Sunday, 14 July 2013

Siasa za Zanzibar: Kasumba Ile Ile, Kwenye Mtungi Mpya!!!

Uzanzibari; Utanganyika ; Utanzania NA MUUNGANO.


Si dhumuni wala sio shabaha ya andiko hili kuleta fananusi au kuja
na fasiri ya mambo matatu hayo niliyo yataja hapo juu.

Sitafanya hivyo kwa sababu ;fasiri halisi ya kikamilifu bado haijapatikana,
fasiri ambayo itaweza kufikia kikomo cha kusema kua "Binaadam fulani na
fulani " - wamekamilika kuwa ni "wataifa fulani";"wajananchi fulani" ,au
"wajaumojafulani " au "Wanamuungano fulani",kwa Watanzania.

Ninasema hivyo kwa sababu "Utaifa Fulani" au "Ujananchi Fulani"
phenomenon hii /kitu hichi hakijapatapo kua kufikia hali ya usimemi /static
kuweza kusema fulani "ameshakamilika kua mtaifa fulani ".Hali kama hiyo
bado hatujaifikia ,ila tu kiserikali na kikawaida mtu huwa mwananchi
wa nchi fulani au "mtaifa wa taifa fulani" kwa misingi ya ukhususiya wake
au kwa ukizazi,uasiliya na uzaliwa wake.

Njia nyingine za ujananchi ni ukubaliko na ujinasibishaji haya yote ni mambo
ambayo yanafugamatana na mmambo ya silka,lugha na utamaduni.

Kwa watu wengine haki za kua raia/uwananchi wanazipata kwa njia za tajinisi.
Hii ni haki ya kuomba uraia baada ya kukamilisha masharti husika kwa mujibu
wa sheria za nchi .

Majina ya Nchi.
Majina haya ya eti Zanzibar,Tanganyika kwa kweli hayana uasilia wala
uthabiti bayana ambao unatokana na watu waasilia wakaazi wa maeneo hayo.
Marehemu Julius Nyerere,ni mmoja miongoni mwa wengi waliowahi kufanya utafiti
wa kina wa majina majina haya ya nchi tofauti kwingi ulimwenguni.

Kuhusu jina Zanzibar au Tanganyika - tukisema ukweli pengine sisi "tulibahatika "
kupewa majina kama hayo kama walivyopeda wale "Watembezi au Wasafiri wa kale
Wavamizi waliotembelea maeneo na ardhi za watu wengine kwa sababu tofauti.

Ninasema "tulibahatika " kwa sababu kuna baadhi ya wenzetu wamepagazwa
majina ya ajabu ajabu ya kijografia tu - kama kwa mfano "South Africa" " Central
African Republic" " South-West Africa " " Western Sahara "au zile nchi ziitwazo
kwa majina ya kiumiliki kama "British Caledonia" ,"French Polynesia".

Kinyume na majina majina hayo yote jina la " Tanzania " ni jina ambalo
limechaguliwa na kukubaliwa na Wananchi wa nchi mbili huru ambazo
zimo kwenye Muungano wetu wa Tanzania .

Dhumuni ya andiko hili ni kusema machache kuhusu yale "Mapendekezo
ya Kamati ya Maridhiano kuhusu Muungano huu na Katiba Mpya".
Mapendekezo hayo yalichapishwa katika ZanzibarYetu tarehe 25/5/20013
wiki moja kabla ya Rasimu ya Katiba Mpya Kutangazwa-Rasmi.

Kwa nini Kamati ya Maridhiano ya Zanzibar iliamua kuchapisha na kuyatangaza
Mapendekezo yake kabla ya kutolewa ile Rasimu ya Katiba Mpya ya Muungano ?

Jee Kamati ya Maridhiano ya Zanzibar ilikuwa na dhamiri za kuandaliya au hata
kuushawishi umma /wananchi wa Zanzibar kwa kadiri fulani kabla ya kuisoma ile
Rasimu ya Katiba Mpya ya Muungano ?

Jee Kamati hiyo ya Maridhiano ,ilikwisha pata fununu fununu kuhusu yaliyokuwemo
ndani ya Rasimu,au Kamati hiyo ilikua inatumiya Uhuru wake wa kujitamka?

Kuhusu Muungano.

(1) Kamati ya Maridhiano inasema kua "Muungano huu umetokana na
Jamhuri mbili kuungana kwa hiyari ".(Tamko lao hili ni jipya).

Hebu tuangalie nyuma wakati wa harakati harakati za misutano ya
kisiasa baina ya wanasiasa wapinzani na wanaounga mfumo wa Muungano.

Wapinzani wa Muungano wanasema kwa ndimi mbili togfauto zenye upotoshi.
Waliyokuwa wakisema hapo kabliya si sawa na haya wayasemayo hivi leo .

Kwa mfano wengi wao walikuwa wakisema kwa khamasa kali kabisa kua:

"Muungano huu haujakuwa wa hiyari na wananchi hawajaulizwa ".
"Muungano wa mabavu baina ya Karume na Nyerere".
"Muungano huu ni tokea za njama za siasa ujasusi za USA".
"Muungano ulikuwa na shabaha ya kuwanyima na kuwapora wananchi wa visiwa
vya Pemba na Unguja kuendeleza siasaza usoshalisti na kuifanya Zanzibar ,kua kama
ni mfano wa Cuba ya Afrika Mashariki".
Wengine kwa kile wakiitacho "utafiti wao " walisema kua eti hat ule ".uasi wa wanajeshi wa Tanganyika
mara tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ndio uliosababisha kufanywa kwa Muungano kwa haraka,
ili kuvunja nguvu za vuguvu la Ukoministi la Afrika Mashariki .

Wapinzani wa Muungano kwa kweli wamekuwa wakitowa sababu nyingi ama za kuupinga na wakati
mwingine huwa wanataka kutowa madai ya kuwepo serikali tatu ,wengine zibaki mbili na wapo hata
wale ambao wanataka kuuvunja Muungano huu.

(2) Kamati ya Maridhiano Zanzibar inatoa madai kua iwekwe bayana katika katiba
mpya kwamba ".. nchi zilizo ungana ni zaidi ya nchi moja/jamhuri au falme".
Na wametowa mifano ya mifumo USA kwa kuwepo neno "States"; USSR kuwepo
neno "Republics"; na UAE kuwepo neno United Arab Emirates.

Mifano hiyo imetolewa ili iwe kama halalisho ya hoja zao za " kuondosha dhana
kwamba Muungano wa Zanzibar na Tanganyika ndio sababu ya "kufutwa kuwepo kwa
bayanisho la wazi la kutambulika kwa nchi mbili hizo kabla ya Muungano.

Mara nyingi mimi hua najiuliza haya yafuatayo.
a) Hivi kweli Zanzibar haina Rais wake aliyechaguliwa na Wazanzibari ?
b) Hivi kweli Zanzibar haina Baraza la Mapinduzi tokea huu Muungano ?
c) Hivi kweli Zanzibar haina Baraza la Wawakilishi tokea Muungano ?
d) Hivi kweli Zanzibar haina serikali yake mbali na ile ya Muungano ?

