Athari za Wizara kung'ang'ania madaraka....
Wakati mamilioni ya Watanzania leo hii wanasherekea siku ya uhuru wa Tanganyika, Huko Zanzibar, suala la uchafuzi wa Mazingira limechukua sura mpya. Hii ni baada ya wizara ya maji, ujenzi, nishati na ardhi kutangaza kuwa hapatakuwa na ruhusa kwa mwekezaji kujenga hoteli pasipo kuwa na water treatment plant na sehemu ya kuchomea taka ngumu ( incinerator).
Tatizo la utupaji wa taka ngumu na taka maji katika ukanda wa hoteli za kitalii na hasa maeneo ya mashariki na kaskazini ya kisiwa hicho yapo kwa muda mrefu sasa. Hoteli nyingi kubwa na ndogo zimekua zikitupa taka zao kwa njia wanazojua wao wenyewe. Kuna hoteli ambazo zimekuwa zikitupa taka ngumu moja kwa moja baharini, wengine kuzichimbia ardhini na wapo waliokuwa wanazichoma sehemu ya mbali toka katika maeneo yao. Hali kadhalika taka maji zimekuwa zikitupwa moja kwa moja baharini na kwenye maeneo ya karibu na bahari.
Matatizo ya kukosekana kwa mfumo wa utupaji wa taka na hasa nje ya halmashauri ya manispaa ua zanzibar, yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na baadhi ya wizara kung'ang'ania madaraka na hasa kwenye maeneo nyeti ya ardhi na uwekezaji. Kimsingi Mamlaka ya Maji huko visiwani inashughulika na usambazaji wa maji safi tu katika visiwa hivyo, huku jukumu la maji taka likiwa chini ya halimashuri ya manispaa ya zanzibar..ambayo ina eneo dogo tu la utawala. Zaidi hata katika eneo hilo dogo la kiutawala, haina sauti kisheria juu ya usimamiaji wa maji taka katika hoteli ambazo zimejengwa ndani ya Manispaa hiyo. Vyombo vinavyohusika hapo ni ZIPA na Idara ya Upimaji na Mipango Miji. Cha kushangaza hata Idara ya Mazingira imekuwa ikiwekwa pembeni mno kuhusu shughuli nyingi za uendelezaji wa ardhi katika visiwa hivyo.
Baada ya Miaka kumi na sita ya uendelezaji wa Mahoteli ya kitalii katika fukwe za visiwa hivyo pasipo na mfumo wowote wa utunzaji wa mazingira, athari zake sasa zimeanza kuoneka wazi. Hoteli hizo hazina mfumo wowote wa kusafisha maji taka kabla ya kuyamwaga baharini na hakuna sehemu maalumu ya utupaji wa taka ngumu katika maeneo ya hoteli hizo. Kila mwenye hoteli anafanya chochote atakachoweza katika kutupa taka zake.
Haya yote yametokana na baadhi ya wizara kung'ang'ania kila kazi, Kwa mfano jukumu la Idara ya Mazingira katika uwekezaji na katika suala zima la maendeleo hasa katika sekta ya ujenzi halijulikani. ZIPA ikishirikiana na Idara ya Mipango Miji/Vijiji wameshindwa kuonyesha ni kwa nanma gani taka zinazozalishwa kila siku katika mahoteli hayo zitakavyoweza kuhifadhiwa, kutupwa au kutumika tena, na mbaya zaidi haijulikani ni mamlaka ipi inayoshughulikia maji taka nje ya Manispaa ya zanzibar.
Iwapo ZIPA na Idara ya Mipango Miji/Vijiji ndio wanaochukua kodi za uanzishwaji wa mahoteli ya kitalii inawapasa wawajibike na kupanga mfumo unaoeleweka ukusanyaji na utupaji wa wa taka katika Maeneo ya hoteli. Ushirikishwaji wa mamlaka za serikali za mitaa katika maeneo hayo pamoja na idara ya mazingira lazima utazamwe upya.
No comments:
Post a Comment