Thursday 18 January 2007

SMZ yafanya kweli

Kwa muda mrefu mifuko ya plastic nyepesi imekuwa ikitumika kwa wingi katika visiwa vya Zanzibar, kuja kwa mifuko hiyo kulitokana na kisiwa hicho kuwa kivutio cha pekee cha biashara katika afrika ya mashariki katika ile miaka ya tisini mwanzoni... Matumizi ya mifuko hiyo ilikuwa ni kwa bidhaa mbalimbali, aidha mteja hakupaswa kulipia chochote kwa ajili ya bidhaa yake kutiwa ndani ya mifuko hiyo.
Umaarufu wa mifuko hiyo ikashika kasi kiasi kwamba ikiwa sio lazima tena kwenda sokoni au dukani ukiwa na kikapu au mkoba. Umaarufu huo ukaongezeka hadi kufikia kwenye vyakula, sasa ikawa ukienda kununua mbatata za urojo huna haja ya kwenda na chombo chako kwani mifuko ya plastiki ipo. Ukishindwa kumaliza biriani yako hotelini, huna shaka kwani mifuko ya plastiki ipo, iwapo chakula kwenye sherehe au shughuli za misiba kikabaki na ukataka kwenda nacho nyumbani, mifuko ya plastiki ilikuwa ni karibu kuliko chombo chochote kile.
Wenye kuishi kwenye nyumba za ghorofa nao wakaja na udhuru wao, kuwa maji ni ya shida na kamwe hajafiki kwenye ghorofa zao! hivyo kuwafanya wapate shida kubwa linapokuja suala la kujisaidia iwe haja kubwa au ndogo. Njia mbadala ya karibu ikawa ni kutumia mifuko hiyo ya plastiki kukamilisha haja zao, na baade kuitupa chini.
Watumiao vyombo vya moto nao hawakuwa nyuma katika kutumia mifuko hiyo. Chombo kiliendeshwa hadi kwisha mafuta, baada ya hapo mtu hukimbilia kituo cha kuuzia mafuta na mfuko wake wa plastiki. Baada ya kuuziwa mafuta ya kuyatia chomboni mfuko hulembewa mbali pasipo kujali lolote.
Miaka ikaenda na ustawi wa mifuko ya plastiki ukashamiri, sasa ikawa kila baada ya hatua mbili utembeapo kwa miguu unakanyaga mifuko iliotupwa ya plastiki. Bustani, baraza na viunga vyote vikajaa uchafu wa mifuko ya plastiki. Kelele za mji kuwa mchafu zikapamba moto na Halmashauri ya Mji ikaonekana haifanyi kazi yake ipasavyo.
Serikali ikaliona hilo, semina, kongamano na warsha zikafanyika ili kujua athari za mifuko hiyo, Halmashauri kwa upande wake ikatunga sheria ndogo ya kudhibiti matumizi ya mifuko, ambayo haikuwahi kufanya kazi hata siku moja.
Baada ya miaka kumi na ushee sasa, serikali imeona na kuamua kulivalia njuga tatizo la mifuko ya plastiki nyepesi, na ni baada ya kuja na sheria kali dhidi ya matumizi ya mifuko hiyo. Ikiwa ni pamoja na kutumikia kifungu cha miezi sita jela au faini ya dola za kimarekani 2000.00.
Matumizi ya mifuko hiyo kwa zaidi ya miaka kumi kumesababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ya kisiwa hicho pamoja na bahari ya Hindi. Ikumbukwe kuwa Taka maji ambazo huchanganyika na mifuko hiyo humwagwa kwenye bahari pasipo kuwepo na mchujo wowote ule, hivyo kuwepo na uharibifu wa maisha katika bahari.
Wafanyabiashara kwa upande mmoja wamekuwa mstari wa mbele kupinga kupigwa marufuku kwa utumiaji wa mifuko mepesi ya plastiki kwa kigezo cha serikali kupoteza mapato ilhali mazingira yakitetekemea. Uwamuzi wa serikali ni wa kuungwa mkono kwa dhati kuanzia kwa wananchi hadi kwa wafanyabiashara, kwani unalengo muhimu wa kuhifadhi na kutunza mazingira ya kisiwa chetu!