Baada ya kujiuliza hayo nikajishitukia kuona kwamba vyombo vyote hivyo vya
kitawala vipo huko Zanzibar.Jee vyombo hivyo vilitumika au vinatumika kwa
masilahi ya kulinda na kutetea katiba ya 1964 au hata ile 1977?
Kasoro,Nywengeza,Kero na Malalamiko ikiwa kwa upande wa Tanganyika kutokuwa
na serikali yake yenye mamlaka kamili zilipata kukosolewa ?
Jee katiba mbili hizo zilipatapo kuhalalashwa na vyombo tawala vya nchi mbili hizo ?

Katiba ya 1977 ilipendekezwa rasmi na pande zote mbili za Muungano, kwa ile
Ridhaa/Ratification rasmi kwenye Bunge la Muungano ambapo wawakilishi wa
Zanzibar walishiriki.

Sura ya 4 ya Katiba ya 1977 inazungumza kwa urefu na mapana kuhusu serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.

Sasa Zanzibar imefutika vipi Kikatiba?
Kero na malalamiko au nyogeza za mambo kutoka 11 - kufikia hata 47 au zaidi ni
suala la ama uzembe wa uongozi/wawakilishi au ukosefu wa utaalamu wa wale
wawakilishi wa Zanzibar katika Bunge la Muungano.Nina wasi wasi kwamba pengine
wawakilishi hao hata hawakuisoma katiba hiyo na kuifahamu,licha nyongeza zilizokuwa
zinapitishwa Bungeni.

Nassoro Moyo,alikuwa ni Waziri wa Sheria alifanya nini kuhusu mambo haya?
Au ndio kama Juma Khamis Faki ,asemavyo "...... wawakilishi wengi bungeni hawana
kazi ila kusinzia ...... na kwa hivyo bora kupunguziwa mishahara yao ....kwa sababu wao
hawawaletei umma faida yeyote na ni kunyume na ahadi zao wakati wa kupigiwa kura".


Lawama ni za Nani? Kwa nini zinazuka hizi " Po simo,Po simo"? Wakati wengi wa
wanasiasa wapigao kelele hii leo walikuwa wanashika khatamu za juu kabisa za
vyombo vya utawala .Hawa hivi sasa wanasingizia kwa kusema "Wakati ule mambo
yalikuwa mazito,kusema kinyume ya wakubwa zetu ".

Wawakilishi wa Zanzibar na Wanasiasa walikua wapi?
Kwa nini lawama zote kusukumiwa wasio " Wazanzibari " ?
Jee Wanasiasa wanaopiga kelele hivi leo ni kwa sababu zao za kibinafsi ?

Sisemi kuwa hawana haki ya kulalamika hivi leo ,ni haki yao kama vile ilivyokuwa haki
yao jana,juzi na miaka yote hapo kabliya - lakini kwa nini walingojea hadi hii leo ?

Sababu zao za kirahisi, wao hurogesha umma kwa kusema " Tulikuwa na Khofu na Woga".
Jee Sasa pale walipokula viapo na kushika Quruani tukufu , kwa Waisilamu na Bibliya kwa
Wakristo - walikuwa wana Dini au Imani Gani ?
Au Unyenyekevu wao ulikuwa tu kwa Vyama Vyao na Sera Zao?
Jee Utwii wao ulikuwa ni wa kutetea na kulinda Masilahi ya Nchi na Katiba au faida zao
za kibinafsi?
(Hapa nataka tuwakumbuke akina Othman Sharif,Kassim Hanga,Saleh Saadala,Idrissa Majura
na Twala).

Kikatiba Zanzibar inayo vyombo tawala "State Instruments",ambavyo nimevitaja hapao kabliya,
lakini ndugu zetu wa Tanganyika hawana vyombo bayana kama hivyo vya utawala .
Sababu za kasoro hiyo au kutobainika kwa vyombo kama hivyo inajulikana na hapana utata
uliojitokeza ambao hautaweza kutatuliwa endapo suala kama hilo litajitokeza .

Kuhusu kuwekwa bayana majina ya Jamhuri zilizoungana.

Kamati ya Maridhiano inasema kua jina jipya la Muungano lazima liwe bayana na
liwe kama ifuatavyo :

"Muungano wa Jamhuri za Tanzania - yaani United Republics of Tanzania".
Yaani Jamhuri ya watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika .

Sababu za kubayainisha majina ya nchi mbili ,ni kwamba jina jipya hilo litasaidiya utambulisho
wa nchi zilizo wanachama katika uwanja wa mahusiano wa Kimataifa.

Kwa upande wa pasi za kusafiria Kamati ya Maridhiano inapendekeza pasipoti hizo zitambulike
wazi kabisa kwenye gamba la usoni mwa paspoti zenyewe yakiwemo maandishi haya:

i) United Republics of Tanzania - Zanzibar Passport.
ii) United Republics of Tanzania - Tanganyika Passport.

Jee Kamati ya Maridhiano inataka haya kwa sababu za "Symbolic Values au Identity Value?".
Uzuri au umuhimu wa sisitizo lao hili linashabaha gani za kisiasa ?

Lakini hata hivyo,kinacho nishangaza ni ile mifano yao ya kutaka kuigiza USA au USSR katika katiba .
Kwa mfano kwenye suala la paspoti sijuwi kama nchi hizo zimepatapo kutowa pasipoti ambazo zimeweka
wazi wazi bangoni ,kua pasipoti hiyo ni kutoka "State" ya Texas ,South Dakota,Alaska,Hawaii ,Porto Rico
California au New Mexico .

Ikiwa ni Pasipoti za Jumuiya ya Uchumi wa Nchi za Ulaya yaani EEC,hilo suala tofauti.
Kwa sababu Jumuiya hii si dhahiri kimikataba kua ni ya Kisiasa,bali ni Jumuiya ya "Soko-Huru la Biashara";
ingawaje zipo ishara bayana zinazo onyesha kua nchi hizo za Ulaya zimo katika kuelekea kwenye ushirikianao
wa muungano jadidi wa kisiasa kwa masilahi yao ya kipamoja "European Common Interests".
Tamko rasmi la 1991 la Helsinki baina ya Gobachov na baba wa G.W.Bush linabainisha masilahi yao hayo..

Shabaha na lengo la Muungano wa Tanzania mbali na ule undugu wa kijadi na uasiliya wa wananchi
wake ; shabaha za Muungano ni sambamba na malengo ya Umoja wa Nchi za Afrika.
Kukataa hili ni upinzani na ni ubishi mtupu wenye misingi ya itikadi za kisiasa za vyama au viongozi
wa vyama na wafuasi wao .

Tukumbuke kua nchi inayoitwa Zanzibar ni Unguja na Pemba ,bila ya Pemba
hakuna Zanzibar na bila ya Unguja hakuna Zanzibar.
Tanzania inajulikana kua ni muungano wa nchi mbili huru za Zanzibar na Tanganyika.
Pasipoti za Tanzania za leo zinatambulika hivyo kua ni za Muungano wa nchi Mbili
bila ya kuwepo majina ya nchi mbili hizo zilizo wanachama.

Kuhusu Uraia.

