Monday 6 August 2012

Zanzibar International Register of Shipping Kufungwa...


Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje Benard Membe, amesema kuwa ofisi za Zanzibar international register of shipping zilizopo Dubai zinafungwa, aidha meli zote za Iran zilizosajiliwa na ZMA zinafutiwa usajili wake.

Wednesday 1 August 2012

Hassan Nassor Moyo- "Nipo tayali kurudisha kadi ya CCM"

Awataka Vijana kuendelea na harakati za ukombozi wa nchi ya Jamhuri ya Watu wa Zanzibar

Mzee Hassan Nassor Moyo leo amefanya mkutano na waandishi wa habari katika ukumbi wa mikutano wa Rumaisa Hotel Malindi Mjini Zanzibar, kujibu hoja mbalimbali zilizo zagaa nchini.

Katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Vijana wa Umoja wa Kitaifa na wanafunzi wa Vyuo Vikuu Mzee Moyo alielezea kuwa msimamo wake anaouonesha sasa si kwa sababu kama Serikali imemtenga kama inavyovumishwa na baadhi ya watu.

Aliwataka vijana waendelee na harakati za ukombozi wa nchi kwani wao si wa mwanzo kuendesha harakati za ukombozi wa nchi.

''Fujo hamkuzianza nyinyi vijana vujo tulizianza sisi toka 1970'' alisema Mzee Moyo huku akishangiriwa na vijana.

Alisema vijana wana haki ya kuuhoji Muungano na wala yeye hawezi kuwazuwiya kwani wamewasomesha wao wenyewe ili kuleta maendeleo ya taifa hili.

Akijibu maswali yaliokuwa yakiulizwa na waandishi wa habari Mzee Moyo alisema yeye ni Mzaliwa wa Zanzibar na hajapata kuomba uraiya wa Zanzibar ila wapo wana CCM hawajazaliwa Zanzibar na wameomba uraiya wa Zanzibar mwaka 1963.

Katika maelezo yake ya awali Moyo alisema hawezi kuyumbishwa na CCM ati kwa kudai Mamlaka kamili ya Zanzibar na kudai Muungano wa Mkataba.

''Hawa Wana CCM wanaodai kuwa turudishe kadi za CCM ni wana CCM uchwara hakuna mwana CCM kindakindaki aliedai sisi turudishe kadi za CCM'' alisema Mzee Moyo huku akiendelea kusema kuwa Ali Ameir si muasisi wa Mapinduzi wala si Muasisi wa Muungano na hajawahi kuwa hata Memba wa Baraza la Mapinduzi''

Nao Vijana wa Umoja wa Kitaifa na Wanafunzi wa Vyuo Vikuu walimuhakikishia Mzee Hassan Nassor Moyo kuwa wapo wapamoja nae na kama atarudisha kadi ya CCM nao watarudisha kadi hizo na kumfata atakapo elekea.

Tayari Vijana wa Umoja wa Kitaifa wamekwisha towa tamko lao la indhari dhidi ya wana CCM wanaowakaripia na kuwatukana Wawakilishi pamoja na Wana CCM wanaotowa mawazo ya Muungano wa Mkataba na kuonya kuwa hali hiyo itahatarisha mchako wa Katiba Mpya.

Jamii Forums

Monday 30 July 2012

"Kuna Harufu Chafu CCM Zanzibar" - Ameir

Mwanasiasa Mkongwe Zanzibar Ali Ameir Mohamed, amesema wakati umefika kwa viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi kuwachukulia mapema hatua za kimaadili na kinidhamu wanachama,Wawakilishi na Wabunge wa chama hicho wenye mwelekeo hasi.

Ameir ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa zamani wa CCM Zanzibar na Mbunge wa zamani wa Donge, alisema hayo kupitia mahojiano maalum yaliyofanyika Kijijini kwake huko Donge Mbiji Zanzibar juzi.

Alisema kuwa kuendelea kuwavumilia wanachama wa aina hiyo ni hatari kwa mustakabali wa uhai wa chama hicho akiifananisha hali hiyo ni sawa na mfiwa kufuga maiti ya ndugu yake ndani ya nyumba anayoishi.

“Chama cha siasa ni mkusanyiko wa kundi la watu wanaokubaliana kisera, kiitikadi na kimfumo hivyo anayejitokeza akipingana na masuala hayo hapaswi kubembelezwa au kuonewa muhali”,alisema Ameir ambaye pia amewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani Tanzania.

Alisema kiongozi, mwanachama, mbunge au Mwakilishi anayepingana na sera ya msingi ya chama chake analazimika kujitoa ili kuonyesha msimamo wa hisia zake.

