"Kuna Harufu Chafu CCM Zanzibar" - Ameir
Mwanasiasa Mkongwe Zanzibar Ali Ameir Mohamed, amesema wakati umefika kwa viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi kuwachukulia mapema hatua za kimaadili na kinidhamu wanachama,Wawakilishi na Wabunge wa chama hicho wenye mwelekeo hasi.
Ameir ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa CCM Zanzibar na Mbunge wa zamani wa Donge, alisema hayo kupitia mahojiano maalum yaliyofanyika Kijijini kwake huko Donge Mbiji Zanzibar juzi.
Alisema kuwa kuendelea kuwavumilia wanachama wa aina hiyo ni hatari kwa mustakabali wa uhai wa chama hicho akiifananisha hali hiyo ni sawa na mfiwa kufuga maiti ya ndugu yake ndani ya nyumba anayoishi.
“Chama cha siasa ni mkusanyiko wa kundi la watu wanaokubaliana kisera, kiitikadi na kimfumo hivyo anayejitokeza akipingana na masuala hayo hapaswi kubembelezwa au kuonewa muhali”,alisema Ameir ambaye pia amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Tanzania.
Alisema kiongozi, mwanachama, mbunge au Mwakilishi anayepingana na sera ya msingi ya chama chake analazimika kujitoa ili kuonyesha msimamo wa hisia zake.
Ameir anasema anaamini kuwa taratibu za kikanuni na kikatiba ndani ya chama chake zitafutwa ili kusafisha hewa chafu inayoonekana kutanda.
“Kila mwanachama au kiongozi ana wajibu na haki ya kutambua chimbuko la historia ya vyama vya TANU na ASP, muundo wa Muungano na harakati zilizoleta Mapinduzi mwaka 1964, asiyekubaliana na ukweli huo nadhani hatoshi kubaki na kuwa mtetezi wa sera za CCM kwa uhai wake”.Alisikika akisema
Aidha mwanasiasa huyo ambaye ni mmoja kati ya wajumbe walioshiriki kuandaa mchakato wa uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, alieleza kuwa yeye anaamini kuwa taratibu husika kupitia vikao vya katiba vya CCM zitafuatwa.
Ameir alieleza kuwa kumejitokeza baadhi ya wanasiasa Zanzibar wanaojigamba kuwa wao ni waasisi wa TANU na ASP wakati ni wazee wa CCM na kwamba si haki yao kujiita ni wana Mapinduzi kinyume na ukweli ulivyo. Alisema waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, wanafahamika kwa majina yao na kwamba anayejitokeza sasa na kudai yeye ni miongoni mwao, ni sawa na mtu anayejipaka damu ya ng’ombe aliyechinjwa na wengine.
“Wana Mapinduzi wa Zanzibar wamebaki wawili hadi sasa,wote sasa ni wazee, Ramadhani Haji Faki na Hamid Ameir Ali, anayethubutu kunyoosha kidole chake na kujiita muasisi wa Mapinduzi, anajivika kilemba cha ukoka”Alisema Ameir.
Alipinga jina la Hassan Nassor Moyo kuwa miongoni mwa waasisi wa ASP na kuwa mmoja kati ya wanamapinduzi kwamba hakuwemo katika harakati za kukiasisi chama hicho wala hakujua siku ya kufanyika Mapinduzi ya 1964 kwa mujibu wa maelezo ya wazee wenzake.
“Moyo ninamheshimu sana, ni mkubwa kiodogo kwangu kiumri ,alikuwa katika Trade Union, hakuwa mwanasiasa aliyeshiriki kukiasisi chama cha ASP,wenzake wanatueleza hata siku yaliofanyika Mapinduzi ya umma hakuijua”Alisisitiza
Akizungumzia kujitokeza kwa Mzee Moyo anayeonekana kutaka Muungano wa mkataba kinyume na sera ya CCM kinachofuata Serikali mbili chini ya Katiba.
Ameir alisema wajumbe hao kufika kwao ndani ya BLW kunatoka na chama cha siasa hivyo matamshi yao hayapingani na sera hiyo ila wanavutana na mfumo wa chama chao.
‘Mzee Moyo nijuavyo ni mwana Muungano wa kikwelikweli, asili yake upande mmoja ni Ruvuma Tanganyika na upande wa pili hapa Zanzibar, anapobeza Muungano huu unaotokana na matokeo ya Mapinduzi na Uhuru wa nchi zetu, sidhani kama anaamua kuafikiana na misimamo tuliokuwa tukipingana nayo kabla ya 1961 na 1964 ”Alisema Ameir.
Kauli hii inakuja wakati kukiwa na katika kampeni kubwa ya kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano wakishirikiana na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara, (JUMIKI) hali iliyosababisha vurugu za makanisa na baa kuchomwa moto Zanzibar.
Mwinyi Sadallah