kuunga mkono juhudi hizi ili kutokomeza kabisa ugomjwa huu wa malaria.
Habari ndio hiyo...
Posted by
Kibunango
at
02:53
0
comments
Labels: Chloroquine, George W. Bush, Jakaya Kikwete, malaria, Quinine, Zanzibar
Friday, 29 August 2008
Mwezi wa gharama wakaribia huko Zenj...
Unapokaribia mwezi mtukufu wa Ramadhani, Jiji la zenj hujaa pilikapilika nyingi mno, ni rahisi sana kutofautisha jinsi watu wanavyoishi kabla ya mwezi huo kwani kila mtu huwa kwenye pilika za hali ya juu, tofauti kabisa na miezi mengine yoyote katika mwaka.
Kijana mmoja aliwahi kunilalamikia kuwa ingependeza kama kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani ikawa kama fainali za kombe la dunia kutokea mara moja kwa miaka minne tena katika nchi tofauti. Akiwa na maana iwapo itakuwa zamu ya Tanzania kufunga mwaka huu nchi zingine hazitofunga mpaka zamu yao ikifika....! Sikupata picha kamili ingekuaje kwa nchi zaidi ya mia mbili duniani humu.. Mawazo kama haya uzaliwa kichwani mwa mtu kutokana na majukumu mengi katika mwezi huo.
Kabla ya mwezi kufika wengi hupata mialiko ya kuhudhuria shughuli za arusi, hii yote ni katika kujiandaa na mfungo, kwani wengi hupenda kufuturu majumbani mwao, hivyo vijana wengi hupenda kufunga ndoa katika kipindi kama hichi ili mradi tu awe na uhakika wa kupata futari murua akiwa kwake.
Hali halisi ya Zenj na hasa katika kuandaa futari husababisha ugumu mkubwa katika mwezi huu. Bei za bidhaa hupanda maradufu hivyo kuwa usumbufu mkubwa kwa waakazi wengi wa kipato cha kati visiwani hapo. Ikiwa bado siku kadhaa kabla mwezi huo kuanza bei ya nyama kwa kilo sasa ni zaidi ya sh. 5,000 huu ni mzigo mkubwa. Ikumbukwe bidhaa za vyakula kisiwani humo nyingi hutoka Bara na Pemba, hata hivyo uonekana kama havitoshi pamoja na ukubwa wa gharama.
Sina hakika kama kisiwa cha pili bado wataendeleza mgomo wao wa kutopeleka vyakula huko Zenj, baada ya muafaka kurudishwa tena mezani, na sina hakika hali itakuaje baada ya kasheshe za karibu miezi mitatu kuhusu Zenj kama nchi zitaathiri vipi mfungo wa mwaka huu. Kawaida pamoja na rais wa Zenj kutembelea kwenye markiti akiwaomba wauzaji kupunguza bei, bei hubaki palepale. Safari hii rais atavuka hatua ya kwenda markiti, kwani itabidi kuwashawishi waletaji bidhaa kufanya hivyo na kuweka siasa kando katika mwezi huu.
Ikumbukwe kuwa wananchi hao hujiandaa kwa muda wa miezi kumi kuja kufunga kwa mwezi mmoja, kwani bila ya kujiandaa na kujiwekea akiba unaweza kuja kuumbuka katika kutafuta futari hivyo kuufanya mfungo kuwa mgumu zaidi. Zaidi ya wao wenyewe kujiandaa, ndugu wengi waishio nje ya Zenj na hasa nje ya Afrika wamekuwa mstari wa mbele kusaidia kupunguza makali ya mwezi huu, kwa kujaza wazenj wengi katika ofisi za west union. Kwani pamoja na kujiandaa na futari pia ni mwanzo wa maandalizi ya sikukuu ya Idd ambayo usheherekewa kwa muda wa siku nne mfululizo. Sherehe hizo ni kubwa sana hasa kwa watoto ambao uwakera wazazi wao kwa kudai nguo mpya na maridadi, toys na kadhia zingine ziendanazo na sherehe hizo.
Mie binafsi napenda kuwatakia Wafungaji wote Mfungo mwema....
Posted by
Kibunango
at
02:49
0
comments
Labels: Idd el fitri, mwezi wa ramadhani, Zanzibar
Sunday, 27 July 2008
Zenj imejaa tele Bara

Hivi karibuni nilitembelea katika Jiji la Mwanza na kubahatika kukutana na bango hili, nilijaribu bila mafanikio kuitafita ofisi hiyo ya Bima ambayo ni mojawapo wa Ofisi zinazojiendesha zenyewe visiwani Zenj. Hapana shaka pamoja na kero zinazozungumziwa Shirika hili linafaidi Muungano kwa kuweza kujitanua hadi Jijini Mwanza.
