Saturday 20 September 2008

Jumba la Maajabu- Beit al Ajaib - House of Wonders....Ni kwanini likaitwa hivyo?



Ni rahisi kuliona unapoingia Zanzibar kwa njia ya bahari. Ni jumba lenye historia ndefu sana katika kisiwa cha Zenj. Leo hii Jumba hilo lenye zaidi ya nguzo 40 linatimiza miaka 125 tokea kujengwa kwake. Mengi yamelikuta jumba hilo kiasi cha kuwa mojawapo ya vivutio vya utalii katika Zanzibar.

Katika kusherehekea miaka 125 ya Jumba hilo ni vema kujikumbusha historia yake na umuhimu wake katika historia ya Zanzibar. Ubunifu wa jumba hili ulifanywa na askari wa meli toka Scottland na lilijengwa na surtan Barghash bin Said katika mwaka wa 1883, kwa ajili ya ofisi yake. Zaidi matumizi ya jumba hilo yamekuwa yakibadilika kadiri miaka ilivyokuwa ikienda na jinsi tawala zilivyokuwa zikibadilika visiwani humo.

Matumizi ya jumba hilo kati ya mwaka 1870-1888(miaka 120 nyuma)ilikuwa ni kwa ajili ya sherehe za kitaifa, kumbuka wakati huo Zenj ilikuwa chini ya utawala wa kisultan... Hadi kufikia mwaka 1913 Waingereza walilifanya jumba hilo kuwa ofisi ya serikali za mitaa. ofisi hizo zilidumu hadi wakati wa uhuru na baadae mapinduzi ya Zanzibar mwaka 1964. Kati ya mwaka 1964 na 1977 Jumba hilo maarufu lilitumika kama jumba la kumbukumbu za ASP na SMZ kwa ujumla... Kwa mfano ndio ilikuwa sehemu pekee ya kuweza kuona magari ya Rais wa kwanza wa Zanzibar Marehemu Abeid Karume.

Ilipoundwa CCM mwaka 1977, Jumba hili liliendelea kutumika kama makumbusho ya ASP na taifa na kama ofisi ya CCM, hali ya jumba haikuwa ya kuridhisha sana pamoja na kuwa na historia ndefu.


Kuja kwa mamlaka ya hifadhi na uendelezaji mji mkongwe kulifungua ukurasa mpya wa hifadhi ya mji mkongwe hii ilikuwa katika miaka ya mwisho ya 1988 hadi mwaka 1994 ambapo sheria ya mamlaka ya hifadhi na uendelezaji mji mkongwe ilipopata baraka za Baraza la wawakilishi na siginecha ya prezidenti.. Mwaka 1992 nilipata kufanya kazi na UNDP kaatika kukarabati Jumba hili na ni hapo nilipopata nafasi ya kuweza kuvinjari jumba hilo kwa mapana na marefu... ni wakati ambapo nilipenda kujua ni kwa nini jumba hilo likaitwa la maajabu, ni wakati ambapo nilipenda zaidi fani yangu ya ujenzi na nilikuwa na kila raha nafuraha ya kushiriki katika matengenezo/ukarabati wa jengo hilo...

Moja ya sifa kubwa ya ya jumba hili ni vita vilivyodumu kwa muda mfupi kabisa katika historia ya vita duniani! Vita hivi vilitokea mwaka 1896, na baada ya vita hivi ndio picha halisi ya jumba hilo kwa leo inavyoonekana. Hii ni baada ya kuunganisha mnara wa saa uliokuwa mbele ya jengo hilo na jengo lenyewe.

Lakini ni kwa nini likaitwa jumba la maajabu?... Wataalamu wa histori ya Zenj wanasema umarufu wa jengo hilo umejengwa kwa sifa zifuatazo;-
1. Ni jumba la kwanza Afrika ya Mashariki kuwa na Umeme.
2. Ni jumba la kwanza Afrika ya Mashariki kuwa na lifti( elevator)
3. Ni jumba la kwanza Afrika ya Mashariki kuwa na mfereji ndani ya nyumba( Bomba la maji)

Lakini kwa nini Jumba hilo sio maarufu sana miongoni mwa wakaazi wa visiwa hivyo? Hii inatokana na imani kuwa katika nguzo zaidi ya arobaini za jumba hilo ni makaburi ya watumwa waliozikwa wakiwa hai...