Tuesday 9 January 2007

Alijenga Baba na kamalizia Mtoto

Leo Wazenj na Watz wanasherekea siku ya Mapinduzi ya Zanzibar ukiwa ni mwaka wa 43. Mapinduzi hayo ambayo lengo lake kubwa ilikuwa kuwapa weusi wengi madaraka ya kujitalawa.

Tokea Mapinduzi kumeshapita awamu zaidi ya sita za uongozi wa ngazi ya juu kabisa visiwani humo, nikiwa na maana marais wa serikali ya mapinduzi, maarufu kama SMZ. Kila awamu iliingia na mambo yake waliyoona ni muhimu kwa wakati wao, zaidi kila awamu inakumbukwa kwa mazuri na mabaya waliyofanya.

Awamu ya kwanza ilikuwa na lengo la kuwawezesha wananchi walio wengi kuwa na maisha bora. Na hii ilithibitishwa na ujenzi wa nyumba bora katika kila pande ya kisiwa hicho. Juhudi za ujenzi huo zilifanyika kwa pamoja kati ya serikali na wananchi. Yaani wote walishiriki kikamilifu katika ujenzi wa nyumba tena wakitumia kila kitu katika kufanikisha azma ya serikali kuwapatia maakazi bora. Utaratibu uliotumika ni kuvunja nyumba ndogo ndogo zilizojengwa kiholela na kujenga nyumba kubwa za ghorofa. Mfano ni majengo ya Forodhani. Kwa upande mwingine nchi za ulaya nazo hazikuwa nyuma kuona wakaazi wa kisiwa hicho wananufaika, Ujerumani nao wakajenga nyumba za maendeleo katika mtaa wa Kikwajuni ambazo zilikuwa na kila kitu ambacho kinahitajika kwa maisha bora.

Awamu iliyofuata ikaona ni vema kuwa na nyumba nzuri vijijini vilevile, hivyo nayo ikajikita katika kujenga nyumba za vijiji huku wao wakitoa mafundi na vifaa vya ujenzi na wananchi wakifyatua matofali. Vijiji vikajengwa na wananchi wakahamia.

Awamu mbili zikapita pasipo kujishughulisha kabisa na masuala ya ujenzi wa nyumba, licha ya kuwepo na matatizo na kasoro nyingi katika ujenzi wa nyumba katika awamu zilizopita. Mojawapo ya matatizo ni kutomalizika kwa ujenzi wa Nyumba za Michenzani na baadhi ya nyumba za vijiji kukosa wakaazi. Aidha matatizo mabaya ya matumizi ya nyumba hizo na uchakavu wa nyumba. Mbaya zaidi ni kwa wale ambao walivunjiwa vibanda vyao kupisha majengo hayo waliendelea kusota pasipo kujua ni lini watanufaika na nyumba bora.

Awamu ya tano iliingia na aina mpya ya ujenzi wa nyumba, ambao uliitwa nyumba za mkopo nafuu, lengo likiwa ni ujenzi wa nyumba za kisasa kwa kuwauzia wananchi hasa wafanyakazi wa SMZ ambao wengi wao walikuwa hawana nyumba. Serikali ya Uchina ikajitutumua na kujenga nyumba za mkopo nafuu. Kasheshe ikaanza wakati wa ugawaji wa nyumba hizo, malengo yakapindishwa na waliopata wakapata na waliokosa wakakosa, malalamiko yakazidi na serikali kama kawaida yake ikaendelea kutoa ahadi kuwa zitajengwa zingine. Zaidi awamu hii ikachungulia na kule kwenye mabaki ya ujenzi wa nyumba za Michenzani. Wakajipanga na kumalizia block moja, wanainchi wakapata nyumba, kama vile haitoshi kukawepo na malalamiko kuwa nyumba nyingi wamepewa watu toka kisiwa cha pili.

Kuingia kwa awamu ya sita kukabadili kidogo sura ya ujenzi wa nyumba, wao wakaona ni bora kumalizia majengo ya Michenzani na kuwapa wale waliovunjiwa nyumba zao karibu miaka therathini na ushee! Wakawata watu hao kuwa wavumilivu kwani serikali haina fedha za kutosha ila nyumba zitamaliziwa.
Hapa sio kama zamani ambapo wananchi walishiriki ujenzi wa nyumba hizo. Sasa ikawa ni kazi ya serikali pekee kumalizia nyumba hizo. Pengine wananchi walishachoka kuisaidia serikali yao. Sijui.