Pengine Mashirika makubwa huko Zenj, ukiondoa Shirika la magari ambalo limepigwa stop kwa namba zake za magari kutumika huko Bara zikafuata mfano wa Shirika la Bima. Asasi zingine ambazo zinaweza kujitatumua huko Bara ni kama asasi ya jeshi la kujenga uchumi, wao wanaweza kuingia katika masuala ya ulinzi, kwani ni soko ambalo linakuwa kwa kasi... Jamaa wa Zenj state engineering ambao pamoja na uwezo wa kujenga nyumba ndani ya siku saba wameendelea kudorora kama sio kufa kibudu kwa kukosa kazi huko zenji, wanayo nafasi nzuri ya kufufuka iwapo wataweza kufuata nyayo za Zantel na Shirika la Bima Zenj
Posted by
Kibunango
at
01:27
0
comments
Friday, 8 February 2008
Lowassa Ajiwekea Rekodi Zake...
Siku ya jana imeingia katika kumbukumbu za serikali na maelfu ya wananchi wa Tz na wengine wenye uhusiano na Tz kwa namna moja ama nyingine.
Katika kuangalia angalia habari ya Lowassa nimekuja kufahamu kuwa ndie Waziri Mkuu wa kwanza kujiuzuru kutokana na tuhumu ambazo nimemgusa moja kwa moja tokea mwaka 1961. Hii ni rekodi kwake na rekodi ya kumbukumbu kwa viongozi wa ngazi za juu ambao kwa namna moja ama nyingine walijiuzuru, pasipo kuwa na tuhumu zinazowakuga wao Binafsi...
Kama vile haitoshi, Bw. Lowassa ameweka rekodi nyingine mpya ya kuwa kiongozi wa juu kabisa kujiuzuru huku akitizamwa na kusikilizwa na maelfu ya Watanzania kupitia Television ya Taifa (TVT). Rekodi nyingine ambayo ameiweka hapo jana ni kujiuzuru mbele ya Bi. Lowassa. Kwa ufupi Bw. Lowassa amejiwekea rekodi kama tatu hivi katika kipindi kifupi kabisa katika historia ya kujiuzuru kwa viongozi hapo Tz.
Mbaya zaidi, ni kuweka rekodi ya kiongozi wa kwanza kujiuzuru muda mfupi kabla ya ziara ya Prezedent Bush, ambaye anatoka huko kulikosababisha Bw. huyo kujiuzuru. Pichani hapo juu ni picha ambayo inaonyesha mapenzi yake na nchi ya Prez. Bush, ambapo sasa anaweza kumwona kwa kupanga foleni kama wananchi wa kawaida.
Posted by
Kibunango
at
13:05
7
comments
Sunday, 20 January 2008
Friday, 18 January 2008
Mambo ya Mapinduzi....
Tukiwa bado tunasheherekea Mapinduzi ya Zenj, nimeona bora leo tujikumbushe baadhi ya misukosuko ya wakati ule wa mapinduzi........
Posted by
Kibunango
at
22:45
0
comments
Monday, 14 January 2008
Wazenj na Mechi za Bure...
Tangu kuchukua nafasi ya Ukurugenzi wa wa timu ya Miembeni, Amani Makungu amekuwa akitoa ofa kadhaa kwa washabiki ya soka visiwani humo kwenda kuona mechi bure. Miembeni ni mojawapo ya timu kongwe visiwani, ambayo imewahi kuwa na mafanikio makubwa kisoka miaka ya nyuma, kabla ya kudorora na kupotea katika ramani ya soka hasa kipindi cha ufadhili cha miaka ya tisini.
Timu hiyo ambayo ipo kwenye kitongoji cha Miembeni ambacho kinajulikana sana visiwani humo kwa makasheshe, ilitwaa ubingwa wa visiwa hivyo mara ya mwisho yapata miaka ishirini(1987). Mwaka jana imefanikiwa tena kuchukua ubingwa wa ligi visiwani humo chini ya ukurugenzi wa A. Makungu na kocha Suleiman Mahmoud Jabri.
