Madeleine wa Zenj
Wengi wetu sasa tunajua kutoweka kwa Madeleine, mtoto wa miaka minne, raia wa Uingereza aliyetoroshwa huko Ureno yapata siku kumi na sita sasa. Vyombo vya habari na hasa vya hapa UK vimekuwa vikitoa maendeleo ya sakata hilo katika kila habari zao. Hivyo kuweza kuwafikia watu wengi kadiri iwezekanavyo. Leo wakati Fainali ya Kombe la FA, kati ya Man Utd na Chelsea, video ya dakika nne ya Madeleine inategemewa kuonyeshwa.Hivyo kuweza kutazamwa na watu zaidi ya nusu bilioni duniani kote.
Huko Zenj kuna mtoto wa kike wa miaka kumi na sita ameripotiwa kutoroshwa na mwalimu wake yapata miezi mitatu sasa. Jeshi la polisi visiwani humo limeomba kusaidiwa na jeshi la polisi la kimataifa(interpol) katika kumtafuta mtoto ambae jina lake ni Maryam Farid Said.
Tofauti ya Maryam na Madeleine ni kubwa sana, Madeleine ni mtoto mdogo sana asiejua hili na lile, wakati Maryam ni msichana mkubwa ambae anajua nini anafanya. Cha kusisimua zaidi ni kuwa Maryam hii ni mara yake ya pili kutoroshwa na wanaume.
Msichana huyo ambae alikuwa ni mwanafunzi wa shule ya binafsi ya bweni huko Bububu Zanzibar ana undugu na Rais wa Tanzania Jakaya M. Kikwete hivyo kuweka utoroshwaji wake kuwa wa mvuto zaidi. Polisi wa visiwani hapo wanashuku kuwa mtoto huyo atakuwa ametoroshwa na mwalimu wake ambae ni raia wa Uganda.
Iwapo mtoto huyo akipatikana, wazazi wake ambao sasa wanamtafuta, itabidi wamkalishe kikao mtoto huyo, kwani hii ni mara ya pili kutoroshwa hivyo kujenga hofu juu ya tabia yake kwa ujumla. Hapana shaka kuwa mtoto huyo anashirikiana na hao wanao mtorosha hivyo kufanya utafutaji wake kuwa mgumu zaidi. Zaidi nawatakia kila la heri Wazazi wa mtoto huyo katika jitihada za kumtafuta mwanao. Hali kadhalika wanachi ambao kwa namna moja ama nyingine ambao watakuwa na habari yoyote ya kuweza kupatika kwa mshichana huyo watoe ushirikiano wao kwa kutoa taarifa katika vyombo husika.