Sunday, 19 August 2007

TV Zanzibar(TVZ): Jionee mwenyewe walivyochoka

Pamoja na kushikilia rekodi ya kuwa kituo cha kwanza cha television ya rangi katika Afrika ya Mashariki kama sio Afrika, Television hiyo imekuwa ikirudi nyuma kimaendeleo kila kukicha. Sababu za kuanguka kimaendeleo zinajulikana sana, kwani zimekuwa zikisikika kila siku masikioni mwetu, toka kwa Viongozi wa Kisiasa hadi kwa Watendaji wa kituo hicho.

Lengo la bandiko hili si kuzungumzia uchakavu wa Majengo au vyombo vya kurushia matangazo ya tv hiyo, bali ni kuzungumzia muundo wa web site yao, ambayo umeniacha hoi bin taabani.

Tovuti ya kituo hicho kikongwe unakatisha tamaa, na haina uhusiano wowote wa moja kwa moja na shughuli za kila siku za kituo hicho. Zaidi Tovuti hiyo ni kama imewekwa kuhifadhi baadhi ya hotuba za Rais na Waziri kiongozi wa Zenj. Pengine ingependeza zaidi iwapo tovuti hiyo ingekuwa ni ya Ikulu au ya Ofisi ya WK!

Sijui ni kazi ya Mkurugenzi au Afisa Uhusiano au Mwangalizi wa ofisi kusimamia update za tovuti hiyo. Kwa yoyote ambae anahusika basi ameshindwa kabisa kuelewa ni kwa nini TV huwa na tovuti, au ndio hadithi ile ile ya vyombo vya SMZ kujipendekeza zaidi kwenye Ofisi za Wakubwa wao, na kusahu kushughulikia maendeleo ya Ofisi zao!

Kwa ufupi ni aibu kubwa na ni kituko kikubwa kama si kioja kwa TVZ kuiweka hewani tovuti yao. Kama walikuwa hawajawa tayali kuweka tovuti, wangeweza tu kushikiria domain yao bila ya kuirusha hewani kitu ambacho hakina uhusiano wowote na shughuli zao za kiutendaji, hata historia yao. Zaidi hiyo Elimu kwa Televisheni naona bado kufikiwa au kufanyiwa kazi

Wednesday, 15 August 2007

Mbinu za Kizenj za Kusafirisha Mizigo...



Moja ya mambo niliyo yaona huko UK ni jinsi wazenj wanavyojitahidi kusafirisha malundo ya vitu vilivyotumika toka UK kwenda Zenj... Mazagazaga hayo ni kuanzia mafriji, mavideo(VHS), maprinter, mamonitor, makomputer, majiko ya umeme /gasi mabafu, vyoo, n.k.




Makontena ya size ya futi 40 ndio maalufu katika kusafirishia mazagazaga hayo.. ambayo mengine yapo katika hali mbaya sana kutumika zaidi ya kufaa kwa kutupwa tu.



Leo hii tuangalie jinsi ya kusafirisha magari matano katika kontena la futi 40......






















Wednesday, 8 August 2007

Safarini Suomi...

Baada ya kuona Vituko kibao vya wazenj hapa Uk... takribani kwa miezi minne sasa, Nageuza safari na kurudi kijiweni huku nikiwa na rundo la vituko vya wazenj hapa uk... tokea wazungu wa unga, hadi vitangi, wasomi na wafanyabiashara, wazazi hadi wajane... ili mradi ni vituko kede kede.. nikipata nafasi nitakuwa nawapasha baadhi ya vituko vyao...

Thursday, 14 June 2007

Mahakama Kuu ni Kimeo....

Nimewahi kuandika kuhusu mashaka makubwa ya mahakama za zenj katika mabandiko yaliyopita, leo hii kumeibuka kadhia nyingine ambayo hapana shaka ipo kwa muda mrefu tu huko zenj..

Imeripotiwa kuwa mahakama za zenj, hasa Mahakama Kuu haina majaji wa kutosha hivyo kukosa hadhi ya kuitwa Mahakama Kuu kwa mujibu wa katiba ya visiwa hivyo. Tatizo la Majaji huko visiwani lipo kwa muda mrefu sana, ingawa kuna wakati smz ilijitia kifua mbele kwa kukodisha majaji toka nje ya visiwa hivyo(Mapopo).

Kwa mwananchi wa kawaida hawezi kuamini kuwa Visiwa hivyo havina majaji, kwani wao mtu yoyote afanyae kazi mahakamani basi ni jaji, kama ilivyokuwa katika hospitali zao kwa wafanyakazi wote huitwa ni madokta.

Pengine ujuha huu wa kushindwa kutofautisha mgawanyiko wa ngazi za wafanyakazi, upo ndani ya vibosile wa SMZ kiasi cha kujisahau kuwa hawana Majaji wa kutosha kuendesha kesi lukuki katika Mahakama Kuu. Udhaifu wa mahakama za zenj na hasa katika watendaji wake umekuwa ni gumzo kubwa katika kipindi hiki, wakati kuna fufunu ya uteuzi wa Jaji Mkuu mpya wa Tanzania,

Ukiachana na hayo ambayo yanatia kichefuchefu, Mahakama ya Mkoa wa Mjini Magharibi ina Mahakimu watatu tu, ambao kwa maneno mengine ndio Mahakimu wa Mikoa yote ya Zanzibar! kwani sio siri kuwa sijawahi kusikia Hakimu wa Mikoa mengine minne wakitajwa, licha ya kesi walizohukumu kuripotiwa...! Hao Mahakimu wa wilaya wapo kwa hesabu ya vidole, na wengi wao wapo katika Mahakama za wilaya ya Mjini na ile ya Magharibi... Nasikia huko Pemba kuna mahakama ya Mkoa vilevile, hata hivyo Hakimu wake kutwa yupo Vuga!

SmZ kupitia kwa ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali wanapaswa kuja na suluhisho la kudumu kuhusu kadhia hii, na sio kila siku kuwa ni watetezi wa uchovu wa SMZ. Iwapo wao ndio wanasimamia Mahakama na sheria zake, basi hawana budi kuwa na mipango madhubuti ili kuona kuwa vyombo vya haki visiwani humu vimekamilika kwa mujibu wa sheria na katiba ya visiwa hivyo. Kitendo cha kuwaondoa Wapopo katika Mahakama zetu kilikuwa kizuri kwa manufaa ya watu na uchumi wetu unaodorola, aidha ipo haja basi ya ofisi hiyo kupanda Jahazi hadi bara ili kupata Majaji wenye kujua sheria zetu na maadali ya Mtanzania.