Kuhusu suala hili la Uraia Kamati ya Maridhiano inatowa mifano ya nchi za kuigizwa.
Pendekezo lao hilo ni sawa na lile la pasipoti kuwekwa bayana ya nchi mwanachama na
wanapendekeza kila nchi iwe na taratibu za uraia na raia wake nje ya suala la Muungano.
Kwa upande huu haieleweki kwa nini Kamati ya Maridhiano ilitoa mifano ya USA au USSR
ya zamani.Kwa sababu kule USA hakuna Uraia wa Texas au wa Alaska ambao ni tofauti na
yule Mmarekani wa Alabama , Missisipi au Oklahoma - uraia ni mmoja tu.

Mapendekezo ya Kamati ya Maridhiano kuhusu katiba mpya ya Muungano,kwa mujibu
wa fikira zangu yanashadidiza kikhamasa na uchochezi wa baridi-baridi na kinjama za
kutaka kuivisha mambo yafuatayo :

a) Insular Mentality/ Uhumu-humu (b) Populism / Usisi Visiwani na Uwao Wabara.
(c) Obsession ya pasts political history/Ushikwaji wa shetani pepo wa siasa za
kizamani au shauku na ubumbuwazi.(d) Nostalgia na Glorification ya hadithi za ulela ulela.
(e) Mish-Mash Of Adamant ideology (f) Wookcoak Arguments and atitudes za kuamini kua
"leaders know best" na hawana chengine ila tu ule ushupavu wa "fierce loyalty to leadership
but with no other qualifications or political history to be where they are today".
Angalia baadhi ya waliomo katika hiyo Kamati ya Maridhiano wana msingi gani wa kujivunia
kisiasa au usomi ?.
Baadhi ya watu waliomo kwenye"Kamati ya Maridhiano"wamo humo si kwa chengine ila
kupiga madebe ya dhidi ya Muungano na kuchocheya chuki baina Zanzibar na Tanganyika.


Bila ya shaka wapo baadhi ya wananchi na wanasiasa ambao wanalo joto lao vifuwani mwao.
Na hilo halishangazi wala si jambo pekelo na wasemapo ".... Tuvumuwe kidogo" au wengine
wanasema "wanataka kutoa joto lao bila ya khofu na woga".
Wana haki ya uhuru huo wa kusema hayo na hawajapapo kukatazwa kufanya hivyo.
Na labda ndio maana baadhi ya wapinzani wa Muungano wanamshukuru Rais Kikwete,kwa
kuwapa nafasi hiyo na wanasema labda ndio sababu moja wapo "...za sifa hizo zilizo mvutia
Obama kuitembelea Tanzania".

Lakini hata hivyo, upo wasi wasi kua kuna baadhi ya wanasiasa wanaitumia nafasi hii,
sio kwa kueleza kero za Muungano ,bali ni kufanya usafii wa siasa-chuki na matusi ambayo
huenda yakaleta vurugu baina ya wananchi na ukatili ambao haijulikani utakuwajee.

Kuvurumishiana lawama na kuitana majina " Watimba Kwiri" au "Vibaraka vya huyu na yule au
"Usaliti na Ukhaini wa hichi na kile " haitaleta natija yeyote .
Inasemekana kuwa hali ya lugha kama hii inayotumiwa na baadhi ya Wanasiasa inakumbusha
zile "Nyigomvi na Matusi ya Kisiasa ya baada ya Uchaguzi wa 1957 kule Zanzibar" na hitimaye
ikabidi kufanyika yale Mapinduzi ya january 1964.

Lugha mbovu na za Kisafii za Zanzibar za baina ya 1959 hadi 1964 ndio hizi hizi zinazojitokeza
hivi sasa ikiwa ni katika masuala ya kisiasa za Zanzibar au hata mahusiano ya baina ya wa Visiwani
na Tanzania bara/ Tanganyika .
Lugha ya kusema "Sisi na Wao ".Hatari hii ipo,ishara zake ni nyingi tokea kwenye mambo ya
udini,matamko ya Uamsho,uchomaji wa Makanisa,kujuruhiwa kwa masheha,uharibifu wa ofisi za
chama cha CCM,kero za vitambulisho,kuhutumiana baina ya viongozi wa vyeo vya juu na lugha kali
kali za kisafii kwenye mikutano ya hadhara na kadhalika .

Lugha hizi za kipotoshi zititufikisha wapi na hao wanaoitumia lugha hiyo;azma zao ni nini ?

Jee kwani wanasiasa wa Zanzibar ,wameishiwa hata wafikie kiwango cha utafutaji wa ubingwa
wa"Mashindano ya Usafii wa Lugha ya Kisiasa Mikutanoni ?".

Hivi sasa ni miaka 50 tokea kuzaliwa Muungano,lakini wapo badhi ya washika khatamu za Uongozi
wa pande zote mbili ambao wapo katika mivutano-siasa isiyo na natija yeyote.
Fatalism na siasa mgando za Kiumwinyi zina nguvu sana hivi sasa visiwani Zanzibar na khasa
ndani ya chama cha CUF-Zanzibar kwenye Kamati ya Maridhiano na wafuasi wa Uamsho.
Nasema haya ili kukumbusha yaliyomtokea Rashid Hamad na wengineo au yanayofanyika
hivi sasa baina ya wale waliomo na wasiokuwemo kwenye Kamati ya Maridhiano.

Tatizo la Uwanasiasa Zanzibar na Tanganyika.

Uwana siasa kwa hivi sasa Tanzania umekuwa ni kama "Kazi ya Malipo/Profession".
Umaa wa wananchi wanashuhudia wazi wazi kwamba wengi wa Wanasiasa wa leo
wanayo itikadi na imani ya kua :
".. Kazi ya kupiga siasa imekuwa kama mchezo ; ni njia moja wapo rahisi ya mtu
kuweza kujiboresha na wengine hata kujitajirisha haraka kihali, mali na Ubinafsiya".

Mama wa sababu zote za uzukaji wa wanasiasa aina hii ni kwamba profession
hii eti inayo "... malipo na natija zake za kipekee na ni kubwa mno..".
"...baadhi ya professional politicians hawa,mbali na mishara minene,wao huweza
kuchukuwa watakacho na hata kufanya wapendavyo".

Kuwepo kwa hali kama hii inasababisha kuzidi kwa Umasikini na Rushwa.
Wananchi masikini wanazidi kudhalilishwa na kuwekwa katika hali ya uomba omba .
Na kwa sababu za Umasikini wao inakuwa wepesi wao "kukubali kutumiliwa" au kuwatumikia
wafadhili wao ambao wanawapa pesa ndogo ndogo za mahitaji yao ya kila leo.
Tatizo hilo linajulikana .

Haikataliki kua upo utovu wa heshima za utekelezaji wa miongozo na sheria za nchi na vile
vile upo uzembe wa kulinda na kutetea siasa bora za maendeleo ya chama tawala.
Lakini mbali na hayo,lazima tujue kua upo ukatili bayana wa siasa-uchumi za Ukoloni mambo
leo unaonekana.Kwa mfano ule mfumo wa siasa za unyongaji-uchumi dhidi ya nchi kama zetu.
Njama hizo za IMF ni moja wapo wa madonda sugu yanayosababisha umasikini katika nchi
nyingi za Afrika .Mbali na hiyo World Bank nayo ina mfumo wa masharti ya mirija ya ukamuaji
na kunyanyasa nchi zetu kiuchumi kupitia wafadhili wetu wa nchi za kigeni.

