Uchovu wa SMZ kwenye masuala ya Umiliki wa Ardhi...
Moja ya matatizo makubwa ya SMZ yapo kwenye masuala ya umiliki wa ardhi. Serikali hiyo ina migogoro mingi kuhusu umiliki na uendelezaji wa ardhi licha ya kuwa na sheria ya Mipango miji/vijiji na Ardhi ya mwaka 1985, Baraza la Manispaa ya mwaka 1995 na Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe ya mwaka 1994.
Sheria hizo zote hapo juu zinasimamia uendelezaji na umiliki wa ardhi, aidha Halmashauri za wilaya nazo kwa upande mwingine zimekuwa zikisimamia uendelezaji wa ardhi. Serikali kuu kupitia kwa Masheha wao nao wamekuwa wakijishughulisha katika masuala ya ardhi.
Katika Mahakama zote visiwani humo kumejaa kesi nyingi za madai ambazo zinahusiana na matatizo ya ardhi.
Leo kanisa la Anglikana huko Zanzibar limekumbushia kadhia yao ya kunyang'anywa ardhi yao na kufanyia mabadiliko ya matumizi. Kimsingi eneo ambalo lina mgogoro ni shule ya msingi Mkunazini ambayo kabla ya mwaka 1964 ilikuwa inamilikiwa na kanisa hilo.
Kinachoshangaza ni hatua ya SMZ kupitia wizara zake kuendelea kubadilisha kinyamela matumizi ya eneo hilo toka eneo la shule na Ibada kuwa eneo la biashara, kwa kuruhusu ujenzi wa maduka katika eneo hilo.
Miaka ya tisini kanisa hilo liliwahi kuomba ruhusa ya kukarabati uzio wa eneo hilo ambao ulikuwa unazama taratibu. Uzio huo unaanzia upande wa mbele ya shule hiyo mkabala na barabara ya Benjamini Mkapa. Kibali cha ujenzi wa uzio huo kilichukua muda mrefu hadi kupatikana. Na kiliweza kupatikana baada ya kanisa hilo kutoa malalamiko mengi kuhusu urasimu wa vyombo vya SMZ.
Ucheleweshaji wa upatikanaji wa Kibali cha Matengenezo ya Ukuta wakati ule sasa ninaweza kuuelewa vizuri. Inaoneka Watendaji wa SMZ walishaona kuwa eneo hilo linafaa kwa kujengwa kwa Vibanda na Viduka vya biashara hivyo walikuwa wanasita kutoa ruhusa ya matengenezo ya ukuta. Na hata walipotoa ruhusa hiyo eneo lilikuwa karibu na shule hiyo halikupewa ruhusa ya ukarabati.
Sasa eneo hilo limejengwa Vibanda vya biashara, na litaendelea kujengwa licha ya maombi ya kanisa hilo kurejeshewa umiliki wa shule hiyo.
Hivi ni nini nafasi ya kuwa na mamlaka ya hifadhi na uendelezaji wa mji mkongwe, iwapo sehemu ambazo zinahitaji kupatiwa hifadhi kutokana na umuhimu wake wa kihistoria, zinashindwa kuhifadhiwa? Kanisa la Anglikana ni muhimu kabisa katika historia ya Zanzibar. Hivyo linatakiwa lipewe nafasi ya ya kuhifadhiwa chini ya Sheria za Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji Mji Mkongwe.
2 comments:
Kibunango!
Hili tatizo la kugombania ardhi limekuwa sugu ktk Jamhuri ya Muungano wa Tz. Lakini yawezekana kabisa chanzo kikubwa cha tatizo hili ni RUSHWA. Corruption yaweza kusababisha sheria ishindwe kufanya kazi na hatimaye kuleta misuguano isiyo kuwa ya lazima.
Mtanzania:
Tatizo la kugombea ardhi lipo, na hasa ardhi mpya... Inapotokea kwenye ardhi ambayo tayali imeshaendelezwa na mamiliki wake wanajulikana na zaidi kwenye eneo ambalo lipo chini ya hifadhi ya Nchi na Kimataifa (Old Stone Town & UNESCO World Heritage City), inabidi kujiuliza sana? Ni rushwa pekee au kuna aina nyingine ya ufisadi...!
Post a Comment