Ufadhili wa Mkurugenzi huyu umewawezesha wapenda soka na washabiki wengi wa timu hiyo kuweza kuona mechi kubwa ya klabu hiyo bila ya viingilio. Mechi yakaribuni ya bure ni ile ya kombe la mapinduzi ambapo Miembeni iliweza kutwaa kombe hilo baada ya kuifunga timu ya Polisi kwa mabao 2-1. Mechi hiyo ya dezo ilihidhuriwa pia na Mh. Aman Karume Rais Zanzibar.
Wengi wamenufaika na hili, lakini ni vema vilevile kuangalia nini athari zake kwa soka la visiwa hivyo. Baada ya wadhafili wakubwa kujitoa kugharamia timu kubwa huko visiwani, soka la visiwani lilianguka sana, kuanzia katika mechi za ndani hadi za kimataifa. Ukiangalia nyuma kidogo kama miaka kumi iliyopita hasa katika kipindi cha miaka ya 1996-1998, kulikuwa na upinzani mkubwa wa vilabu kutokana na utajili wa wafadhili wao. Timu ambazo zilikuwa zikivuma kipindi hicho ni Mlandege, Malindi na Shangani, ambazo zote zilikuwa chini ya ufadhili wa wafanyabiashara. Timu kama ya Malindi iliweza hata kusajili wachezaji toka Ulaya ya Mashariki na Afrika vilevile. Klabu kama Miembeni, Kikwajuni na Small Simba ambazo hazikuwa na wafadhili ziliporomoka vibaya katika kiwango cha soka visiwani humo.
Lakini nini kilitokea baada ya wafadhili kujitoa kwenye klabu hizo? Ni kufanya vibay kwa timu hizo, kuwepo na migogoro na kadhia zingine. Sasa klabu zinazomilikiwa na asasi za serikali zikanza kuibuka upya. Timu kama KMKM ambayo ilikuwa tishio katika miaka ya 80 ikarudi tena, huku timu ya Polisi ikiibuka na kuchukua ubingwa wa Zenj na kujiwekea historia yake. Mafanikio ya kablu hizi ni kutokana na wachezaji wake kuwa ni waajiliwa wa asasi hizo.
Miembeni inawapasa kutofumba macho katika suala la kuona timu hiyo inabaki kung'ara kama zamani. Ni wajibu wa kila mwanachama, mpenzi na shabiki wa klabu hiyo kukuna kichwa ni kwa namna gani anaweza kuchangia kuona timu hiyo inakuwa na maendeleo endelevu, badala ya kuendelea kumtazama mtu mmoja akifanya kila kitu kwa klabu hiyo kongwe visiwani. Matokea ya ufadhili wa mtu mmoja/mfanyabiashara yapo wazi kwa kablu kadhaa za visiwani humo. Hivyo ni vema kujifunza kutokana na makosa yaliyofanyika katika kablu hizo. Huu usiwe muda wa kuchekelea kuingia uwanjani bure, bali uwe muda wa kuangalia ni kwa vipi timu hiyo itaweza kukaa katika chati ya juu na kufanikiwa kisoka bila ya kutegemea ofa.
Posted by
Kibunango
at
11:47
1 comments
Saturday, 12 January 2008
Leo ni Miaka 44 ya Mapinduzi ya Zenj
Kila la heri kwa wanamapinduzi wote wa Visiwa vya Zenj, hali kadhalika kwa wasomaji wote wa blog hii...
Mapinduzi Daima...
Katika moja ya vituko vilivyotokea katika shehere za mwanzo za kusherherekea Mapinduzi ya Zenj ni pale Marehemu A. Karume alipokuwa akitoa hotuba yake ambayo ilikuwa ikielezea mafanikio na faida za Mapinduzi hayo. Kwa sauti yake nzito sawa na kilo kadhaa za Nyati, ambayo kwa upande fulani iliwafanya wasikilizaji wake kuwa na kauoga fulani, alitamba kuwa serikali ya mapinduzi (wakati ule) ina fedha nyingi za kigeni(us dollar)zaidi ya idadi ya waakazi wa visiwa hivyo. Aliendelea kwa kusema kuwa fedha hizo ni nyingi kiasi kwa anaweza kumpatia kila mwananchi dola mia za kimarekani na bado fedha ikabaki.
Kijana mmoja kiasi cha miaka kumi na mbili hivi, alinyosha mkono ili aweze kuuliza swali,Wazee waliokuwa karibu yake walijaribu kumzuia kijana huyo kutonyosha mkono. Purukushani hizo zilivuta idadi kubwa ya watu kutazama upande wao, badala ya kuendelea kusikiliza hotuba. Hali hii ilimfanya Marehemu Karume kumruhusu kijana huyo aulize swali lake. Huku akijiamini sana kijana huyo aliuliza hivi..
