Asiyetaka Kuishi Unguja Atoke!
- Karume Amwambia Balozi wa Iran.
Bwana Karume amesema hayo alipokutana na Balozi wa Iran aliye nchini Ethiopia ambaye kwa wakati huu anatembelea nchini Tanzania Bw. M.E Moghadom. Walizungumza juu ya wasichana Waajemi walioozwa Zanzibar wiki iliyopita.
Bw. Karume amesema hakuweza kusema chochote juu ya wasichana wane Waajemi ambao wameolewa kwa vile walikuwa wakiishi na mabwana zao "Wanafurahia sana" alitamka.
Bw. Karume alisema "Hatuwezi kufuata vile watu wengine wanafanya kwa kuwa sisi ni watu huru".
Aliongeza "Tunajivunia kusema kuwa tunaishi kwa furaha".
Alimwambia Balozi huyo kuwa wasichana wamekwishaolewa na kwamba walikuwa wakiishi kwa furaha na mabwana zao.
Kuhusu sheria za ndoa, Bw. Karume alisema zilifanywa ili kuwezesha kila raia kuoa bila kubaguliwa.
Alisema yale yaliyotokea katika magazeti yalikuwa jitihada za mabeberu na kuongeza; "Ninaposema mabeberu sisemi weupe peke yao lakini wote wanaofuata amri zao".
Alisema kuwa nchi zilizo jirani haziwezi kufahamu hila na maarifa ya mabeberu lakini sisi tunazijua hatuna hofu kwa sababu hivi karibuni watajulikana.
Bw. Karume aliongeza kusema kuwa habari hizo zote zilikuwa zikitoka kwa watu ambao hawakupendezwa na maendeleo yaliyokuwa yakifanyika nchini.
"Tutawezaje kuishi kwa udugu ikiwa tutakubali wengine kufikiri kuwa watu wa chini?" Aliuliza Bw. Karume.
Alisema wajibu wa kwanza wa Chama cha Afro-Shiraz Party ulikuwa kuondoa ukabila na kufanya watu kujisikia wenye furaha na kufurahia uhuru walioupata kwa shida.
Aliongeza kusema kuwa mafungu mafungu ya watu yalimalizika katika Zanzibar na kusema " Watu watawezaje kufurahia uhuru wao ikiwa ukabila unaendelea katika Jamii?"
Bw. Karume alisema ulikuwa wajibu wa watu wote waliostaarabika kuondoa kabisa ubaguzi na shida miongoni mwa watu.
Aliuliza " Tutawezaje kuwa na umoja ikiwa hatuwezi kuoana?"
Bw. Karume alimwambia Balozi aliyetembelea kuwa alikuwa huru kukutana na Waziri wa wasichana walioolewa katika State House na akakutana nao.
Chanzo: Gazeti la Baraza
Toleo: Namba 1623
Tarehe: Alhamisi Oktoba 1, 1970
Bei: Senti 35 Kenya, Senti 40 Tanzania na Uganda