Haya yote ni miongoni mwa yanayo athiri uchumi na maendeleo ya nchi zetu mbili.
Inatambulika wazi kabisa kua panapokuwepo hali ya uchumi kama nilivyoeleza hapo juu na
kuwepo ukosefu wa nidhamu na uadilifu kwenye mfumo tawala na viongozi,basi bila ya
shaka patazuka ugonjwa wa rushwa ambao unambukiza umma katika misha yao ya kila leo.

Wananchi ambao wengi wao ni masikini na hasa vijana wa chini ya miaka 40 ambao ni asilimia
45 % ya wananchi wengi wao hawana kazi wala elimu ya kutosha ,basi kwa sababu ya umasikini
wao wanaweza kutumiliwa kirahisi na baadhi ya wanasiasa wapotoshi kusababisha fujo na ghasia
ili kutekeleza malengo yao ya ubinafsiya wao na kusahau masilahi halisi ya nchi .

Hebu tujiulize tokea kuanza mfumo wa vyama vingi vya siasa na kuanzishwa kwa ile siasa ya
"Kila Kitu Rukhsa "(ieleweke wazi hapa kua simsemi Mzee wangu/Mwalimu wangu Sheikh Ali
Mwinyi Hassan hapa ) "Freemarket" "Economic Recovery Program " au hata zile siasa na Miongozo
ya IMF na World Bank , zote hizi zimetufikisha wapi ?
Can our development take place when our production depends on the whims and demands of capitalist
developed societies or the so called "open,free world market ?.
Tukiamini hivyo,basi maendeleo yetu yatakuwa kama kuamini kupata ushindi kwenye mchezo wa
kamari ,na kwenye mchezo kama huo ni wengi wanao porwa - umasikini utazidi .

Mfumo wa "open free market" nchini umetuletea matajiri kuwa matajiri zaidi ;na umasikini hivi
sasa umekuwa kama "ukimwi " upo kwa wingi na hauna dawa .
Umasikini huo unapo zidi kukuwa nao unazalisha madhara mengine kwenye jamii ,kwa mfano rushwa
ujambazi ,utapeli ,wanawake na wanaume kuuza viungo vyao.
Kwa baadhi ya wanasiasa hali kama hiyo hutumiliya umma wa masikini hao "the lumpen " kwa njama na
ukatili wa shabaha zao za kisiasa.

Siasa za Wapinzani badala ya kuwaambia wananchi ukweli ".. wanasingizia kila ukosefu,kila shida
ziliyopo nchini sababu hua ni chama tawala.
Wengine huwa wanalaumu CCM hata panapo tokea ukosefu wa vua au hata ikiwa juwa ni kali sana,
basi kinacholaumiwa hua aidha Mapinduzi ya 1964 au siasa za Chama Cha Mapinduzi .

Wapo baadhi ya wanasiasa ambao hawapati usingizi ikiwa hawajaweza kuzusha lolote la kuleta
mambo ya mivutano na usafii au usambazaji huki na ubaguzi baina ya wananchi hata kidini.
Ikiwa si kunyokowa nyokowa ukosefu wa hichi na kile,patakuwepo hadithi za "Usisi na Uwao ";
wakisha hapo patakuja masuala ya nani au nini "Uzanzibari,Uzanzibara,na Ubara au Utanzania".

" Hebu tuseme kweli ,shetani aone aibu "

Ni kweli kabisa kua ukweli una uma - lakini kila Mzanzibari Mkweli anajuwa wazi kwamba,
siasa za mivutano ya ndani ya Unguja za kusema " Wao na Sisi " ambazo ni za utafautishaji wa
watu baina Wavisiwani (Sisi) na Wabara(Wao) hii si siyasa mpya ya leo.
Hii ilikuwa ni msingi mkubwa wa"...kasumba ile ile ya siasa ya ZNP-Hizbu kabla ya uhuru na inasemekana
kua ni moja wapo wa miongoni mwa sababu nyingi za Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964.
Ni kasumba ile ile,kwenye mtungi mpya wa CUF na Uamsho - hasa kwenye masuala ya Muungano na "Usisi na Uwao".
Ile slogan ya "Zanzibar Kwanza" ni wito wa jazba na suala la Nini na nani ana haki ya Uzanzibari ni uchokozi?.


Ni uchokozi kwa sababu katika siasa za kale palikuwa na hata vichekesho vya kusema kua ikiwa mtu hakujuwa
kutofautisha baina ya "L" na "R" kutamka"Haluwa " kua "Haruwa",ntu huyo alinyanganywa Uzanzibari wake.
Lakini aliyesema "Bana" badala ya "Bwana" au aliyesema" Nkate" badala ya "Mkate" hakupoteza Uzanzibari wake.
Ila tu yule aliyesema "Nkate" alitambulika kuwa ni mtoka Pemba;na yule aliyesema "Bana",alitambulika tu kuwa yeye
ana asili ya Barahindi.Na yule aliyesema "Manyegi au Manyege badala ya "Mwenyeji",alitambulika kwamba ni mtu
mwenye asili ya Arabuni ,yeye nae pia hakukataliwa "Uzanzibari wake".Lakini wale walioyesema "Haruwa" badala ya
"Haluwa";Uzanzibari wao ulitiwa mashakani na wasi wasi na hata kupoteza haki ya kupiga kura -kwa nini ?.
Wamasai au watu wasio kuwa waisilamu wanasumbuliwa na kubaguliwa kichokozi na kwa chuki hata za kidini.Kwa nini ?

Mara ngapi Nassoro Moyo,inambidi hadharani kujieleza kua yeye ni mzalia wa Zanzibar na kusema kwamba ni baba
yake tu ndiye mwenye asili ya bara?
Kwa nini inambidi awe anasema hayo katika mikutano ya Kamati ya Maridhiano,lakini Eddy au hata Professor Abdul Shariff,
hawalazimiki kufafanua mambo yote hayo?
Jee Ndugu Moyo ameshanusia kasumba hiyo ya Uhizbu katika Kamati yao ya Maridhiano?.

Ubovu na fitina za siasa zenye kuchunguza uasiliya wa Mzanzibari nilioutaja hapo juu,hivi sasa umerejeshwa kwa njia
nyengine mpya hasa mjini Unguja na katika baadhi ya vijiji vya huko Pemba .
Ishara kama hizo zipo za "Kidhahir " na zipo nyegine nyingi za " Kujitakia ".

Si dhani kuwa huu ni wakati wa siasa kama hizo;wasemao kinyume ya hayo basi wanazo sababu zao maalum za kisiasa
ambazo wanazificha .Wanasiasa kama hawa wanawajibika kujitamka hadharani.

Inawezekana kua ipo miongozo ya siri ya baadhi ya vikundi ndani ya chama chao ,Kamati au Taasisi
zao nchini Zanzibar ambazo zina agenda nyenginezo za siri za kuteteresha amani iliyopo.