Umaliziaji wa nyumba za Michenzani utakuwa ni furaha ya pekee kwa Rais Aman Abeid Karume. Kwani nyumba hizo zilijengwa na baba yake ambae alikuwa ndio rais wa kwanza wa SMZ. Pengine Karume ameshawishika kumalizia nyumba hizo ili kukamilisha ndoto za baba yake ambae alitaka kuona kuwa wananchi wake wanaishi katika nyumba zilizo bora kabisa. Aidha ni kuondoa kero za wale ambao walivunjiwa nyumba zao kwa mategemo ya kuishi kwenye nyumba bora, na kujikuta wakisubiri kwa zaidi ya miaka arobaini.

Mwisho napenda kuipongeza SMZ kwa kufikisha miaka 43.

Sunday 31 December 2006

Mahakama za Zenj na Matatizo ya Ubabe

Mahakama za zenj katika ngazi zote kuanzia mahakama ya wilaya hadi mahakama kuu ya rufaa zimekuwa zikukutana na wababe ambao hupinga maamuzi ya mahakama hizo kwa muda mrefu sasa.

Tukio la hivi karibuni huko Kibeni katika mkoa wa Kaskazini linathibitisha kuwa maamuzi mengi ya mahakama yamekuwa hayakubaliwi na wanajamii na hasa yale ambayo yamekuwa yakihusisha ujenzi wa nyumba.

Zipo kesi nyingi kuhusu migogoro ya ardhi katika Zanzibar, kesi hizi nyingi zimetokana na kutokuwepo na uwazi katika sheria ya ardhi ya mwaka 1985. Kwa ufupi ardhi yote ya Zanzibar ni mali ya serikali na sio vipando katika ardhi hiyo. SMZ ndio yenye jukumu la kupanga na kugawa ardhi visiwani humo, na kutoa umiliki wa ardhi kwa mtu binafsi, taasisi, mashirika n.k

Kwa upande mwingine serikali hiyo hiyo imekuwa ikitambua baadhi ya hati miliki za ardhi ambazo zilitolewa kabla ya mapinduzi ya Zanzibar(1964) mwa madai kuwa ardhi hizo hazikuwahi kutaifishwa na kuwa mali ya serikali au zimetiwa wafku hivyo serikali haiwezi kuzitaifisha...! Sasa unaposema kuwa ardhi yote ya Zanzibar ni mali ya serikali huku ukijua kuwa sio kweli maana yake ni nini? ka si kupotosha ukweli na kujenga mazingira ya dhuluma!

Matatizo mengine ambayo yanachangia kuwafanya wananchi kuwa wababe dhidi ya maamuzi ya serikali na vyombo vyake, ni kutojulikana kwa wigo za kiutawala visiwani humo. Haijulikani ni wapi ardhi ya serikali inaanzia na wapi inaishia, hata hizo wizara zimekuwa kimya kuelimisha wananchi juu ya suala zima la ardhi.. Wananchi wameachwa kwenye giza huku watawala wakijua hilo pasipo kufanya lolote za ya kukurupuka pale yanapotokea matatizo ya ardhi kwa kutoa amri kubwa kubwa.

Ubabe wa wananchi katika kupinga Hukumu za Mahakama umetokea huko Shakani katika wilaya ya Magharibi mkoa wa Mjini/Magharibi na sasa zimehamia katika mkoa wa Kaskazini. Hii yote ni kwa sababu SMZ imeshindwa kusimamia sheria zake. Iwapo serikali hiyo ingekuwa wazi na hasa kwenye eneo la ardhi lenye migogoro mingi, hapana shaka kusingekuwepo na matatizo haya ya baadhi ya watu kukejeri na kupuuza amri za mahakama.

Kingine watendaji wa SMZ, kwa kujua mapungufu ya serikali wamekuwa ndio mashawishi wakubwa wa kuwepo kwa migongano ya ardhi. Aina hii ya undumilakuwili inatisha na inapaswa kufanyiwa kazi

Friday 29 December 2006

Watanzania wanapokutana

Mwaka huu unaokwisha kuwekuwepo na matukio mbalimbali yaliyoweza kukutanisha watanzania toka zaidi ya mji mmoja.. hapa chini ni mojawapo ya matukio hayo