Wazenj na Kuzamia Ulaya
Kwa miaka mingi kumekuwepo na njia mbalimbali zilizotumiwa na vijana kwenda kutafuta kile wanachodai ni maisha bora. Njia ambazo zilipata umaarufu mkubwa ni ile ya kuzamia kwenye meli.Hii ilikuwa ni katika ile miaka ya themanini ambapo soko la ubaharia lilikuwa kubwa kwa vijana wa kiafrika. Vijana wa Zenj nao hawakuwa nyuma katika hili, wengi waliacha shule na kukimbilia kuzamia meli kwa lengo la kufika ulaya.
Mwishoni wa miaka ya themanini na mwanzoni miaka ya tisini, njia ya kwenda ulaya ilibadilika toka kuzamia meli na kupanda pipa (ndege). Hamu ya kwenda ulaya ilizidi kuwa kubwa mno miongoni wa vijana, na wengine walidiriki hata kuteka ndege(ATC)ili tu waweze kufika huko ulaya. Zaidi wengi waliweza kutumia njia nyingi za kulaghai familia zao au kuiba ili tu waweze kufika huko Ulaya.
Miaka ya tisini, wasomi wa kizenj nao wakaingia katika anga ya kuzamia huko Ulaya na Marekani. Ushawishi mkubwa ulitokana na wingi wa vijana kukimbilia ulaya na hasa Uingereza kwa madai ya ukimbizi kutokana na mfumo wa vyama vingi. Wasomi wengi ambao walibahatika kusomeshwa na SMZ asilimia kubwa wameamua kutorudi tena Zenj na sasa wanaendelea na kutafuta maisha yao huko Ulaya na Marekani. Katika kundi hili wapo pia wale walioacha kazi zao muhimu katika SMZ na mashirika ya SMZ.
Katika karne hii mpya imeibuka njia nyingine ya kuzamia huko ulaya, hii ipo katika uwanja wa michezo na utamaduni. Baada ya mwanamasumbi wa Tanzania Bara kuzamia huko Australia katika michuano ya jumuiya ya madola mwaka 2006, wachezaji wawili wa Zenj Heroes nao waliingia mitini, hii ilikuwa ni mwaka 2007. Mwaka huu nao imeripotiwa kuwa wasanii wawili nao wameingia mitini baada ya kumaliza masomo yao huko nchini Norway.
Kwa ufupi hizo ni njia mbalimbali ambazo wazenj wameona ndio nzuri kabisa ili kuweza kufika huko ulaya. Zaidi kumekuwepo na mafanikio katika ngazi ya kifamilia kwa baadhi ya wazenj waliokimbilia huko ulaya. Wengine wamekutana na maadhibu makubwa ikiwa ni pamoja na kuukana uraia wa nchi yao, kiasi kwamba kwa sasa wanaweza kuja nchini mwao kwa kuomba viza. Wapo ambao wametekwa na mambo ya huko ulaya ambayo hayana faida yoyote kwao zaidi ya mashaka makubwa ya afya zao. Hawa ni wale waliojiingiza katika kutumia madawa ya kulevya na ukahaba.Wapo vile vile wauzaji wa madawa ya kulevya ambao wanaendelea kuwaangamiza wenzao watumiayo madawa hayo.