Ameir anasema anaamini kuwa taratibu za kikanuni na kikatiba ndani ya chama chake zitafutwa ili kusafisha hewa chafu inayoonekana kutanda.

“Kila mwanachama au kiongozi ana wajibu na haki ya kutambua chimbuko la historia ya vyama vya TANU na ASP, muundo wa Muungano na harakati zilizoleta Mapinduzi mwaka 1964, asiyekubaliana na ukweli huo nadhani hatoshi kubaki na kuwa mtetezi wa sera za CCM kwa uhai wake”.Alisikika akisema

Aidha mwanasiasa huyo ambaye ni mmoja kati ya wajumbe walioshiriki kuandaa mchakato wa uundwaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar, alieleza kuwa yeye anaamini kuwa taratibu husika kupitia vikao vya katiba vya CCM zitafuatwa.

Ameir alieleza kuwa kumejitokeza baadhi ya wanasiasa Zanzibar wanaojigamba kuwa wao ni waasisi wa TANU na ASP wakati ni wazee wa CCM na kwamba si haki yao kujiita ni wana Mapinduzi kinyume na ukweli ulivyo. Alisema waasisi wa Mapinduzi ya Zanzibar, wanafahamika kwa majina yao na kwamba anayejitokeza sasa na kudai yeye ni miongoni mwao, ni sawa na mtu anayejipaka damu ya ng’ombe aliyechinjwa na wengine.

“Wana Mapinduzi wa Zanzibar wamebaki wawili hadi sasa,wote sasa ni wazee, Ramadhani Haji Faki na Hamid Ameir Ali, anayethubutu kunyoosha kidole chake na kujiita muasisi wa Mapinduzi, anajivika kilemba cha ukoka”Alisema Ameir.

Alipinga jina la Hassan Nassor Moyo kuwa miongoni mwa waasisi wa ASP na kuwa mmoja kati ya wanamapinduzi kwamba hakuwemo katika harakati za kukiasisi chama hicho wala hakujua siku ya kufanyika Mapinduzi ya 1964 kwa mujibu wa maelezo ya wazee wenzake.

“Moyo ninamheshimu sana, ni mkubwa kiodogo kwangu kiumri ,alikuwa katika Trade Union, hakuwa mwanasiasa aliyeshiriki kukiasisi chama cha ASP,wenzake wanatueleza hata siku yaliofanyika Mapinduzi ya umma hakuijua”Alisisitiza

Akizungumzia kujitokeza kwa Mzee Moyo anayeonekana kutaka Muungano wa mkataba kinyume na sera ya CCM kinachofuata Serikali mbili chini ya Katiba.

Ameir alisema wajumbe hao kufika kwao ndani ya BLW kunatoka na chama cha siasa hivyo matamshi yao hayapingani na sera hiyo ila wanavutana na mfumo wa chama chao.

‘Mzee Moyo nijuavyo ni mwana Muungano wa kikwelikweli, asili yake upande mmoja ni Ruvuma Tanganyika na upande wa pili hapa Zanzibar, anapobeza Muungano huu unaotokana na matokeo ya Mapinduzi na Uhuru wa nchi zetu, sidhani kama anaamua kuafikiana na misimamo tuliokuwa tukipingana nayo kabla ya 1961 na 1964 ”Alisema Ameir.

Kauli hii inakuja wakati kukiwa na katika kampeni kubwa ya kutaka Zanzibar kujitenga katika Muungano wakishirikiana na Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara, (JUMIKI) hali iliyosababisha vurugu za makanisa na baa kuchomwa moto Zanzibar.

Mwinyi Sadallah

Friday 27 July 2012

"Kuitetea Zanzibar Katika Muungano." Balozi Ali Karume


Mtu yoyote ambae anadai kuitetea Zanzibar katika Muungano, hawezi wakati huo huo kudai Muungano uvunjike. Iwapo Muungano utavunjika, hiyo Zanzibar utaiteteaje katika Muungano ambao umeshavunjika? Lazima kuitetea Zanzibar katika mfumo wa Muungano ambao unatoa haki sawa kwa nchi mbili ambazo zimeungana. Mwanzo wa haki hizo ni katika kuongoza Muungano kwenye safu zote za Serikali ya Muungano, kuanzia ngazi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Nchi mbili zikiungana huwa zinasaka "Equity" kwenye huo Muungano. Uwiano wa haki huleta usawa kwa pande zote mbili na kuchelea upande mmoja kujihisi wametawaliwa au wamemezwa. Kujihisi au kuwa na hesia ya kutawaliwa huleta unyonge wa kuhisi kuna ukosefu wa utetezi; maana kwenye utetezi kamili, hakuna kupunjwa, kunyanyaswa, au kuonewa. "In politics, perception is everything". Kwenye siasa, kilakitu hutokana na hesia. Ukihisi unadhulumiwa, huwachi kulalamika.

