Friday, 11 January 2008

Wazenj na Kuzamia Ulaya

Kwa miaka mingi kumekuwepo na njia mbalimbali zilizotumiwa na vijana kwenda kutafuta kile wanachodai ni maisha bora. Njia ambazo zilipata umaarufu mkubwa ni ile ya kuzamia kwenye meli.Hii ilikuwa ni katika ile miaka ya themanini ambapo soko la ubaharia lilikuwa kubwa kwa vijana wa kiafrika. Vijana wa Zenj nao hawakuwa nyuma katika hili, wengi waliacha shule na kukimbilia kuzamia meli kwa lengo la kufika ulaya.

Mwishoni wa miaka ya themanini na mwanzoni miaka ya tisini, njia ya kwenda ulaya ilibadilika toka kuzamia meli na kupanda pipa (ndege). Hamu ya kwenda ulaya ilizidi kuwa kubwa mno miongoni wa vijana, na wengine walidiriki hata kuteka ndege(ATC)ili tu waweze kufika huko ulaya. Zaidi wengi waliweza kutumia njia nyingi za kulaghai familia zao au kuiba ili tu waweze kufika huko Ulaya.

Miaka ya tisini, wasomi wa kizenj nao wakaingia katika anga ya kuzamia huko Ulaya na Marekani. Ushawishi mkubwa ulitokana na wingi wa vijana kukimbilia ulaya na hasa Uingereza kwa madai ya ukimbizi kutokana na mfumo wa vyama vingi. Wasomi wengi ambao walibahatika kusomeshwa na SMZ asilimia kubwa wameamua kutorudi tena Zenj na sasa wanaendelea na kutafuta maisha yao huko Ulaya na Marekani. Katika kundi hili wapo pia wale walioacha kazi zao muhimu katika SMZ na mashirika ya SMZ.

Katika karne hii mpya imeibuka njia nyingine ya kuzamia huko ulaya, hii ipo katika uwanja wa michezo na utamaduni. Baada ya mwanamasumbi wa Tanzania Bara kuzamia huko Australia katika michuano ya jumuiya ya madola mwaka 2006, wachezaji wawili wa Zenj Heroes nao waliingia mitini, hii ilikuwa ni mwaka 2007. Mwaka huu nao imeripotiwa kuwa wasanii wawili nao wameingia mitini baada ya kumaliza masomo yao huko nchini Norway.

Kwa ufupi hizo ni njia mbalimbali ambazo wazenj wameona ndio nzuri kabisa ili kuweza kufika huko ulaya. Zaidi kumekuwepo na mafanikio katika ngazi ya kifamilia kwa baadhi ya wazenj waliokimbilia huko ulaya. Wengine wamekutana na maadhibu makubwa ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa nchi yao, kiasi kwamba kwa sasa wanaweza kuja nchini mwao kwa kuomba viza. Wapo ambao wametekwa na mambo ya huko ulaya ambayo hayana faida yoyote kwao zaidi ya mashaka makubwa ya afya zao. Hawa ni wale waliojiingiza katika kutumia madawa ya kulevya na ukahaba.Wapo vile vile wauzaji wa madawa ya kulevya ambao wanaendelea kuwaangamiza wenzao watumiayo madawa hayo.

Monday, 31 December 2007

Heri ya Mwaka Mpya

Napenda kuchukua nafasi hii adhimu kuwatikia kila la heri katika kuukaribisha mwaka mpya wa 2008. Mwaka huu tumeona mengi na kukutana na mwengi, yakiwamo ambayo tuliyapenda na ambayo hatokujapenda. Ni vema kuendelea kujaenzi yale yote ambayo tumeweza kujifunza katika mwaka huu. Na ni bora zaidi kuangalia kwa kina kwa yale yote ambayo hatukuweza kuyatekeleza katika mwaka huu, ili tuweze kuyatekeleza katika mwaka ujao.

Zaidi tushereheke kwa amani huku tukiweka mikakati mizuri kwa mwaka ujao.