Thursday 18 September 2008

Ndoto inapoyeyuka....


Kwa muda mrefu kumekuwepo na uvumi wa kuwepo kwa mafuta katika visiwa vya Zanzibar, hii ni kutokana na chunguzi mbalimbali zilizowahi kufanyika katika visiwa hivyo katika nyakati tofauti. Uvumi huo kwa kiasi uliweza kuwafanya Wazenj waanza kutembea vifua mbele wakiwa na imani siku moja itafika na mafuta yatachimbwa katika visiwa hivyo katika kiwango cha biashara. Hii ilipelekea hata serikali ya muungano kuingiza kinyamela suala la gesi asilia na mafuta katika mambo ya muungano, na kufanya neema hiyo kama itakuwepo basi itakuwa ni ya muungano.

Taarifa za hivi karibuni kuwa kuna uwezekano mdogo wa kuwepo kwa mafuta hayo kumesababisha Wawakilishi kutoamini masikio yao toka kwa mtaalamu wa uchunguzi wa mafuta.... Kwa maelezo zaidi soma hapa

Monday 15 September 2008

Ngoma Afrika Band na Ziara yao Ulaya...









Bendi ya mziki wa dansi ya The Ngoma Africa inayoongozwa na mwanamziki nguli Ebrahim Makunja alimaarufu Ras Makunja hilifanikiwa kuufunga mtaa mrefu katikati ya jiji la mji mashuhuri wa Hamburg,katikati ya eneo maarufu hamburg-Haltona,
kulikuwa pata shika ya Nguo Kuchanika wakati bendi hiyo mashuhuri kwa kuwadatisha washabiki hakili na mziki wao wa dansi "Bongo dansi" kutoka Tanzania ukiwa unarindima
Live katikati ya mji katika tamasha kubwa la aina yake Afrika-Festival.

Hilikuwa majira ya saa 2.30 usiku wakali wa mziki wa dansi barani ulaya "The Ngoma Africa band walipanda jukwaani na kuanza kuporomosha nyimbo zao za kiswahili zilizo sindikizwa na mdundo mkali wa dansi ! mziki ambao uliweza kuwazoa mashabiki kwa kasi
ya aina yake na kuwatia kiwewe maelfu ya washabiki katika tamasha hilo.

*Ni Ras Makunja na Bendi ya The Ngoma Africa !
siku hiliyofuatia 30-08-2008 wakali wetu hawa walipanda jukwaa kubwa katikati ya
mji wa Krefeld,katika onyesho kubwa la wiki ya mwafrika (Africa Week) huko nako kuwa
patashika washabiki wamataifa mbali mbali wakiwa wamechanganyikiwa na mdundo wa
dansi wa Tanzania,jukwaa lilikuwa limezungukwa na walinzi wenye suti na miwani meusi,
Ras Makunja na kikosi chake wakiwa jukwaani na kuhakikisha mdundo huo unawamtingisha kila mtu.

Bendi hiyo ambayo imefanikiwa kuwanasa washabiki wa ulaya na mziki wao wa dansi
kutoka bongo Tanzania,inasemekana ndio bendi pekee ya mziki wa dansi iliyoweza kugusa hisia za kila mshabiki,si watoto wala wakubwa,vijana kwa wazee,wake kwa waume,wazungu na weusi hili mradi dansi lao linatingisha.

Taarifa hii imeletwa kwa hisani kubwa na Msema Kweli

Sunday 14 September 2008

Madawa ya kulevya na Zenj...Watoto matatani!