Kwa mfano,ile slogan ya "Zanzibar First" yaani ni kama " Wito wa kuitana Vitani".
Hii pekee ni ishara moja wapo ya " re-emergiance of hate politics " yaani ni ile ile ya
" Usisi dhidi ya Wao " yaani wale wote wasemao "Haruwa badala ya Haluwa" na dhidi ya
wale wote ambao wana fikra nyingine kuhusu suala la Uzanzibari ,Muungano na katika Mpya .

Ilikuwaje hata ikawa "Uzanzibari na Ujananchi/Uwananchi unakubalika au kukatalika kwa
misingi ya itikadi au msimamo wa kila mtu kwenye suala la Zanzibar kuwemo au kutoka kwenye Muungano
huu tulio nao hivi sasa?
Wapinzani wa Muungano wanasahau jambo moja ; jee zile haki ya binaadam za uhuru wa kufikiri ,kujitamka
na kuchaguwa wamezipeleka wapi ?
Zile slogan zao za "Haki " "Haki Kwa Nani " " Haki kwa wote" Slogan zimemepotelea wapi ? Au ni za unafiki ?.

Nina uliza hayo kwa sababu ya matamko yao makali ya baadhi ya Wanasiasa wa visiwani na
hasa wale wapinzani wabishi dhidi ya Muungano .Mshupavu wa ukaidi huo ni kwa mfano Mheshimiwa Jussa
na wengineo wa chama cha CUF au wengineo ambao wanajitokeza au kuzuka zuka katika mikutano ya Uamsho.

Kwa vyo vyote vile, mada hii kwa leo sitaweza kuijadili kikamilifu kwa sababu ,endapo nitafanya
hivyo basi sitaweza kutimiza niliyokusudiya katika andiko langu hili.

Kwa hivyo,bora nirejee kwenye yale "Mapendekezo au "hoja" na "mifano " iliyotolewa na wafuasi wa
CUF na Uamsho kwenye mikutano yao ya hadharani inayo chapishwa kwenye Zanzibaryetu, kwa niaba
ya Kamati ya Maridhiano kuhusu suala la Uraia.
Wanakamati wa Maridhiano wamependekeza mambo mengi na la Uraia wamependekeza kama hivi
ifuatavyo:

" Kwa vyo vyote vile katiba mpya isijumlishe suala la uraia kuwa la pamoja kupitia
Muungano.Kila nchi mwanachama katika Muungano ibakie na uraia wake na raia zake ".

Kwa pendekezo lao hilo wanajaribu kulitilia mkazo au kuhalalisha "hoja" yao hiyo wameto mifano ya
mifumo ya "Ushirikiano/Jumuiya ya Uchumi wa Nchi za Ulaya/EEC/European Union au mfumo wa
Freemarket and Free Movement of People etc".
Kwa kweli mifano ya pendekezo lao hili ni la aina za Ki-wishful-thinking na kwa kadiri fulani ni
njama za upotoshi na siyo hivyo tu bali zipo ishara za ubutu na ubabaishaji wananchi .

Lina ubutu ,kwa sababu mfumo wa Jumuiya ya nchi za Ulaya umeanzishwa kutokana na
mazingara makhasusi,kwa mahitaji maalum yenye malengo ya ndani nchi wanachama ambazo
zimepelelea na kudhibiti shabaha zao za siasa-uchumi za kuingiza utajiri wa mali asili kutoka nchi
za ngambo njee ya bara lao la Ulaya yaani kutoka Africa,Asia and Latin America.

Pili ,mfano wao unao ubutu mwengine kwa sababu Jumuiya ya EEC,ni Jumuiya wa uchumi,
jumuiya ambayo kwa wakati huo huo ina nguvu za kijeshi zenye malengo ya kisiasa za
kulinda na kutetea "interests zao " kote ulimwenguni kwa kila hali hata kwa njia za kivamizi kama
vile walivyo fanya Iraq na Libya kwa visingizio na choko choko za uwongo.

Hali halisi na misingi ya mazingara yaliyo unda Jumuiya ya Kiuchumi wa Ulaya ni tofauti kabisa
na misingi na azma asiliya za Muungano wa Tanzania.
Muungano wetu una misingi ya undugu wa kijadi ambao ni sambamba ya maazimio ya umoja wa nchi
za afrika.

a)Kupigania Umoja na Muungano wa Bara la Afrika,kufuatana na Umajumui wa Afrika yaani
Pan-Africanism.
(b) Kulikombowa Bara la Afrika kutoka kwenye Utumwa wa Ukoloni Mambo Leo.
(c) Kulilitowa bara la Afrika kwenye Utumwa wa Kiuchumi na kukomeshwa kwa Ukimwishi wa Utamaduni
wa nchi za Afrika.

Historia imejiweka wazi na inajisemea wenyewe .
Hebu tuchunguze historia ya East African Cummunity na tujiulize nani walilimbika fitina na ukorofi hata shirikisho la
East African Community-likalala pero ?.

Ni hao hao watawala wa kale ,ndio waliosambaza fitina na mivutano mwishowe wakapata wasaliti wa ndani ya
East African Community na wakaibomowa Jumuiya hiyo 1972.

Ni hao hao hivi sasa ndio wanaotushawishi tufuate mifumo ya Jumuiya zao,Ushirikiano wao na hata mifumo ya aidha
Jumuiya zao au Miungano yao - tubomowe yetu tuliyo nayo.

La kushangaza ni kwamba mara tu ,baada ya kutubomoleya EA -Community yetu ,Waulaya hao hao wakaanzisha
Jumuiya yao ya Uchumi wa nchi za Ulaya , EEC mnamo mwaka 1972.
Yalifanyika hayo mwaka huo huo mara tu walipokwisha tumaliza na tukabomowa ile East African Community .

Cha kustaajabisha hivi leo , ni kwamba Waulaya hawa hawa - hivi sasa wamo katika kuengeza nchi wanachama kwenye
Jumuiya yao. Croatia na Bulgaria zinaiingia kwenye Jumuiya yao kiuchumi tu,bali hata kwenye mambo ya kijeshi na kisiasa
zao za ndani na nje za nchi zao .

Siasa yao inapelelewa kwa " Slogan " ya Wito wa kulinda na kuhifadhi hicho wakiitacho "European Common Interests ".
Sasa hebeu tujiulize hichi wakiitacho"European Common Interests" ni nini ?.

Verejee hii leo tuone watu wetu ndugu zetu wananchi wa Tanzania ,wanataka kuvunja Muungano wao uliojengwa kwa
taabu na mashaka ya miaka 50 ?. Kwa visingizio vya wivu wa vyeo ushikaji wa khatamu za serikali ?.

Ubutu mwingine ni kwamba, kulitowa suala la Uraia lisiwepo kwenye mambo ya Muungano.Kufanya hivyo itakuwa sawa
kwenye kinyume au usaliti wa azma na malengo au shabaha takatifu za wale Wazee wawili ambao ni Wazazi wa Muungano wa
Jamhuri za Tanzania.