Monday, 5 November 2007

Safarini South Africa

Wapenzi wa kona hii, napenda kuwapa taarifa kuwa nitakuwa safarini South Africa kwa masuala ya kifamilia. Kwa wapenzi wa blog mliopo South napenda kupiga hodi rasni. Kwa muda wote ambao nitakuwepo South nitaendelea na blog hi kwa kuwapa Uhondo,visa na ujumbe wowote ule kuhusu zenj africa ya kusin,

Monday, 15 October 2007

Leo ni Sikukuu Zenj (15/10/07)

Wananchi wa Zanzibar leo watendelea kuwepo mapumzikoni, katika kusherekea sikukuu ya Idd El Fitri. Hayo yalitangazwa na Mkurugenzi wa Idara ya Utumishi visiwani humo. Kwa kawaida sikukuu hii huwa na mapumziko ya siku mbili rasmi, hata hivyo mwaka huu iliangukia siku ya mapumziko, hivyo pengine SMZ wakaona ni vema na siku ya Jumatatu wananchi wake waendelee kufaidi kusherekea sikukuu.

Visiwani sikukuu za Idd husherekewa kwa muda wa siku nne mfululizo,ambapo siku mbili kati ya hizo huwa ni mapumziko rasmi, na zingine mbili husherekewa baada ya saa za kazi kwisha. Viwanja rasmi hutengwa na Halmashauri za miji kwa ajili ya watu kwenda huko kushereheka, karibu kila aina ya burudani huwepo katika viwanja hivyo. katika viwanja hivyo huwepo na maduka ya kuuza toys,vibanda vya vyakula, vibanda vya kupiga picha, vibanda vya tombola, vibanda vya taarabu, disco na uchekeshaji na vibanda vingine. Kwa Halmashauri hizo ni wakati mzuri wa kukusanya kodi kubwa katika kipindi kifupi zaidi cha ukusanyaji wa kodi. Aidha kwa wananchi ni wakati wa kutumia kwa nguvu katika kipindi kifupi.

Kwa wafanyakazi wa SMZ sherehe hizi hufana zaidi iwapo zitaangukia mwisho wa mwezi, kwani wengi wao hua na uhakika wa kupeleka familia zao katika viwanja hivyo kwa muda wote. Iwapo una familia, mke/wake na watoto, basi hupenda kuwa na nguo mpya kwa siku zote za sikukuu, pesa ya kwenda na kurudi na za kujichana wawepo viwanjani humo.. huku watoto ukiwa ndio wakati wao wa pekee kununua toys wazipendazo. Hivyo kwa mfanyakazi wa SMZ inabidi awe amejinyima sana ili kuweza kufurahisha familia yake.

Kujinyima kwa wafanyakazi hao si kitu rahisi sana kutokana na viwango vya mishahara na hali halisi ya maisha visiwani humo, hii husababisha wasiwe na mipango ya muda mrefu ya kujiandaa na sherehe hizo, zaidi ya kuomba Mungu sherehe hizo ziangukie karibu na mwisho wa mwezi.

Katika ile awamu ambayo wafanyakazi walikuwa wakilipwa mishahara yao katika siku ya arobaini, kulikuwepo na tabia ya wafanyakazi kulipwa nusu msharaha iwapo sikukuu itaangukia katikati ya mwezi. Hii iliwapunguzia machungu ya kusubiri mshahara wa siku ya arobaini na kuweza angalu kuvinjali na familia zao katika viwanja vya sikukuu. Hata hivyo wakati huu nusu mshahara haikutoka na zaidi leo wameambiwa kuwa wapumzike. Kwa upande wa wengi hii ni kero kwao. Iweje upumzike wakati huna hata senti mfukoni. Wengi wanaona bora wangeenda huko kwenye maofisi yao kufanya kazi kuliko kukaa nyumbani pasipo kuwa na kitu. Mbaya zaidi iwapo mfanyakazi ana akaunti ya katika Benki ya Watu wa Zanzibar(PBZ), ina maana kuwa leo hatoweza kutoa fedha zozote, kwani benki itakuwa imefungwa na PBZ hawana ATM...

Hivyo nina imani kuwa pamoja na nia nzuri ya SMZ, kuwapa wafanyakazi siku ya leo kuwa ya mapumziko, sio wengi ambao wamefurahia tangazo hilo. Zaidi limewaweka katika wakati mgumu wa kujibu maswali mengi toka kwenye familia zao.