Wazenj na Mechi za Bure...
Tangu kuchukua nafasi ya Ukurugenzi wa wa timu ya Miembeni, Amani Makungu amekuwa akitoa ofa kadhaa kwa washabiki ya soka visiwani humo kwenda kuona mechi bure. Miembeni ni mojawapo ya timu kongwe visiwani, ambayo imewahi kuwa na mafanikio makubwa kisoka miaka ya nyuma, kabla ya kudorora na kupotea katika ramani ya soka hasa kipindi cha ufadhili cha miaka ya tisini.
Timu hiyo ambayo ipo kwenye kitongoji cha Miembeni ambacho kinajulikana sana visiwani humo kwa makasheshe, ilitwaa ubingwa wa visiwa hivyo mara ya mwisho yapata miaka ishirini(1987). Mwaka jana imefanikiwa tena kuchukua ubingwa wa ligi visiwani humo chini ya ukurugenzi wa A. Makungu na kocha Suleiman Mahmoud Jabri.
Ufadhili wa Mkurugenzi huyu umewawezesha wapenda soka na washabiki wengi wa timu hiyo kuweza kuona mechi kubwa ya klabu hiyo bila ya viingilio. Mechi yakaribuni ya bure ni ile ya kombe la mapinduzi ambapo Miembeni iliweza kutwaa kombe hilo baada ya kuifunga timu ya Polisi kwa mabao 2-1. Mechi hiyo ya dezo ilihidhuriwa pia na Mh. Aman Karume Rais Zanzibar.
Wengi wamenufaika na hili, lakini ni vema vilevile kuangalia nini athari zake kwa soka la visiwa hivyo. Baada ya wadhafili wakubwa kujitoa kugharamia timu kubwa huko visiwani, soka la visiwani lilianguka sana, kuanzia katika mechi za ndani hadi za kimataifa. Ukiangalia nyuma kidogo kama miaka kumi iliyopita hasa katika kipindi cha miaka ya 1996-1998, kulikuwa na upinzani mkubwa wa vilabu kutokana na utajili wa wafadhili wao. Timu ambazo zilikuwa zikivuma kipindi hicho ni Mlandege, Malindi na Shangani, ambazo zote zilikuwa chini ya ufadhili wa wafanyabiashara. Timu kama ya Malindi iliweza hata kusajili wachezaji toka Ulaya ya Mashariki na Afrika vilevile. Klabu kama Miembeni, Kikwajuni na Small Simba ambazo hazikuwa na wafadhili ziliporomoka vibaya katika kiwango cha soka visiwani humo.
Lakini nini kilitokea baada ya wafadhili kujitoa kwenye klabu hizo? Ni kufanya vibay kwa timu hizo, kuwepo na migogoro na kadhia zingine. Sasa klabu zinazomilikiwa na asasi za serikali zikanza kuibuka upya. Timu kama KMKM ambayo ilikuwa tishio katika miaka ya 80 ikarudi tena, huku timu ya Polisi ikiibuka na kuchukua ubingwa wa Zenj na kujiwekea historia yake. Mafanikio ya kablu hizi ni kutokana na wachezaji wake kuwa ni waajiliwa wa asasi hizo.
Miembeni inawapasa kutofumba macho katika suala la kuona timu hiyo inabaki kung'ara kama zamani. Ni wajibu wa kila mwanachama, mpenzi na shabiki wa klabu hiyo kukuna kichwa ni kwa namna gani anaweza kuchangia kuona timu hiyo inakuwa na maendeleo endelevu, badala ya kuendelea kumtazama mtu mmoja akifanya kila kitu kwa klabu hiyo kongwe visiwani. Matokea ya ufadhili wa mtu mmoja/mfanyabiashara yapo wazi kwa kablu kadhaa za visiwani humo. Hivyo ni vema kujifunza kutokana na makosa yaliyofanyika katika kablu hizo. Huu usiwe muda wa kuchekelea kuingia uwanjani bure, bali uwe muda wa kuangalia ni kwa vipi timu hiyo itaweza kukaa katika chati ya juu na kufanikiwa kisoka bila ya kutegemea ofa.
1 comment:
Post a Comment