Kuuvuruga na kuuharibu Muungano wa Tanzania haitokuwa ni usaliti wa hali ya juu tu bali ni dhidi ya imani ya ile "spirits of the
founding fathers". Isitoshe itakuwa ni ukomo kwenda minyume na ya wale wote waliokuwa wamesimama kidete kuunda huu
Muungano wetu huu wa kijadi na itakuwa ni donda la malengo ya Umoja wa nchi za Afrika.Itakuwa ni kinyume na malengo ambayo
yalikubaliwa na kutambulikwa na vyama vyote vilivyokua vikigombania uhuru wa nchi za afrika.


Ingawaje ni kweli kwamba, tunawaona baadhi ya "vigogo vya siasa za kale",hivi sasa wapo kwenye kambi ya wapinzani wa Muungano
lakini kuwemo kwao huko haihalalishi kwamba hayo wasemayo ni kweli na matakatifu. Kamwe !!

Wayasemayo hivi leo kua eti :
" ....wakati ule wa siasa kali ,mtu alikuwa hawezi kutowa fikira zake huru...".
".... kila alilokuwa akisema Mzee Karume ,halikuweza kupingika".
".... kila alilosema Mwalimu Nyerere,halikuhojiwa na kadhalika".

Ikiwa hiyo ndio hali ya mambo ilivyokuwa wakati ule ;jee kwani hali kama hiyo haipo hivi sasa katika vyama vyao ?
Kwa nini Rashid Hamad alishambuliwa na hata katolewa katika chama cha CUF ?
Kwa nini CCM imefukuza baadhi ya wanachma wao au hayaonekani yanayotokea katika Chadema ?.

Jee hisia au siasa kama hizo ,au wanasiasa kama hao wanaweza kuaminika ?.
Jee wanasiasa kama hawa wanaona ya wengine tu ,lakini hawajioni wenyewe wafanyavyo?.
Jee wanayasema hayo hivi leo kwa sababu wao wamejaaliwa kuwa na ndimi mbili ?
Jana walitumia limi la upande wa kushoto kulaumu makosa ya wengine na hivi leo hao hao wanataka kutumia limi lao la upande
wa kulia kwa kuficha maovu wafanyayo - au vipi ?.

Wasi wasi wangu ni kwamba ,siasa ya leo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ina ukali wa pili-pili, na iknanibidi kuuliza
jee "vigogo hivi vya kale " au aina ya "Professional Politicians"watatumia ulimi gani katika siasa zao za kujiboresha na hata
waweze kutanguliza masilahi yao binafsi ,na kudharau masilahi ya taifa na Umoja?.

Si ni hawa hawa na ndio wale wale waliokuwa wakilikataa Azimio la Arusha?.
Si ni hawa hawa waliokuwa wakisema kua Azimio la Arusha liishie chumbe?.
Walisema hayo kwa nini ?
Walifanya hivyo kwa sababu Azimio la Arusha lilikuwa na miiko yake. Azimi Lili haramisha wizi wa mali za taifa.
Azimio la Arusha lilikua lina mhoji na kumsuali kila mwanasiasa jinsi anavoupata utajiri wake.

Ilikuwa ni mwiko kwa "Mwanasiasa kuiba mali za serikali na za wananchi leo watu wanaporwa tu kwa nguvu za
kitawala na ujangiri na rushwa.Mashamba ,viwanja vya watu wanauziwa watu sita au hata kumi wakati mmoja.

Rasimu ya Katiba ya Muungano inapendekeza kua " Ni Mwiko kwa Mwanasiasa Kusema Uwongo".
Jee wanasiasa wa leo watasema kua "Miiko wa kuzuwiya Uwongo kwa wanasiasa nao uishiye kule kule Chumbe ?".

Wengi ya baadhi ya hawa vigogo vya zamani vya kisiasa hawakuipenda ile siasa ya Miiko ya Uongozi.
Hadithi za watu wa aina hii ni nyingi,tukizianza hatutamalizia dhumuni ya andiko hii .

Bora Turejee katika suala la Uraia .

Sasa tujiulize.
Kamati ya Maridhiano ,inasema kwa upande mmoja "...kila nchi iwe na raia wake;
pawe na freemarket na free movement of people ;lakini sheria za uhamiaji wanadai kila nchi
mwanachama iwe na sheria zake kwa sababu ya udogo wa Zanzibar.Lakini papo hapo
wanasiasa hawa wanapendekeza pafanyike utaratibu ambao raia wa nchi mbili, wawe na haki za
kufaidika na wapewe fursa zote katika nchi mwanachama nyiingine,lakini Zanzibar iwe
na umakhsusi kuhusu mambo ya uhamiaji kwa sababu ya udogo wake .

Itakuwa ni jambo la busara endapo Kamati ya Maridhiano itajieleza hicho wakitakacho?
Na wajieleze kwa nini walitowa "Mapendekezo yao wiki moja kabla ya uzinduzi rasmi
wa Rasimu ya Katiba ya Muungano,kwa sababu kufanya kwao huko pengine ndio maana
wasemayo aidha yanagongana au yanapinduwa ukweli wa yaliomo katika Rasimu.
Bomani ,amefunguwa watu macho - na ameuzika uwongo mwingi wa wapinzani wa Muungano.
Kuna mambo yaliyo pendekezwa na Kamati ya Maridhiano ambayo kwa kifupi huenda
yakaeleweka kua wakitakacho ni ile iitayo :
" Chetu Chetu,Chao Chetu ndani ya au nje ya huu Muungano wetu".

Kuwepo fikra kama hizi basi zitasababisha Upotoshi.

Wapo baadhi ya wanasiasa ambao wamejilewesha kujihisi na kuamini kua wao kama ni watume
wa kisiasa.Wanaamini kua kila wasemalo liwe kama mshafu.
Fikira zao hizi ni za kiulevi na wivu wa vyeo na "Umwinyi au itikadi za Fatalism".
Mara nyingi fikira kama hizi zinatokana na Political Ignorance/Ujinga wa Kisiasa na wakati
mwingine baadhi ya wanasiasa hawa hujitokeza kijeuri,ubishi na ujabari wenye ukosefu wa
ukomavu kwenye masuala jumla ya kisiasa za jamii.

Baadhi ya ujinga huu wa kisiasa unaweza kupaliliya zile "delibarate misleading politics"
zenye shabaha za ubibinafsi na usambazaji wa potoshi za Populism.Potoshi za kuwaambia wafuasi
wao wapendayo kusikiya na kupigiwa vigelegele na kuyarudiya hayo kwa hayo wakifuata ule mtindo
wa propaganda za Gollbes ,aliyekuwa waziri habari ambaye aliamini kua "...kila unapo rudia uwongo
huo huo mara kwa mara na wananchi hawana nafasi ya kusikia jengine,basi mwishowe wanabidi
kuamini uwongo huokuwa ni ukweli".

Mapendekezo ya Kamati ya Maridhiano kuhusu masuala ya uraia,uhamiaji,na uwakilishaji katika
mahusiano ya kimataifa.

Jinsi ya Kamati hiyo ilivyo panga Mapendekezo yake ,ni dhahiri kabisa kwamba kuyatowa mambo
hayo matatu kwenye mambo ya Muungano itakuwa ni sawa na kuukataa Muungano kwa ujumla .