"Mhe. mimi naomba kupatiwa dola zangu mia sasa hivi..."
Posted by
Kibunango
at
15:46
0
comments
Friday, 11 January 2008
Wazenj na Kuzamia Ulaya
Kwa miaka mingi kumekuwepo na njia mbalimbali zilizotumiwa na vijana kwenda kutafuta kile wanachodai ni maisha bora. Njia ambazo zilipata umaarufu mkubwa ni ile ya kuzamia kwenye meli.Hii ilikuwa ni katika ile miaka ya themanini ambapo soko la ubaharia lilikuwa kubwa kwa vijana wa kiafrika. Vijana wa Zenj nao hawakuwa nyuma katika hili, wengi waliacha shule na kukimbilia kuzamia meli kwa lengo la kufika ulaya.
Mwishoni wa miaka ya themanini na mwanzoni miaka ya tisini, njia ya kwenda ulaya ilibadilika toka kuzamia meli na kupanda pipa (ndege). Hamu ya kwenda ulaya ilizidi kuwa kubwa mno miongoni wa vijana, na wengine walidiriki hata kuteka ndege(ATC)ili tu waweze kufika huko ulaya. Zaidi wengi waliweza kutumia njia nyingi za kulaghai familia zao au kuiba ili tu waweze kufika huko Ulaya.
Miaka ya tisini, wasomi wa kizenj nao wakaingia katika anga ya kuzamia huko Ulaya na Marekani. Ushawishi mkubwa ulitokana na wingi wa vijana kukimbilia ulaya na hasa Uingereza kwa madai ya ukimbizi kutokana na mfumo wa vyama vingi. Wasomi wengi ambao walibahatika kusomeshwa na SMZ asilimia kubwa wameamua kutorudi tena Zenj na sasa wanaendelea na kutafuta maisha yao huko Ulaya na Marekani. Katika kundi hili wapo pia wale walioacha kazi zao muhimu katika SMZ na mashirika ya SMZ.
Katika karne hii mpya imeibuka njia nyingine ya kuzamia huko ulaya, hii ipo katika uwanja wa michezo na utamaduni. Baada ya mwanamasumbi wa Tanzania Bara kuzamia huko Australia katika michuano ya jumuiya ya madola mwaka 2006, wachezaji wawili wa Zenj Heroes nao waliingia mitini, hii ilikuwa ni mwaka 2007. Mwaka huu nao imeripotiwa kuwa wasanii wawili nao wameingia mitini baada ya kumaliza masomo yao huko nchini Norway.
Kwa ufupi hizo ni njia mbalimbali ambazo wazenj wameona ndio nzuri kabisa ili kuweza kufika huko ulaya. Zaidi kumekuwepo na mafanikio katika ngazi ya kifamilia kwa baadhi ya wazenj waliokimbilia huko ulaya. Wengine wamekutana na maadhibu makubwa ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa nchi yao, kiasi kwamba kwa sasa wanaweza kuja nchini mwao kwa kuomba viza. Wapo ambao wametekwa na mambo ya huko ulaya ambayo hayana faida yoyote kwao zaidi ya mashaka makubwa ya afya zao. Hawa ni wale waliojiingiza katika kutumia madawa ya kulevya na ukahaba.Wapo vile vile wauzaji wa madawa ya kulevya ambao wanaendelea kuwaangamiza wenzao watumiayo madawa hayo.
Posted by
Kibunango
at
13:41
0
comments
Monday, 31 December 2007
Heri ya Mwaka Mpya
Napenda kuchukua nafasi hii adhimu kuwatikia kila la heri katika kuukaribisha mwaka mpya wa 2008. Mwaka huu tumeona mengi na kukutana na mwengi, yakiwamo ambayo tuliyapenda na ambayo hatokujapenda. Ni vema kuendelea kujaenzi yale yote ambayo tumeweza kujifunza katika mwaka huu. Na ni bora zaidi kuangalia kwa kina kwa yale yote ambayo hatukuweza kuyatekeleza katika mwaka huu, ili tuweze kuyatekeleza katika mwaka ujao.
Zaidi tushereheke kwa amani huku tukiweka mikakati mizuri kwa mwaka ujao.
Posted by
Kibunango
at
13:05
0
comments