Kwenye nchi zinoungana kisiasa, tatizo la kwanza ni kupanga safu ya uongozi utoridhisha sehemu zote za Muungano. Mara nyingi, katika kuepuka vurugu za kuchagua Rais mpya wa Muungano, mapendekezo ni kwamba Rais wa nchi moja ndie awe Rais mpya wa huo Muungano. Hii humaanisha kwamba Rais wa ile nchi nyengine awe Makamo wa Rais, ili wale Marais wawili kabla ya Muungano, waongoze serikali ya Muungano kwenye safu ya Rais na Makamo wake. Pia, humaanisha kwamba baada ya kipindi au vipindi muafaka, na yule Makamo au kiongozi mwengine kutoka nchi yake, aweze kuongoza kwenye safu ya Urais wa Muungano. Na upande wa pili wa Muungano utowe Makamo wa Rais.

Katiba ambayo tumepania kuibadili, imetamka wazi kwenye hilo, na watetezi wa Zanzibar hilo wamelifurahia. Katika Katiba mpya, bora hilo libaki, na katika kutilia mkazo "Equity" na uwiano utaochelea migogoro na malalamiko ya kuelemewa, ni bora Katiba itamke wazi juu ya suala la kupishana na kuwepo zamu kwenye Urais na vyeo vyengine vya juu.

Kila Katiba huwa na Yaloagizwa, Yaloelezwa, na Yanotegemewa kutokana na itikadi. "Traditions" ni kitu muhimu katika uteuzi wa viongozi, na katika Muungano ni lazima kujenga itikadi ya kuteua viongozi kutoka pande zote mbili. Watetezi wa nchi zao ni lazima kusimamia hilo. Lazima kuwe na "Deliberate attempt" Jaribio la makusudi na la dharura kutoa zamu kwenye uongozi, ilimradi watoteuliwa wakidhi sifa zinotegemewa. Hayo yamefanyika katika historia ya Muungano wetu, na sioni kwanini iwe mwiko kuirejea historia hiyo. Katika demokrasia, wengi wape kutokana na wingi wa kura, na tusipofanya jaribio la makusudi na la dharura kuwapata viongozi wa safu za juu kutoka sehemu zote za Muungano wetu, basi wengi watatoka sehemu moja na kuendelea kujenga hisia kwamba sehemu moja ya Muungano imeelemewa. Ndio maana kuna wengine wanajihisi wamesakamwa na wanaomba waachiwe wapumuwe.

Tunapopata fursa ya kuchagua viongozi wa juu, kama vile Rais wa Jamhuri ya Muungano, ni vyema wale wanaodai kuitetea Zanzibar wawe mstari wa mbele katika kumpata mgombea bora kutoka Zanzibar na kumsaidia ili ateuliwe. Hili ni muhimu kufanyika, hasa baada ya uongozi wa ngazi ya juu kabisa kukamatwa na viongozi kutoka sehemu moja ya Muungano kwa muda mrefu. Mwenyekuitetea Zanzibar kikweli kwenye hilo, hawezi kudai kwamba hakuna Mzanzibari anofaa kwenye wadhifa huo. Anayechukua msimamo huo, anachangia Zanzibar kusakamwa na kukosa pumzi. "Tuacheni tupumuwe" aambiwe na yeye pia. Mzanzibari anayewakataa wagombea wote kutoka Zanzibar na kumuunga mkono mgombea kutoka bara kwa hali na maji aendelee kutawala, asidai kwamba anaitetea Zanzibar na kudai "Tuacheni tupumuwe". Kwani kwenye kusakamwa na Bara, na yeye si alichangia? Ya yeye alichangia katika kutukosesha pumzi, ilimradi yeye apumuwe vizuri zaidi baada ya kutuuza. "We were sold down the river to the highest bidder by our own kith and kin". Kikulacho kinguoni mwako.

Umefika wakati Watanzania tuwe makini sana. Tutetee haki zetu kwenye Muungano wetu, na tujizatiti katika kuepusha "Dhana" ya aina yoyote ya kwamba upande mmoja wa Muungano wetu, umeelemewa. Tuunde Katiba mpya itoondowa dhana ya kutawaliwa na tutoe fursa kwa pande zote ziachwe zipumuwe. Tukishindwa kwenye hilo, tutajitakia maradhi. Na wahenga walisema "Maradhi ya kujitakia; Mtu hapewi pole".

Balozi Ali Abeid Amani Karume.