Wanao sisitiza hayo ,hawayafanyi hayo kwa sababu ya masilahi ya wananchi wengi wa
Zanzibar .Hizi ni njama za kuandaliya uanzishaji wa mfumo mpya wa tabaka za kijamii nchini
Zanzibar.Njama hizi zinandaliwa na "professional politicians" ambao wanashirikiana na baadhi
ya wafuasi wao wakiwa aidha ni wa mchanganyiko wa viongozi wa CUF na baadhi wa CCM
baadhi ya wazenji waishio nje ya Tanzania.

Lengo na shabaha zao ni moja ni kulinda masilahi yao ya kibinafsi kwa hivi sasa na kwa siku za
usoni.Malengo yao yenye misingi ya wivu wa kugombania vyeo na dhamana kwenye serikali na
vyeo vengine vya kati pamoja na vile vyeo vya kuiwakilisha Zanzibar katika nchi za njee,
kama kazi za Kibalozi.Mara nyingi huwa tunasiki:

"Mbona nafasi za kibalozi nyingi zimeshikwa Watanganyika ?
"Mbona Wazanzibari hawapewi uwaziri katika serikali ya Muungano?".
"Katika Umoja wa Mataifa kuna Mzanzibari mmoja tu ".
Katika Mkutano wa Bububu hivikaribuni Jussa ,alisema kuwa mara tu watakapo itowa Zanzibar
kwenye "...tumbo la chatu la Muungano basi Seif Shariff ,atapewa Urais wa Zanzibar na Moyo
ataitundika bendera ya Zanzibar katikaUmoja wa Mataifa ... ".
Ikiwa haki hiyo ipo kimkataba au kimakuliano na masharti ya qualifications na mazoezi ya ujuzi
wa kazi yapo kwa upande wa Wazanzibari,basi kwa nini wahusika hawajadai haki zao hizo ?
Au hadithi itakuwa ni ile ile "....tulisema lakini wale wabara kule Dodoma walitukatalia ".
Ikiwa hayo wasemayo ni kweli basi na waonyeshe ushahidi wa kimaandishi au ndio watakuja na ule mtindo wa kusingizia
maiti wa kusema "....tulikuwa na khofu nawoga na hata Mzee Karume hakuwa na mambo ya kuweka makaratasi".

Elements za watu kama hawa zimeelezwa kikamilifu na Mwalimu Nyerere, in 1995 alipokuwa akizungumzapamoja na
waandishi wa habari mjini Dsm.

Kasim Hanga ,aliwahi kuyazungumza hayo hayo,kivyake kwa wakati wake lakini kwa bahati mbaya hakueleweka au
aliyoyasema yalipindiliwa na akapagazwa uwongo.
Hakuungwa mkono na wanasiasa wa wengi wa Zanzibar kwa sababu ya "woga na khofu za wakati ule".
Hitimaye inajulikana yaliyo wafika yeye pamoa na Othman Shariff,Twala,Saleh Saadalah, na Idirissa
Majura . M/Mungu awalaze wote mahala pema -amina .

Wananchi waambiwe ukweli.

Baadhi ya "wansiasa wanaamini kua endapo watapata nyadhifa za kuendesha nchi na uwakilishaji wa
nje ya Tanzania ,basi Zanzibar itafunguliwa milago yote ya "neema ,misaadana zakat ".
Na kwa missada hiyo Zanzibar itaweza kuendelea kwa sababu kwanza ni ndogo na itabahatika kupata
misaada yote hiyo kutoka kwenye nchi zote tajiri za Kiisilamu za Arabuni.

Lazima tuelewe kua suala la ukosefu wa maendeleo Zanzibar au afrika kwa ujumla sio kwa ukosefu wa misaada bali ni
shida za uadilifu na uzembe wa wanatawala na kwenye umma wenyewe.
Baadhi ya Wananchi ambao wengi wao aidha wanapata misaada ya fedha kutoka kwa ndugu zao waishiyo
nje au wanategemea kufanyiwa kila kitu na serikali.Wanategemea kufanyiwa na sio kulifanyia taifa lao.
Kazi zilizozopo aidha hawazitaki au hawana ujuzi na mazoezi ya kazi zinawezaza kupatikana.
Ziwengi wanaopenda kazi za kilimo ,ufugaji au uvuvi - kuna baadhi ambao wanazidharau kazi kama
hizo.

Fikira za kuomba omba na kutegemea misaada kwa ajili maendeleo hazipo tu kwa wananchi wa wakawaida bali hata
kwenye Baraza la Wawakilishi Zanzibar huwa mara nyingi zinajitokeza.
Kwa mfano Mheshimiwa Raza ,mara tu alipoingia kwenye Baraza la hilo basi miongoni mwa
aliyoyasema ni "...Tunataka kuingia katika Umoja wa nchi za Kiisilamu kwa sababu ya njaa zetu
lakini tuliambiwa kua bora ombi la uwanachama huo uombwe kwa niaba ya Tanzania kamili ".
Nguzu Raza,alikuwa akisema mambo mawili kwa wakati mmoja.
Kwa upande mmoja ni ile tamaa ya kupata misaada itakayo towa njaa na kwa mwingine alikua
anatowa lalamiko la "kubanwa kwa Zanzibar kuwa na uhuru wa kufanya mahusiano ya kimataifa
na nchi za njee " kama kwa mfano faida zitakazo patikana endapo Zanzibar itakua mwanachama
wa nchi za kiisilamu ".

Wanasiasa wengine wanawapa tamaa wananachi wa Zanzibar kua:
"Jamhuri huru ya Zanzibar itakuwa inanawiri na itakuwa ni kama Dubai ya Afrika Mashariki.
Mataa yatakuwa yanamurika mchana na usiku Pemba na Unguja mijini ,mashambani na hata
kwenye mapori ".
Tamaa hiyo ndiyo inayo rogesha baadhi ya Umma wa Wazanzibari .

Na kwa bahati mbaya au kwa sababu ya umasikini ulio sambaa nchini basi wapo baadhi
ya wananchi ambao wana amini "Uchawi huo wa wapiga madebe matupu ya Siasa".

Kuna wengine wanao amini kua "Taa za barabarani na hata taa kwa ujumla za ulimwenguni
zilianza kuwepo Zanzibar kabla ya Ulaya au Marekani".

Baadhi yao utawasikia wakijifurahisha kwa kujiuliza na kujijibu wenyewe kusema hivi:
"Television za kwanza East Africa zilianza wapi? Zanzibar !!!.
"Kilwa ile ilikuwa ya nani ? Zanzibar !!! "Ile Mombasa ilikuwa ya nani? Zanzibar !!!
Nani kaanzisha uvaaji wa kanzu na kofia Msumbiji na Tanganyika? Zanzibar.
Nani aleyepeleka ustaarabu Rwanda,Congo,Uganda na Kenya ? Zanzibar!!.
"Ubalozi wa kwanza wa Marekani East Afrika ilikuwa wapi ? Zanzibar 1837 !!

