Tuesday, 12 January 2010

Miaka 46 Gizani




Leo ni sikukuu ya Mapinduzi ambapo yanatimiza miaka 46, tofauti na miaka iliyopita sherehe za mwaka huu zinafanyika gizani. Katika kusherekea sherehe hizo kitaifa zitafanyika kule kwenye matatizo ya muda mrefu ya giza na action za kelele za jenereta.
Kila la heri katika kusherekea mapinduzi

Mapinduzi Daima

Saturday, 2 January 2010

Mapacha Walioungana Wazaliwa Zenji...

Mwanamke mmoja mkazi wa Zanzibar, Farihati Maulid (18) amejifungua watoto pacha wa kiume walioungana.

Mwanamke huyo alijifungua kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Mnazi Mmoja jana saa tatu asubuhi na mapacha hao wako katika chumba cha uangalizi maalumu.

Mkunga wa hospitali hiyo, Halima Habiba Abdallah, na Dk. Mwana Omar ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Uzazi, wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema tukio hilo ni la kwanza kwa muda mrefu katika hospitali hiyo wanaendelea kupata ushauri kutoka kwa wataalamu wengine wa afya.

Pacha hao wana moyo mmoja, na wameunganika kuanzia kwenye kitovu hadi kwenye mfupa wa kidari.

“Tunasubiri wataalamu kufanya uchunguzi zaidi, lakini kwa sababu wana moyo mmoja na wana uzito wa kilo 2.8 itakuwa ngumu kuwatenganisha na kupona, haijulikani ni viungo gani vingine kila mmoja anavyo vya peke yake,” alisema Dk. Omari.

Habari zaidi zinasema mama wa watoto hao ni mkazi wa Mwanyanya, Bububu katika Manispaa ya Zanzibar na mimba hiyo ilikuwa ya kwanza.

Friday, 1 January 2010

Zenjiflava: Mtandao Mpya.....




Mtandao mpya umefunguliwa kwa ajili ya kuleta habari tofauti (muziki, matukio, mitindo, utamaduni, burudani na kadhalika) kutoka Zanzibar na Pemba. www.zenjiflava.com

Kwa wale ambao wanataka kutuma habari zao zinazohusu Zanzibar na Pemba ili ziwekwe kwenye mtandao, naomba mtumie barua pepe hizi: info@zenjiflava.com au zenjiflava@hotmail.com

Kwa wale ambao wanataka kupiga soga (online chat) huku mkicheki habari mbalimbali kwenye tovuti basi mnabidi mjiunge kwanza. Mkiangalia kwenye mtandao, hapo juu kulia mtaona majina ya watu mbalimbali waliojiunga ambao wako LIVE wanapiga soga, ukigonga katika jina basi utaweza kuongea nao.

Thursday, 31 December 2009

Mzee Rashid Mfaume Kawawa Ametutoka....


Rashid Kawawa wa pili toka kushoto.

Waziri Mkuu wa Tanganyika na mpigania huru wa Tanganyika na Muasisi wa Muungano mzee Rashid Mfaume Kawawa amefariki dunia. Habari ambazo zinatiririka taratibu kutoka vyanzo mbalimbali zinadokeza kuwa mzee Kawawa amefariki dunia leo na mpango wa kulitangazia taifa msiba huu mkubwa uko mbioni na wakati wowote kuanzia sasa Rais Jakaya Kikwete atalihabarisha taifa juu ya msiba huu wa kitaifa wa mmoja wa viongozi waliopendwa na waliolitumikia taifa kwa muda mrefu. Mzee Kawawa alikuwa ni swahiba wa karibu zaidi wa baba wa Taifa Mwalimu Julius K. Nyerere.

Mzee Kawawa alizaliwa Mei 27 , 1926 huko Songea kijiji cha Matepwende mkoani Ruvuma. Alianza elimu ya msingi huko Liwale Lindi. Aliendelea na elimu ya kati (middle school) hapo Dar-es-Salaam school ambapo mmojawapo wa wanafunzi wengine ni marehemu mzee Kanyama Chiume mpigania uhuru toka Malawi aliyeishi uhamishoni nchini Tanzania kwa muda mrefu. Wengine katika shule hiyo wakati huo ni pamoja na kina Abdul Sykes, Ali Sykes, Hamza Aziz na Faraji Kilumanga.

Aliendelea na masomo yake huko Tabora Boys kati ya 1951-1956. Alikuwa ni Waziri Mkuu wa Tanganyika mwaka 1962 wakati Mwalimu Nyerere alipoamua kwenda mikoani kujenga chama na kufanya shughuli za kisiasa. Baadaye aliteuliwa tena kuwa Waziri Mkuu mwaka 1972-1977 na akawa miongoni mwa wahamasishaji wakubwa wakati wa vita ya kumng'oa nduli Idi Amin ambapo alitembelea wapiganaji wetu waliokuwa mstari wa mbele kule Uganda. Hii ilimpatia jina la "Simba wa Vita" jina ambalo lilimkaa vyema kwa muda mrefu.

Kabla ya kuingia katika harakati za kupigania Uhuru Mzee Kawawa alikuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa Shirikisho la Wafanyakazi mwaka 1955 ambapo alichaguliwa kuwa Katibu wake Mkuu wa kwanza. Ni katika nafasi hii ndiyo aliweza kuanza kushiriki kwa nguvu zaidi katika harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika akihamasisha wafanyakazi. Kabla ya hapo alikuwa ni Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi wa Serikali.

Februari 1956 Mzee Kawawa aliacha kazi yake ya Shirikisho la Wafanyakazi kutokana na kuwa mwajiriwa wa serikali kitu ambacho kilimkataza kuhusisha na siasa na kuamua kuingia katika harakati za kudai uhuru kupitia TANU. Alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya TANU mwaka 1957, Makamu mwenyekiti wa TANU mwaka 1960.

Mwaka 1964 baada ya Muungano Mzee Kawawa alikuwa ni Makamu wa Pili wa Rais akiwa ni msaidizi wa Rais wa Muungano kwa upande wa mambo ya Bara.
Katika siasa amewahi kushika nafasi mbalimbali ikiwemo ile ya Ukatibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi na Makamu Mwenyekiti wa CCM na amekuwa mjumbe wa kudumu wa Kamati Kuu ya CCM.

Mzee Kawawa alikuwa ni mtoto wa kwanza kati ya watoto nane na mojawapo ya kazi zake za awali ilikuwa ni uchezaji wa filamu za uhamasishaji na akawa ndiye mcheza filamu wa kwanza kiongozi mweusi (lead actor).

Mzee Kawawa alikimbizwa hospitali hapo jana kutokana na hali yake kuwa mbaya na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi; ambapo mapema leo asubuhi alifariki dunia. Mipango ya mazishi inaandaliwa.

Mungu ailaze roho ya Marehemu Pema Peponi,Amin

Source: Jamiiforums