Matumizi ya madawa ya kulevya huko Zanzibar sasa yamechukua sura mpya ambayo ni mbaya sana na ya kutisha katika historia ya matumizi ya madawa hayo Visiwani humo. Athari za mwanzo kwa jamii ya visiwa hivyo ilikuwa ni pamoja na kuvunjika kwa ndoa, umalaya na wizi. Hatua ya sasa ni kuambukiza watoto wadogo virusi vya ukimwi kwa kuwachoma sindano zenye damu isiyo salama. Huu ni unyama wa aina yake kutokea huko visiwani.

Hadi kufikia mwaka 2001, Zanzibar ilikuwa tayali imepata umaarufu mkubwa wa kuwa bandari ya kupitishia madawa ya kulevya. Umaarufu huu ulisadikiwa kufunika hata umaarufu wa soko la watumwa uliotokea miaka mia mbili iliyopita. Ukuuaji wa biashara ya ya madawa ya kulevya katika Zanzibar ulikwenda sambamba na uporomokaji wa bei ya karufuu katika soko la dunia na kupanda chati kwa biashara ya utalii.

Awali, Zanzibar ilikuwa ni pepo ya wasafiri watumiao Bangi. Hii ilitokana na urahisi mkubwa wa kupatikana kwa bangi visiwani humo. Taratibu madawa mengine ya kulevya yalianza kuingia visiwani na kufikia kilele katika miaka ya tisini.

Zanzibar kuwa pitisho kubwa la madawa ya kulevya katika ukanda wa Afrika ya Mashariki, kunahusishwa sana na mabadiliko ya ya kiutawala huko Afrika ya Kusini, ambapo utawala wa kibaguzi ulifikia kikomo. Ulinzi mkali katika bandari ya Mombasa baada ya ulipuaji wa balozi za USA huko Nairobi na Dar es Salaam ni sababu nyingine inayotajwa ya Zanzibar kuwa kimbilio la kupitishwa kwa madawa hayo. Aidha ubinafishwaji wa Uwanja wa ndege wa Zanzibar katika miaka ya mwishoni ya tisini umetajwa kuchangia kwa kiasi kikubwa kukua kwa upitishaji wa madawa hayo katika Zanzibar.

Matumizi ya madawa ya kulevya yamekuwa yakienda pamoja na uongezekaji wa maambukizi ya virusi vya ukimwi. Hii hasa kwa wale wanaojidunga sindano. Uchunguzi unaonyesha kuwa asilimia 46 ya watumiaji wa madawa hayo hushare sindano, huku zaidi ya asilimia 50 wakifanya ngono (group sex na anal sex) ili kupata madawa hayo. Baadhi ya vijana huweza kutumia hadi US$ 240 kwa mwezi kupta madawa hayo.

Matumizi ya sindano yaliweza kuingia katika sura mpya katika miaka ya hivi karibuni, baada ya kuongezeka kwa watumiaji wasio kuwa na uweo wa kununua madawa hayo. Njia maarufu ya "flash blood" iligunduliwa ambapo mtumiaji wenye nazo mfukoni, hujidunga sindano yenye heroin, na akimaliza kijidunga ufyonza damu yake kutumia sindano hiyohiyo na kumpatia asie na uwezo damu yake ilichanganyika na heroin(diluted). Mchanganyiko huu uweza kumpatia nishai asiye kuwa na uwezo wa kununua herion.

Hali ya sasa ni mbaya mno kama si ya kutisha. Kwani watumiaji wa madawa hayo sasa hupita mitaani na kuwachoma sindano watoto wadogo, sindano hizo ni zile ambazo wanatoka kuzitumia kwa madawa yao ya kulevya, hivyo kuwepo na uwezekano mkubwa wa kuwapatia watoto hao maambukizi ya virusi vya ukimwi. Huu ni unyama mkubwa kabisa katika historia ya matumizi ya madawa hayo pamoja na ugonjwa wa ukimwi visiwani hapo. Kwa ufupi wazazi wengi wapo katika hali ya hofu na hasa wale wanoishi katika mitaa yanye vijana wengi wa kubembea, aidha kwa watoto ni adha kubwa mno kwao kwani inabidi kukaa ndani tu kwa usalama wao...