Ukweli wa mambo ni kwamba ,kwa mfano huwo ubalozi ulifunguliwa kwa sababu ya
kuharakisha biashara zao za Watumwa kwenda Amerika .
Na yote wanaotaka kujifakharisha na kujinasibisha nayo ni ya "Utawala wa Kigeni wa kale
wa Waarabu na mfumo wao wa siasa ya Utumwa ambao ndio sababu ya sababu nyingi za yale
Mapinduzi ya 1964.Mapinduzi ambayo yalingowa hisia za udhalilifu na unyonge wa wengi na ndiyo
leta hata kuanza mtindo wa Television East Afrika .

Wakisia hayo utawaona wanavyo payuka payuka "Oh sio hivyo,sio hivyo ,mfumo wa utumwa
wa waarabu haukiwa wa kikatili ukilinganishwa na ule wa Wazungu".
Fikira za watu kama hawa ni kwamba wao bado wapo katika hali ya " colonised in mind body
and soul ".
Watu kama hawa wanahitaji wakombolewe kwenye fikira za kiutumwa na udhalilifu
wa kifikra walio nao .

Hawana wala hapana sababu yeyote ya wao kujifakharisha/Glorification na zile hadithi za alifu
ulela ulela za utawala dhalimu za Kigeni za Omani , Muskati ,za Kireno au hata za Uingereza.

Watanzania/Wazanzibari ambao wanajinasibisha na tawala hizo za Kigeni ,wao huwa wanapenda
yatajwe "mazuri" wanayo fikiri wao ;lakini yasisemwe ambayo wao hawayataki yazungumzwe na
hawapendi hata kulaani mfumo wa Utumwa .
Tatizo la watu kama hawa ni kwamba bado wanahitaji kile kiitwacho " Decolonization from
mental slavery".

Siasa ya Utumwa au Ukoloni ,ikiwa ya Wazungu au Waarabu hapana iliyo na nusu dhambi au robo
ya dhambi .Utumwa na Ukoloni wa kigeni wa aina yote unabeba dhambi kamili.
Na ni dhambi dhidi ya Uungwana na ubinaadam.

Siasa za Uhumu Humu "Uvisiwani ".

Siasa za "Uvisiwani" ,"Populism" na mgando wa hizi "Insular Mentality " kwa kweli zinatiya balaa
na zimewateka nyara sana baadhi ya wananchi kwa sababu ya uchache wa ujuzi na elimu zao.

Mama wa ujinga huu ni umasikini wao ulio jaa nchini .Mara nyingi ndugu zetu hawa wao huwa
na imani kubwa ya kuyakubali na kuamini kila lisemwalo na wakubwa zao kwa umuri,elimu
au ushikaji dhamana au cheo cha kazi.
Wameganda kwenye ulemfumo kitabaka za kijamii "social structure " na Fatalism ,fikra ambazo
hazina maana katika ulimwengu wa leo .

Jamii yeyote ambayo inaongozwa kwa taratibu na fikira kama hizo huwa ni pingamizi za kwa
binaadam kua huru na kwa maendeleo ya kawaida .
Mfumo au taratibu kama hizo zinabomowa uhuru wa kufikiri na wa kujitamka na ni aduwi mkubwa
katika kudhibiti na kusambaza Demokrasia nchini.

Haiwezekani kwamba eti uzaliwa au ukubwa wa cheo cha mtu kihalalishe " kusema uwongo na
kudhulumu au wasiwajibike kuhojiwa kwa yale wanayo yatamka na vitendo vyao katika jamii ".

Msingi wa siasa bora ni kuwepo Miongozo na Miiko kwa Wanasiasa na Viongozi.
Miiko ya kukomesha na kupiga vita Uzembe ,Uwongo ,Wizi wa Mali za Umma!!
Azimio la Arusha liwe ndio "jicho ,sikio na masharti ya uongozi" wa daraja zote
za tawala .

Rasimu ya katiba mpya ya Muungano inapendekeza mambo hayo.
Jee wapo wanasiasa wa Zanzibar ambao kwa sababu ya kuwepo Miiko kama hiyo au kama ile
ya Azimio la Arusha ndio sababu zitakazo wapa kuseme kua Muungano umazikie Chumbe ?

Ikiwa ni hivyo basi ,ipo sababu kubwa ya kuwa na wasi wasi kuhusu wanasiasa au hata
viongozi hao kwenye misingi ya udemokrasia wao na kuheshimu mambo yafuatayo.

(1) Good Governance (2) Trancparancy(3) Credebility na Accountability .

Haiwezekana kuwepo utawala/serikali takatifu bila ya misingi au nguzo nne hizo.
Itikadi potoshi zenye giza la "Insular Mentality,Umwinyi ,Political Ignorance and Fatalism" ndio
mama wa ajali na misuko suko tuliyo shuhudia katika historia yetu ya 1961,1963,1964,1967,
1972;1973;1974;1977;1985;1990;1995;2001 na 2005 pasina kusahau yaliyotokea bandarini
Zanzibar 1948.

Nimesema hapo kabla katika andiko hili kua,ahadi potoshi za "Professional Politicians" ni nyingi mno.
Kero na kasoro za kikatiba zipo katika mfumo wa leo wa Muungano zinahitaji marekibisho .
Uzembe pamoja na Ukosefu wa nidhamu na uadilifu upo ,wapo wanasiasa tawala wenye makosa
ugonjwa wa nepotism upo yote haya yanahitaji kutatuliwa kwa njia za amani na maelewano.

Tatizo la suala la mfumo wa Katiba Mpya ya Muungano, shina lake lipo kwenye misingi ya itikadi
ideological kwenye vyama na wafuasi wa vyama hivyo .Wengine wanaitumilia dini kwa malengo yao
ya kisiasa.

Lakukumbukwa ni :
Chema Chetu Cha Milele Ni Muungano Wetu.
Muungano utiliwe nguvu kabisa, uwe jadidi ,madhubuti na ka mising ya Usawa.
Muungano Oyeeee!!!!!!


Ali Mtsashiwa

Saturday, 1 June 2013

State of Zanzibar...


State of Zanzibar? Issue ipo mahakamani...

Tuesday, 7 May 2013

Jaa la Jang'ombe na Usalama wa Watoto...


Watoto hawa pichani walionekana katika jaa la Jang'ombe wakitupa taka. Jaa hilo lina kontena la kuhifadhia taka hata hivyo wakati watoto hawa wakitupa taka zao lilikuwa limefurika na kusababisha taka kutupwa nje ya kontena.

Mbaya zaidi watoto hawa hawakuwa na hata na viatu wakati wakitupa taka zao. Hii ni hatari kwa maisha yao na kiafya kwa ujumla. Itakuwa ni jambo la busara kwa wazazi kuhakikisha kuwa watoto wao wanapowatuma kwenda kutupa taka wawe wamevaa viatu.

Aidha kwa upande wa mamlaka husika ya ukusanyaji wa taka, hawana budi kuhakikisha sehemu za kutupia taka zinakuwa katika hali nzuri kila wakati ili kuweza kuzuia tatizo lolote ambalo litaweza kuokea kutokana na mirundiko ya takataka.


Picha kwa hisani ya Sabri Juma

Friday, 26 April 2013

Muungano Oyeee!


Somewhere near Shangani...