Tuesday, 8 September 2009

Siku Aman Karume alipomtoa nishai Ali Karume...


Pichani Prezidenti wa Zenj akiweka wazi njia aliyoitumia kumzuia mdogo wake Ali Karume kuchaguliwa kuingia katika kinyang'anyiro cha uprez wa Jamhuri ya Muungano alipotembelea Finland mwezi wa tatu mwaka 2005.

Safari hii Aman Karume atakutana na kimbembe kama hiki, kwani Ali tayali ameshaweka wazi nia yake ya kumrithi, huku Nadhoda akionyesha nia kwa mbali ya kugombea kiti hicho, hivyo kumpa mtihani mkubwa Amani hapo 2010.

Saturday, 5 September 2009

Sunday, 30 August 2009

“SMZ iwache kushabikia na kuendeleza ubaguzi dhidi ya raia”


TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 29 Agosti 2009

“SMZ iwache kushabikia na kuendeleza ubaguzi dhidi ya raia”

Kufuatia taarifa iliyochapishwa jana na gazeti la The Guardian juu ya hatua ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuwalazimisha Wazanzibari wenye asili ya Kingazija kwenda kujisajili rasmi kama raia wa Watanzania, Chama cha Wananchi (CUF) kinatoa tamko lifuatalo:

“Kwanza ni kiwango cha juu cha ubaguzi na upotofu kwa SMZ kuendeleza sera zake za kibaguzi dhidi ya Wazanzibari wa makundi tafauti. Misingi hii ya kibaguzi ilianza kujengwa dhidi ya Wazanzibari wenye asili ya Pemba kwa kuwanyima fursa na haki kadhaa za msingi zikiwemo za kielimu, kiuchumi na kisiasa; na sasa baada ya kwisha kuwabagua Wapemba, SMZ inawageukia Wangazija. Serikali ya kweli ya watu haisimamii ubaguzi na utengano, bali mapenzi baina ya watu wake na mshikamano.

“Pili, kisingizio kinachotolea na SMZ kwamba huko ni kufuata sheria iliyotolewa kwa njia ya Dikrii ya Rais tangu mwanzoni mwa Mapinduzi ya Zanzibar na kwamba eti kwa kuwa hiyo ni sheria ambayo haijafutwa kwa hivyo haijatanguka, ni upotofu mwengine wa hali ya juu. Kwanza ilikuwa ni kosa kwa Rais Abeid Karume kutoa tamko hilo ambalo lilikuja kuwa dikrii, kwani aliingiza ugomvi wake binafsi na baadhi ya Wazanzibari waliokuwa na asili ya Kingazija katika masuala ya utawala na khatima ya wananchi. Pili, inasemwa kuwa Mapinduzi yalifanywa kwa lengo la kuwaunganisha Wazanzibari na kufuta misingi ya kibaguzi; kwa hivyo hiyo ilikuwa ni Dikrii iliyokwenda kinyume na misingi ya Mapinduzi na basi ilikosa uhalali tangu mwanzoni.

“Tatu, inaonekana uongozi wa SMZ hauijui hata hiyo jamii ya Wazanzibari unayoitawala. Haijifunzi ukweli kwamba ni mchanganyiko wa asili, makabila, mataifa na historia tafauti ndio ulioifanya Zanzibar kuwa Zanzibar waliyoipata wao (SMZ) kuitawala. Wanapowabagua watu ambao wameleta mchango mkubwa wa kuijenga Zanzibar kijamii, kielimu, kiutamaduni na kisiasa, inafaa Wazanzibari wajiulize tena na tena juu ya aina ya uongozi uliopo madarakani. Ni lazima serikali hii iwache kushabikia na kuendeleza ubaguzi dhidi ya raia.”

Imetolewa na:

Salim Bimani
Mkurugenzi wa Uenezi na Mahusiano na Umma, CUF

Thursday, 27 August 2009